Na Zitto Kabwe, MB
Wiki ya Machi 18 - 22, 2014 ilianza
kwa siku ya Jumanne Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji
Joseph Sinde Warioba aliwaslisha rasmi Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania katika Bunge Maalumu la Katiba. Wiki hiyo imeishia kwa siku ya
Ijumaa Rais wa Jamhuri ya Muungano ndugu Jakaya Mrisho Kikwete kutoa hotuba kwa
Bunge Maalumu. Hotuba zote zimepokelewa kwa hisia tofauti kulingana na msimamo
wa kila mtu kuhusu hoja inayoonekana ni kubwa
kuliko zote katika mchakato wa
kuandika Katiba Mpya - Muundo wa Muungano. Wale wanashabikia muundo wa Serikali
Tatu, walifurahishwa mno na hotuba ya Jaji Warioba. Wale wanaoshabikia muundo
wa Serikali mbili walifurahishwa mno na hotuba ya Rais Kikwete. Sikufurahishwa
na hotuba zote mbili.
Nitaeleza.
Moja, hotuba zote mbili zilichukua
muda mrefu zaidi kuelezea sura moja tu ya Rasimu ya Katiba nayo ni sura ya Sita
inayohusu muundo wa Jamhuri ya Muungano kana kwamba Katiba hii inahusu suala
hilo tu. Ni dhahiri suala hili ni kubwa na muhimu kwani linahusu uhai wa Dola
yenyewe na siwezi kubeza. Hata hivyo masuala kama Haki za Raia ni muhimu zaidi
kwani hata uwe na muundo wa namna gani wa muungano au hata muungano wenyewe
kuvunjika, bila ya kuwa na haki za msingi za raia kwenye katiba katiba hizo
zitakataliwa tu na wananchi. Huu mtindo unaozuka wa kudhani muundo wa muungano
ndio mwarobaini wa matatizo ya ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka,
ubadhirifu, umasikini, elimu ya hovyo, afya dhaifu, utatufikisha pabaya na hata
kurudi tena kuandika katiba kudai haki hizo. Jaji Warioba na Rais Kikwete
wameshindwa kuruka kiunzi cha kwamba Katiba ni zaidi ya Muungano.
Pili, wote wawili Rais Kikwete na
Jaji Warioba wamejenga hoja zao kuhusu miundo ya Muungano wanayopendekeza au
kuunga mkono kutokana na misingi ama ya 'malalamiko' au 'hofu'. Jaji Warioba
aliorodhesha malalamiko 11 ya upande wa Zanzibar dhidi ya Muungano na
malalamiko 10 ya upande wa bara. Kimsingi malalamiko yote ya upande wa bara
yanazaliwa na vitendo vya upande wa Zanzibar isipokuwa lalamiko namba vii linalohusu
kupotea kwa utambulisho wa Tanganyika katika muundo wa Muungano.
Jaji Warioba anajenga msingi wa
pendekezo la Tume yake kutokana na kujibu malalamiko au maarufu kero za
Muungano na anasema
"....muundo wa Serikali mbili
hauwezi kubaki kwa hali ya sasa. Muungano wa Serikali mbili waliotuchia waasisi
siyo uliopo sasa...... waasisi walituachia Muungano wa Nchi Moja yenye Serikali
mbili, na siyo Nchi Mbili zenye Serikali Mbili". Nukuu hii niliipenda
kuliko zote katika Hotuba ya Mzee wangu Warioba.
Rais Kikwete alijenga msingi wa maoni
yake kwenye hofu za kuwa na Serikali tatu. Hofu hizo ni pamoja na gharama za
kuendesha Muungano, kuzuka kwa hisia za Utaifa wa Utanganyika na Uzanzibari,
uwezekano wa Muungano kuvunjika kwa kushindwa kuhudumia majeshi na hata Jeshi
kuchukua Nchi ikipidi na kutupilia mbali katiba na Serikali ya Muungano
kutokuwa na Rasilimali zake. Rais alisema 'Serikali ya Muungano ni egemezi na
tegemezi' nukuu ambayo niliipenda kuliko zote katika Hotuba ya Mzee wangu
Jakaya Kikwete.
Rais Kikwete hakuniridhisha kabisa
namna ya kumaliza kero za Muungano kwa muundo uliopo sasa kwani muundo huo
umeshindwa kuzimaliza kwa takribani miaka 50 tangu Muungano uundwe. Haiwezekani
muundo uliozalisha kero lukuki ndio utarajiwe kuzimaliza kero hizo. Kwa
vyovyote vile ni lazima kuwa na muundo mpya lakini kiukweli ni lazima muundo
huo mpya ujibu hofu alizoeleza ndugu Rais maana ni hofu za kweli.
Jaji Warioba hakuniridhisha na namna
suala la Uraia litakavyotatuliwa kwani kutoa jibu la kubakia na 'kukubali' Nchi
mbili halafu uraia mmoja kunaleta mashaka makubwa. Kama tunataka kuwa na Uraia
mmoja ni lazima tuwe Nchi moja, hatuwezi kuwa na Nchi mbili uraia mmoja.
Vilevile vyanzo vya mapato ya
Muungano ni vidogo mno kuendesha dola. Hivyo basi rasimu iliyopo mbele ya Bunge
Maalumu ina mapungufu makubwa japo imetoa mapendekezo yatakayomaliza malalamiko
ya Muungano.
Sasa kazi ya Bunge ni moja tu nayo ni
kuboresha rasimu iliyopo mbeleyake ili kumaliza kero za muungano zilizopo na
kujibu hoja za hofu za muundo mpya. Hakuna sababu ya kubishana kwenye takwimu
za Tume, tume imefanya wajibu wake na sasa Bunge Maalumu nalo litimize wajibu
wake.
Iwapo kama kweli tunataka kusikia
Watanzania wanataka nini kwenye muundo wa Muungano, tusimamishe Bunge na twende
tukawaulize kwa kura (referendum). Vingivenyo tuboreshe rasimu iliyopo na
iliyotokana na maoni ya wananchi wote kwa kujibu hizo hofu muhimu alizoainisha
ndugu Rais na hayo malalamiko muhimu yaliyoainishwa na Tume. Sio kazi ya Bunge
Maalumu kutafuta ubora wa hotuba zilizotolewa mbele yetu bali kuona mazuri
ndani ya hotuba hizo yasaidie kazi yetu Tuzingatie kuwa tusijenge Nchi kwa
kujibu malalamiko na hofu tu maana hofu na malalamiko hayaishi katika dunia
inayobadilika kwa kasi sana.
Tuamue tunataka kuwa Jamhuri ya Muungano
ya namna gani. Nini sababu ya Jamhuri yetu na aina gani ya Tanzania tunataka
kujenga. Tuanze kwa kutafsiri sababu ya Tanzania kuwepo na Tanzania gani
tunataka kujenga kisha tutunge Katiba itakayowezesha kutufikisha huko tutakapo
kufika.
Imeandikwa na Zitto Kabwe
Chanzo: https://www.facebook.com/zitto2010/posts/650775064959182
No comments:
Post a Comment