Picha ya Maktaba ikionyesha siku ya Ufunguzi wa Bunge maalumu la Katiba hapa Tanzania
JUKATA yaandaa maandamano kushinikiza
livunjwe
MWENENDO usioridhisha wa Bunge
Maalumu la Katiba linaloendelea mjini Dodoma umesababisha wanaharakati,
taasisi, vyama vya siasa na watu wa kada mbalimbali kutamani Bunge hilo
livunjwe.
Moja ya taasisi zilizoamua kuvalia
njuga suala la kuvunja Bunge hilo ni Jukwaa la Katiba (JUKATA), ambalo
limejitoza kuwaongoza wananchi wenye uchungu na taifa lao na walio nje ya Bunge
kujitokeza na kuungana katika harakati za kutaka kulivunja Bunge hilo.
Katika mkutano wake na waandishi wa
habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, Jukata imepanga kuandaa maandamano
makubwa ya wananchi kutoka jijini Dar es Salaam hadi Dodoma, kumshinikiza Rais
Jakaya Kikwete alivunje Bunge hilo kwa madai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kimevuruga mchakato wa kupatikana Katiba Mpya.
JUKATA imesema kuwa imeamua kufanya
hivyo kwa kile ilichodai kutoridhishwa na mwenendo na kasi ya Bunge hilo ambalo
tangu Rais Kikwete alipolizindua rasmi, limepoteza mwelekeo kwa kuibua malumbano
na makundi ya kiitikadi yanayopigania masilahi binafsi, huku CCM ikionyesha
dhahiri kutaka kupata Katiba yenye masilahi kwa chama hicho tawala.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mwenyekiti wa JUKATA, Hebron Mwakagenda, alisema
kuwa Jukata itatumia Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwaongoza wananchi katika
harakati hizo.
Ibara hiyo inaelekeza kuhusu mamlaka
ya wananchi, ikiwemo wananchi ndio msingi wa mamlaka ya nchi na serikali
inawajibika kwa wananchi.
Alisisitiza kuwa maandamano hayo ya
kihistoria, yataanzia jijini Dar es Salaam kwenda Dodoma na kuwataka wananchi
wenye uchungu na upotevu wa fedha zinazotumika kwa wajumbe wa Bunge hilo
Dodoma, wajitokeze kuhakikisha Bunge hilo linavunjwa na kutafuta utaratibu bora
zaidi wa kuandika Katiba Mpya.
Mwakagenda alisema kuwa wamefikia
hatua hiyo kwani hawaridhishwi na namna Bunge hilo linavyoendelea kwani
halionyeshi kama linaweza kuwapatia Watanzania Katiba Mpya.
Aidha, alisema kuwa tangu Rais Kikwete
alipolihutibia Bunge na kumshambulia Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji Joseph Warioba, utulivu umezidi kukosekana na imeathiri mwelekeo
wa Bunge hilo na kuzidisha mgawanyiko.
Alimlalamikia Rais Kikwete kwa
kupingana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyoichagua yeye mwenyewe, ambayo
awali alikuwa akiisifia kwamba imefanya kazi nzuri.
“Rais alipewa nafasi ya
kuhutubia Bunge, matokeo yake akainanga
hotuba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ni sawa sawa na kujipinga yeye mwenyewe
na kuwapinga Watanzania waliotoa maoni yao,” alisema.
Mwakagenda alisema hotuba ya Rais
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa, haikupaswa kutolewa na mkuu huyo wa nchi
ambaye kazi yake ni kuliunganisha taifa na kuhubiri amani, upendo na
maridhiano, hasa katika kipindi hiki cha kupata Katiba mpya.
Katika hatua nyingine, Jukata
imebaini kuwa tangu kuanza kwa Bunge la Katiba viongozi wa serikali wamekuwa
wakiwatisha waandishi wa habari kwa kisingizo cha kuwa wazalendo.
“Wao wanawatisha wanahabari kwa
misingi ya kuwa wazalendo na waandike kile ambacho serikali inataka, tunataka
serikali iache vitisho kwa wanahabari ili waweze kufikisha habari kwa wananchi,
ili wakati wa kupiga kura ya maoni, waweze kufanya maamuzi yatokanayo na habari
walizopewa,” alisema.
Aidha, alisema wanalitaka Bunge hilo
kusitisha kutumia kura kama njia ya kufikia maamuzi ya kupitisha katiba, na
kuwataka waige utendaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kikao chao cha
kupitisha kanuni kilivyofanya kazi.
“Uzoefu duniani unaonyesha kuwa
kinachoongoza utengenezaji wa katiba ni hoja, ushawishi, mijadala, muafaka na
maridhiano na si kupiga kura na kuzomeana na kutukanana, upigaji kura
ukiendelea madai ya Katiba mpya yataendelea hata baada ya kupitisha katiba hiyo,”
alisema.
Alisema kuwa Katiba inayotengenezwa
ni ya Watanzania wote na si ya wanasiasa na viongozi, hivyo kitendo cha
wanasiasa na viongozi kuwa na sauti kubwa katika utengenezaji wa Katiba
kumefanya mchakato huo utekwe na wao ambao idadi yao ni asilimia 85.
Mwakagenda alisema kitendo cha
kutumika misimamo ya chama chochote cha siasa katika kutengeneza katiba ni kosa
na kimesababisha mabishano kuwa ya vyama vya siasa na Bunge hilo kugawanyika
kiitikadi na kimisimamo, hasa katika suala la Muungano.
Kelele za kutaka Bunge hilo livunjwe
zimekuwa zikitolewa na watu wa kada mbalimbali, wakiwemo baadhi ya wajumbe wa
Bunge hilo.
Juzi mjumbe wa Bunge hilo, Lekule
Leizer, alipendekeza kwa Mwenyekiti wa Kudumu wa Bunge, Samuel Sitta, kuandika
barua kwa Rais Jakaya Kikwete ili alivunje kama muafaka wa aina gani ya kura
itumike kwenye maamuzi hautapatikana.
“Kamati ya kanuni imefanya kazi hii
kwa shinikizo la kuridhisha pande zote mbili, sasa kama tutaendelea kubishana
hapa bila kupata muafaka tunaomba Rais avunje Bunge turudi nyumbani,” alisema.
Laizer alisema inatia uchungu kuona
wajumbe wakiendeleza mivutano huku wakilipwa posho wakati hakuna kazi yoyote
wanayoifanya zaidi ya kubishana na kuzomeana.
Naye Freeman Mbowe, alishauri suala
hilo lirudi kwenye Kamati ya Maridhiano ili viongozi waridhiane badala ya
kuendelea kupoteza muda kwa kulumbana kwa jambo ambalo hawataweza kufika
mwisho.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment