MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba,
Profesa Ibrahim Lipumba, amekataa uteuzi wa nafasi ya ujumbe kwenye Kamati ya
Uongozi uliofanywa na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Bw. Samuel Sitta.
Alisema uteuzi huo hauna nia njema ya
kupata Katiba Mpya na kudai Bw. Sitta, analiendesha Bunge hilo kwa matakwa ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Prof. Lipumba alitoa msimamo huo
bungeni mjini Dodoma jana baada ya Bw. Sitta, kutangaza majina matano ya
wajumbe wa kamati hiyo ya uongozi.
Wajumbe hao ni Fakharia Hamis
Shomari, Mary Chatanda, Prof. Lipumba, Amon Mpanju na Hamoud Abuu Jumaa.
Baada ya kutangaza majina hayo,
mjumbe wa Bunge hilo Bw. John Mnyika, aliomba ufafanuzi kwa Bw. Sitta juu ya
uteuzi huo na kudai kamati hiyo imekosa uwiano wenye sura ya kitaifa kwa pande
mbili za Muungano ambazo ni Zanzibar, Tanzania Bara.
Pia Bw. Mnyika alisema, kamati hiyo
pia haina mjumbe kutoka chama kikuu cha upinzani bungeni ambacho ni Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Akitoa ufafanuzi wa madai hayo, Bw.
Sitta alisema kamati hiyo imezingatia uwiano wa vyama na jinsia ambapo miongoni
mwa wajumbe aliowateua mmoja ametoka Zanzibar, Bi. Faharia Hamisi Shomari na
Prof. Lipumba angewawakilisha wajumbe wa kambi ya upinzani katika kamati hiyo.
"Si lazima kila chama kipewe
nafasi ambazo zipo tano tu, sina ubaya na CHADEMA wala chama kingine chochote
cha siasa ila nimejitahidi kufanya uteuzi kwa kuzingatia uwiano bila upendeleo
hivyo naomba wajumbe turidhike," alisema Bw. Sitta.
Hata hivyo, Prof. Lipumba alisema
hataweza kuingia katika kamati hiyo kama chambo akiwakilisha kambi ya upinzani
kwani tangu awali, nia yake ya kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF), ni
kuiunganisha Zanzibar na Tanzania Bara.
"Jinsi mchakato huu unavyokwenda ni wazi kuwa hakuna
nia njema ya kupata Katiba ya wananchi, hivyo siwezi kuingia katika kamati kama
mjumbe... nitapambana katika kamati yangu namba 10 ambayo inaongozwa na Bi.
Anna Abdallah na ndani ya Bunge hili ili kujenga hoja.
"Nawaachia wenzangu muweze
kuendelea na mipango yenu ya kulifanya Bunge hili kuwa la Chama Cha Mapinduzi
(CCM), lakini kwa kweli, nimesikitishwa na mpango mlionao," alisema.
Naye mjumbe wa Bunge hilo, Bw. Kangi
Lugola, alimwomba Bw. Sitta kubatilisha uteuzi wa wajumbe wa kamati hiyo kwa
kuwatoa wajumbe ambao ni wanachama wa CCM na kuwaweka wajumbe kutoka upinzani
ili kuondoa manung'uniko yaliyopo.
"Ni ukweli usiopingika kwamba,
CCM tuko wengi hivyo nilitegemea dhana ya kutomeza wadogo isingekuwepo,
ungeweza kuteua wajumbe watano kwa kuangalia jinsia na makundi Maalumu lakini
asiwemo mjumbe wa CCM hata mmoja.
"CCM ni gari kubwa, tukiliacha
likaserereka bila kukanyaga breki mara kwa mara, tutasababisha ajali nyingi
sana katika utungaji wa katiba, wana CCM tusijenge hofu kwa sababu ya wingi wa
wapinzani kuingia katika kamati ya Uongozi," alisema.
Alimshauri Bw. Sitta, kuondoa
manung'uniko kwa kubatilisha uteuzi wake, kuchagua makundi mengine na kama kuna
dhana ya Tanganyika kutomeza Zanzibar, kwa nini kusiwe na dhana ya CCM
kutowameza watu wachache katika Bunge hilo?
Aliongeza kuwa, wajumbe wa Bunge hilo
wamempa heshima na dhamana kubwa Bw. Sitta katika kuliongoza Bunge kwa
kuzingatia weledi, umakini na umahiri wa kuhakikisha hakuna mzozo kwenye
kutunga Katiba Mpya waitakayo Watanzania.
Akitoa ufafanuzi zaidi, Bw. Sitta
alimshukuru Prof. Lipumba kwa uamuzi wa kukataa uteuzi huo na kusema ni haki ya
mjumbe kupokea uteuzi huo au kuukataa kutokana na imani yake.
"Unapoteuliwa ni hiari yako
kuipokea nafasi hiyo au kutoipokea, nashukuru Prof. Lipumba kwa kuamua kusema
ulichokiona wewe ni ukweli na kukataa uteuzi wa Mwenyekiti," alisema Bw.
Sitta.
Aliongeza kuwa, yaliyotokea
yameshatokea kwani ni vigumu kufurahisha nafsi ya kila mmoja kwa lile analotaka
lifanyike, hivyo hoja ya kuchagua wapinzani pekee katika kamati hiyo pia
utakuwa ubaguzi kwa wengine hivyo ataendelea kutenda na kusimamia haki za Bunge
hilo.
Mjumbe mwingine, Bw. James Mapalala
alisema anatambua wingi wa CCM katika Bunge hilo ila kwa upande wake, hajaona
faida ya wapinzani kuwepo bungeni kwani ni udhalilishaji.
Aliviomba vyama vyenye wajumbe wengi
kama CCM katika Bunge hilo, viheshimu uchache wa wengine kwani wote wapo
bungeni kwa ajili ya kupata Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano si katiba ya
chama fulani.
Alisema CCM imepoteza heshima na
kuonesha dharau kwa wajumbe wengine wanaotoka vyama vingine vya siasa na
makundi ambapo wajumbe kutoka chama tawala, wanatumia mabavu kufanya maamuzi
ambayo yangepaswa kushirikisha wajumbe wote.
"Natoa mfano, jana (juzi),
wakati tukitaka kuchagua Mwenyekiti kwenye kamati yangu namba moja, kuna mtu
alikuja, kukaa kwenye kiti na kusema kuwa yeye ndio Mwenyekiti.
"Nilisimama kuhoji nani
aliyemchagua ila wakasimama watu wengi na kusema huyo tumemchagua huku wakipiga
makofi nikawa sina la kufanya ila nikasema sitopiga kura.
"Sisi tunaotoka vyama vidogo,
tunapaswa kupewa heshima kama wajumbe wengine waliopo humu... tunaomba haki ya
kuheshimiwa hata tukitoa mawazo yasiyozingatiwa," alisema Bw. Mapalala.
Naye Bw. David Kafulila, alisema
katika moja ya nukuu ya Bw. Sitta, aliwahi kusema kati ya vipaumbele vyake ni
kuweka usawa katika Bunge, lakini kauli yake kuwa wajumbe wa CCM ndio wengi
katika Bunge hilo si jambo sahihi.
Alimshauri Bw. Sitta, kujipa muda na
kufikiria uteuzi wake wa wajumbe watano katika kamati hiyo kwani hali si shwari
kwani Bunge hilo limechukua sura ya nchi si chama.
Mchungaji Peter Msigwa, alisema ni
kitu cha aibu kama wakifanya maamuzi ya kupitisha Katiba na wananchi
wakayakataa hivyo suala la vyama lisiwepo katika Bunge hilo ili kupata Katiba
bora.
Bw. James Mbatia, alisisitiza suala
la Katiba liwe la Jamhuri ya Muungano na kumtaka kila mjumbe avae uhusika kama
mwananchi wa Tanzania ili kukamilisha mchakato huo.
Naye Bw. Vincent Mzena, aliwasihi
wajumbe kutoka CCM kutoonesha hisia zao za moja kwa moja ndani ya Bunge hilo
kutokana na wingi wao kwani wajumbe wengine wanajiona wanyonge.
Aliwataka wajumbe wengine wasiotoka
CCM, kutoogopa wingi wa wajumbe kutoka chama tawala bali wazingatie hoja ambazo
watazitoa na kuzikubali kama zitakuwa za maana na kuzikataa kama zitakuwa
hazina tija kwa Taifa.
Dkt. Ave-Maria Semakafu, aliwataka
wajumbe wa Bunge hilo kuweka pembeni ushabiki wa vyama na kuhisi mambo bila
kujua hatima yake na kama wajumbe wataona kuna mashaka katika uteuzi wa kamati
hizo ni vyema wakatumia kanuni walizotunga ili kupata mwafaka wa jambo husika.
"Naomba tuache kuhisi, tukiona
wanatuletea ratiba isiyoeleweka tutumie kanuni zetu kutengue baadhi ya kanuni
zinazotuongoza ili tuweze kutengeneza mwafaka ambao utatuongoza na hatimaye
kupata katiba bora," alisema Dkt. Semakafu.
Chanzo: Majira
No comments:
Post a Comment