Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta (kulia) akiongoza kikao cha kwanza cha Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo, mjini Dodoma jana. Na Mpigapicha Wetu
Afafanua utata ulioibuliwa katika
taarifa yake mbele ya Bunge la Katiba.
Dar es Salaam. Wakati Ikulu
ikitangaza kwamba Rais Jakaya Kikwete amevunja Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
tume hiyo imetoa ufafanuzi wa baadhi ya maeneo ya Rasimu ya Katiba.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana,
ilieleza kuwa Tume ya Jaji Joseph Warioba ilivunjwa tangu Machi 19, ikiwa ni
siku moja baada ya kuwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni mjini Dodoma.
Wakati taarifa ya Tume ya Warioba
ilitolewa jana jioni, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilikuwa imeshatoa
taarifa ya kuvunja tume hiyo mapema jana ikieleza kuwa shughuli za tume hiyo
zilikoma tangu Jumatano iliyopita.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Rais wa Jamhuri ya Muungano alivunja rasmi Tume
ya Mabadiliko ya Katiba tarehe 19 Machi, 2014 kwa Tangazo la Serikali Na.81 la
tarehe 21 Machi, 2014,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu.
Hata hivyo, Jaji
Warioba aliliambia gazeti hili jana kuwa hadi wanakutana juzi kwenye
kikao cha mwisho cha tathmini walikuwa hawajapokea barua ya kuvunjwa kwa tume
yake.
“Barua ya Ikulu tumeipokea leo.
Tulikuwa hatuna taarifa kwamba tume yetu imevunjwa hadi tulipopokea barua leo
(jana). Tulifanya kikao chetu cha mwisho cha tathmini jana (juzi),” alisema Warioba alipozungumza na Mwananchi
jana jioni.
Warioba pia alithibitisha kwamba
taarifa ya ufafanuzi (imechapishwa ukurasa wa 37) ni ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
Taarifa hiyo ya Tume ya Warioba
imetaja baadhi ya sababu za kupendekezwa kwa muundo wa serikali tatu kuwa, ni
pamoja na Serikali ya Muungano kutokuwa tena na nguvu upande wa Zanzibar na
Rais kupokwa baadhi ya madaraka aliyopewa kikatiba.
Ufafanuzi wa Tume
Taarifa hiyo ya tume ilisema:
“Waasisi walituachia mambo 21 (ukiacha usajili wa vyama) kwenye orodha ya
Muungano. Katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita yamepunguzwa. Mambo yote
yaliwekwa kwa utaratibu uliowekwa na Katiba lakini yameondolewa kinyume na
Katiba.”
Iliongeza: “Sehemu zote mbili
ziliamua kuachia baadhi ya mambo yake kuwa chini ya Serikali ya Muungano, sasa
sehemu moja inaondoa mambo yake. Kwa hiyo Serikali ya Muungano itakuwa
inashughulikia zaidi mambo ya upande mmoja.”
Kasoro nyingine iliyotajwa na tume
hiyo ni hatua ya waasisi wa Muungano kuwa waliacha Bunge lenye madaraka nchi
nzima, lakini sasa ni lazima sheria linazotunga zipate idhini ya Baraza la Wawakilishi
kwa upande wa Zanzibar.
“Waasisi waliacha Rais akiwa na
madaraka kamili. Madaraka hayo
yamepunguzwa bila kufuata utaratibu wa Katiba. Waasisi walituachia Mahakama ya
Rufani yenye madaraka kamili. Madaraka haya yamepunguzwa. Waasisi waliunganisha
nchi mbili ikawa moja. Sasa tunazo nchi
mbili,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza:
“Hii ndiyo inafanya wananchi wa
Tanzania Bara waamini Zanzibar ni huru katika mambo yao. Wanaona ina mamlaka kamili kushughulikia
mambo yake na imechukua rasilimali zake.
S
erikali ya Muungano imebaki na
mamlaka na rasilimali za Tanzania Bara.”
Taarifa hiyo ilisema wakati wabunge
wa Zanzibar wanashiriki kuamua mambo ya Tanzania Bara, wabunge wa Tanzania Bara
hawana nafasi ya kushiriki katika kuamua mambo ya Zanzibar.
Tume hiyo ilisema ilikuwa vigumu kwa
Zanzibar kurudi kwa hiyari kwenye hali ya awali, ikiwa ni pamoja na kufuta
kipengele cha nchi mbili kwenye Katiba yake, hivyo waliamua kupendekeza mfumo
wa serikali tatu kama hatua ya kuzingatia malalamiko ya Tanzania Bara.
Tume iliona kwamba pamoja na mambo
haya kufanywa kinyume na Katiba ya Muungano, hali ibaki hivyo hivyo. Lakini kwa
kufanya hivyo basi nayo yasipuuzwe.
Hivyo Tume nayo ikapendekeza Serikali ya Tanganyika iundwe.
Hali ilivyo
Tume hiyo imevunjwa huku kukiwa na
mjadala mkali kuhusu hotuba ya Jaji Warioba katika Bunge Maalumu pamoja na ile
ya Rais Kikwete aliyoitoa wakati akizindua Bunge hilo, Machi 21, mwaka huu.
Kutokana na hotuba hizo kukinzana,
hasa kuhusu aina ya muundo wa Muungano unaotakiwa, baadhi ya wajumbe wa Bunge
Maalumu walipendekeza Jaji Warioba apewe fursa ya kuitwa bungeni kutoa
ufafanuzi wa masuala mbalimbali na pengine kujibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa
na Rais Kikwete.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa
kwa mujibu wa kifungu cha 5 na 6 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83
kwa Tangazo la Serikali Na.110 la 2012.
Wajumbe wake 30 waliteuliwa na Rais
Kikwete kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment