Saturday, March 22, 2014

Ujerumani yaishutumu Urusi kwa kuigawa Ulaya

Ujerumani Jumamosi(22.03.2014) imeishutumu Urusi kwa kujaribu kuigawa Ulaya wakati mvutano wa mtindo wa Vita Baridi ukipamba moto juu ya mustakbali wa Ukraine baada ya Urusi kulinyakuwa jimbo lake la Crimea.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk mjini Kiev. 

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk mjini Kiev. 
Rudio la onyo hilo kutoka taifa ambapo urafiki wake na Rais Vladimir Putin umestawi wakati akiwa madarakani kwa miaka 14 linakuja wakati kukiwa na juhudi za mataifa ya magharibi za kuimarisha uungaji mkono kwa viongozi wa mpito wa serikali ya Ukraine mjini Kiev ambao waliupinduwa utawala uliokuwa ukiungwa mkono na Urusi mwezi uliopita.

Waziri Mkuu wa Canada Stephen Harper anakuwa kiongozi wa kwanza kutoka kundi la Mataifa Saba yenye Maendeleo Makubwa ya Viwanda Duniani kukutana na rais wa mpito Oleksandr Turchynov mjini Kiev tokea Crimea iitishe kura ya maoni ya kudai uhuru hapo tarehe 16 mwezi wa Machi ambayo ilishuhudia Urusi ikikamilisha rasmi madai yake ya kuingiza Ukraine katika himaya yake hapo Ijumaa.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani ambaye nguvu kubwa ya uchumi wake imetimiza dhima muhimu katika hatua ya Ulaya kukabiliana na msimamo wa kikaidi wa Putin ameonya kwamba mustakbali mzima wa wa bara la Ulaya uko hatarini.

Jaribio la kuigawa Ulaya
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na Rais wa Ukraine Oleksandr Turchynov mjini Kiev.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na Rais wa Ukraine Oleksandr Turchynov mjini Kiev.

Frank- Walter Steinmeier amewaambia waandishi wa habari kufuatia mkutano wake na Waziri wa Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk kwamba " Kura ya maoni huko Crimea ni ukiukaji wa sheria ya kimataifa na ni jaribio la kuigawa Ulaya."
Steimeier amemwambia Yatsenyuk kwamba wamekutana hapo leo hii kwa sababu wanajuwa kwamba hali bado ni tete.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani ameongeza kusema kwamba Ujerumani inataka kuisaidia serikali ya Ukraine inayounga mkono Umoja wa Ulaya "kwa kadri tunavyoweza".

Steimeier pia amempongeza Waziri Mkuu huyo wa Ukraine kwa kutangaza kwamba serikali yake inawajibika kwa wananchi wote wa Ukraine.
Amesema "Umeelezea kwamba haki za jamii ya watu wachache lazima ziheshimiwe ...hizi ni ishara njema ambazo nchi inazihitaji katika hali hii."
Katika ziara hiyo Steimeier pia alikutana na Rais wa Ukraine Oleksandr Turchynov na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambaye alikuwa Kiev kukutana na viongozi wa nchi hiyo kuwahakikishia mshikamano wa kimataifa.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon mjini Kiev.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon mjini Kiev. 

Ziara ya Steinmeier inakuja siku moja baada Ukraine kusaini ibara za kisiasa za makubaliano ya ushirikiano na Umoja wa Ulaya. Yatsenyuk amesema makubaliano hayo ya ushirikiano ni "jambo ambalo mamilioni ya Waukraine walikuwa wakiyatarajia".Pia ametowa wito wa kuwepo kwa ushirikiano mkubwa zaidi wa kijeshi kati ya nchi yake na Umoja wa Ulaya.

Amesema "Inabidi tupatiwe silaha upya na kuimarisha vikosi vya ulinzi vya Ukraine."
Umhimu wa mshikamano
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk mjini Kiev. 
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk mjini Kiev. 

Mshikamano huo wa kidiplomasia yumkini ukatimiza dhima muhimu ya kisaikolojia nchini Ukraine wakati serikali ya nchi hiyo ikikabiliwa na duru mpya za shinikizo la Urusi zenye kujumuisha vitisho vya wazi vya kuusambaratisha uchumi wa Ukraine kwa kupandisha bei zake za gesi na kudai malimbikizo ya malipo ya madeni yake yenye mzozo ambayo nchi hiyo haimudu kuyalipa.

Ishara kuu ya mshikamano huo kutoka Ulaya imetolewa hapo jana mjini Brussels kwa kusainiwa makubaliano ya kuwa na uhusiano wa karibu kati ya Ukraine na Umoja wa Ulaya ambao kukataliwa kwake na utawala wa Ukraine uliokuwa ukiungwa mkono na Urusi ndiko kulikopelekea kuzuka kwa maandamano ya miezi mitatu yaliyosababisha maafa na ambayo ndio yaliyopelekea kuanguka kwake hapo tarehe 22 mwezi wa Februari.

Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk akibadilishana majalada na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy wakati wa kusaini makubaliano ya ushirikiano na Umoja wa Ulaya upande wa kisiasa mjini Brussels. 
Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk akibadilishana majalada na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy wakati wa kusaini makubaliano ya ushirikiano na Umoja wa Ulaya upande wa kisiasa mjini Brussels. 

Makubaliano hayo yanaiweka Ukraine kwenye hatua madhubuti kuelekea kujiunga na Umoja wa Ulaya ambapo waandamanaji waliokuwa wamechoshwa na rushwa na kudhibitiwa na Urusi walikuwa wakiipigania na ambao Putin alikuwa akiihofia kwa sababu ya mauti iliyokuwa ikiyaashiria kwa kwa ndoto yake ya kuunda himaya itakayoongozwa na Urusi ya majimbo ya zamani ya Muungano wa Kisovieti.

Makubaliano hayo yanatazamiwa kufuatiwa na yale ya kiuchumi miezi michache baadae ambayo yataiondolea moja kwa moja vikwazo vya biashara Ukraine na nchi hiyo kutakiwa kufanya mabadiliko ya miundo ya taasisi zake yanayohitajika kuchangamsha uchumi wa nchi hiyo uliokuwa katika hali ya kuzorota kwa miongo miwili.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa/Reuters
Mhariri : Bruce Amani

Chanzo: DW Swahili

No comments: