Dar es Salaam. Wadau wa elimu nchini
wameichambua elimu ya Tanzania na kueleza kuwa, tatizo la kuporomoka kwa elimu
ni matokeo ya sera na mifumo mibovu na si uhaba wa miundombinu kama madawati,
vitabu au majengo.
Pia wamesema, Serikali inatakiwa
kulitangaza tatizo la matokeo mabovu ya mitihani ya wanafunzi kama janga
laTaifa, ili liweze kutiliwa mkazo kwa lengo la kushughulikiwa ipasavyo.
Hayo yalisemwa jana katika kongamano
la kujadili mchango wa tafiti huru katika kuboresha elimu ya Tanzania,
lililoandaliwa na Taasisi ya Uwezo Tanzania lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM).
Akitoa mada iliyosema, “ Kwa nini
jitihada zetu za kuboresha elimu hazizai matunda”, Mkuu wa Taasisi isiyo ya
Kiserikali ya Twaweza, Rakesh Rajani alisema kinachotakiwa kuboreshwa ni sera
za elimu , ili kuendana na matakwa ya elimu inayotakiwa kufundishwa kwa
wananfunzi.
“Hapa tatizo siyo uhaba wa walimu,
madawati na majengo’ Tatizo lipo katika mfumo na sera zake, hata tukiboresha
yote hayo bila kuzingatia sera hakuna tutakachovuna,” alisema Rajani
Aliongeza: “Miaka minane imepita kila
mwaka bajeti ya Wizara ya Elimu inaongezwa, lakini matokeo bado ni mabovu,
tunatakiwa kujiuliza wapi tunakosea na kuhoji fedha hizo zinakwenda wapi kama
zinaongezwa na hakuna tofauti.”
Naye Mratibu wa Taasisi ya Uwezo
Tanzania, Zaida Mgalla alisema “Matatizo ya elimu nchini yatangazwe kama janga
laTaifa, tukiendelea kuwapeleka hivyo hivyo tutegemee kupata wataalamu walio
chini ya uwezo.”
Mgalla alisema, Serikali inajivunia
ongezeko la watoto wanaoandikishwa darasa la kwanza, lakini swali la kujiuliza
je, wanakwenda shule wanajifunza?
Kwa upande wake, Profesa Mstaafu
Justinian Galabawa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Elimu, alisema
serikali inatakiwa kutenga vipaumbele vichache vya Taifa, ambavyo itaweza kuvisimamia
na kuvitekeleza.
“Tukiwa na vipaumbele vingi
hatutaweza kuvisimamia, tuisimamie elimu walimu, wanafunzi majengo na
rasilimali zote zinazohusu elimu hata kama ni kidogo zisimamiwe ipasavyo,”
alisema Profesa Galabawa.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment