Katika ulimwengu wa leo neno blog
siyo kitu kigeni, leo hii karibu kila mtumiaji wa internet anayo blog yake.
Blogu hizi kuna zile zinazotembelewa na watu wengi na kuna zile zinazopata
watembeleaji kwa mdondo.Je umewahi kujiuliza kwanini watu hawatembelei blog
yako kama wanavofanya kwa blog fulanifulani? Ingawa kuna sababu nyingi kama
umri wa blog, umarufu wa mmiliki wa blog nk lakini kuna kuna vitu ambavyo
unaweza kuvifanya na vikakuongezea idadi ya watembeleaji.
Hivyo kwenye makala ya leo
tutaangalia ni vitu gani vya msingi kuzingatia ili blog yako ivutie wasomaji
wengi zaidi.
1. Ishi kwenye blogu yako, chagua
uelekeo unaokufaa.
Kama umekuwa ukifuatilia tasnia hii
ya blogu, utagundua kuwa makala nyingi zinazoandikwa kwenye blogu nyingi za
Tanzania huwa zinafanana sana, na hata muelekeo wa hizi blogu huwa ni uleule.
Ingawa ni jambo la kawaida kwa kila mtu kukimbilia sehemu inayopendwa na wengi
(blogu za habari), lakini jinsi unavyokimbilia sehemu yenye watu wengi, ndivyo
jinsi unavyongeza ushindani.
Siyo tu ushindanni, bali wengi
wamejikuta wakiingia kwenye uelekeo ambao hawaumudu hivyo siku ya mwisho
wanajikuta wakikopi na kupaste.
Hivyo, jambo la muhimu ni kuchagua
uelekeo unaoupenda na kuuweza, mara nyingi kazi ya kublog huwa rahisi kama
unablogu kitu unachokipenda, mfano, binafsi nikiwa ninaandika makala zenye
uelekeo wa IT kwenye Blog ya Dudumizi, kwakuwa ninapenda IT na ndiyo maisha
yangu ya kila siku hivyo kwangu kuandika makala za IT ni sehemu ya maisha
yangu, na jinsi kazi inavyokuwa rahisi ndivyo utakavyoweza kuandika makala
nyingi zaidi na zenye mvuto zaidi, hivyo huvutia wengi zaidi.
Pia jinsi unavyokuwa wa kipekee,
ndivyo unavyopata watemebeleaji wengi zaidi, mfano, badala ya kukimbilia kwenye
blogu za habari na michapo, kwanini usijikite kwenye blogu za yanayoendelea
vyuoni na kuonesha maisha ya wanafunzi, kwanini isiwe blogu ya hadha ya usafiri
na foleni nk.
Wana blogu wanatakiwa kuwa wabunifu,
wawe watu wanaofikisha maono yao juu ya mambo ya kijamii kwa kutumia intaneti,
na wao ndiyo wataisaidia jamii yetu.
Kumbuka; Unapochagua uelekeo,itakusaidia
kujua nani mlengwa wako, na vitu gani muhimu huyo mlengwa wako vinamuhusisha,
hapa utaangalia mambo kama elimu, upeo wa uelewaji na hata vitu wanavyopenda
kusoma. Kwa kujua vitu hivi itakusaidia kuandika makala zinazosomwa na zenye
kueleweka na wahusika. Kumbuka, haublogu ili usome wewe mwenyewe bali ni kwa
ajili ya watemebeleaji wako. Hivyo kuwafahamu wao ni moja ya hatua muhimu
itakayowawezesha kusoma na kuzipenda makala zako.
2. Tumia mitandao ya kijamii
Mitandao ya kijamii ni kitu cha lazima
kama unataka kuongeza watemebeleaji wa blogu yako. Mitandao hii ni vijiwe vya
mamilioni ya watemebeleaji ambao pia ni watemebeleaji wa blogu yako pia, hivyo
ni lazima uhakikishe unatumia vyema mitandao hii.
Hakikisha kila makala ya blogu yako
inaenda moja kwa moja kwenye mitandao jamii, pia hakikisha kwenye kila makala
kuna kitufe cha share, like, g+ nk mbavyo vitawawezesha muingiliano na mitandao
jamii.
Ingawa mitandao jamii ni muhimu,
lakini, epuka matumizi yaliyozidi na hata kuwachukiza watembeleaji, kuna baadhi
ya blogu kila unapofungua unakutana na kidirisha cha
kulike ambacho hukuzuia kufanya
lolote mpaka ulike kurasa ya Facebook. Hi inaweza kuwa kero kwa watembeleaji wa
blogu yako. Kitu cha muhimu hapa ni, usiwalazimishe
watu kulike au kushare makala zako,
bali washawishi kwa ubora wa makala.
3. Blogu yako iwe na spidi ya haraka
Je ni watu wangapi wapo tayari
kusubiria dakika tano mpaka blogu yako ikawa tayari kufunguka? Kama wewe blogu
yako ni mpya, ni dhahiri kuwa hakuna atakayesubiri, na kama wewe blogu yako ni
maarufu, basi watasubiri kwakuwa hakuna mbadala na pindi watakapopata mbadala
basi wataanza kupungua siku hadi siku.
Blogu kuchelewa kufunguka kunaweza
kusababishwa na mambo mnegi kama uwingi wa makala, teknolojia iliyotumika na
hata mrundikano wa vitu; mfano, kwenye blogu nyingi za Tanzania, kumekuwa na
rundo la matangazo kabla ya kuanza kwa makala, na matangazo haya ni picha kubwa
ambazo kila moja inachukua ujazo tosha na kuifanya blogu iwe taratibu sana.
Kuna njia nyingi za kuonesha makala
na matangazo idadi sawa kwa mtindo ambao hautoathiri spidi ya blogu yako ambayo
nimeielezea kwenye kipengele cha muonekano.
4. Fikiria jina kamili
Blogu kama ilivyo Website, inaweza
kuwa na jina, leo hii kuna blogu nyingi sana maarufu zina majina, kama
www.mjengwablog.com, www.8020fashionsblog.com nk, kuwa na jina kamili la blog
yako kutasaidia kukumbukika na pia itakusaidia kwenye mitandao ya utafutaji. Si
hayo tu, pia itakusaidia pindi unapotaka kuhamia kwenye website kamili kwani
hautatakiwa kuwataarifu watembeleaji tena.
Nimewahi kuandika mambo ya kuzingatia
pindi uchaguapo majina ya website / blog
Kwa wale wanaotumia Blogspot, unaweza
kununua jina (domain) halafu ukalielekeza kwenye blogspot na watu wakatumia
jina kamili kufungua blog yako na sio .blogspot.com tena ila wewe utaendelea
kuichunga kwenye blogspot kama kawaida.
Gharama ya jina haizidi elfu 20 ya
kitanzania, unaweza nunua kwa kwenda hapa
5. Muonekano bora ni kitu cha lazima
Kwenye falsafa ya watumiaji wa
mitandao tunasema; mtembeleaji wa wavuti hutumia sekunde zisizozidi tatu
kutafuta anachokitaka na kama atashindwa kukipata, basi kutimka, hivyo blogu
yako ni lazima iwe na uwezo wa kufikisha ujumbe na kumvutia somaji ndani ya
sekunde tatu.
Blogu isiyovutia haiwezi kuwa na
watembeleaji wengi, na hata kama wengi wanakuja, basi hutimka (baunce) bila
kusoma chochote. Leo hii kuna makampuni mengi sana yanayoweza kukusaidia
kutengeneza blogu au website kwa gharama nafuu kabisa, unaweza kutafuta kwa
kuandika website design in tanzania kwenye google na kuangalia makampuni
yanayoweza kukusaidia.
Ingawa mitandao ya blog kama Bloggers
ni mizuri kwa kuanzia, ila jinsi blog yako inavyozidi kukua, ndivyo umuhimu wa
kuwa na blog inayojitegema unavyoongezeka.
Gharama za kutengeneza blog isiyo ya
blogspot.com si ghali na hi itakupa uwanja mpana wa kuchunga na kuiboresha blog
yako.
6. Takwimu ni muhimu pia
Ingawa mada ni jinsi ya kuongeza
wasomaji wa blog yako, lakini hatuwezi kuacha kuongelea umuhimu wa takwimu.
Kuna usemi unaosema, kama usipoipima, basi hautoweza kuiboresha. Hivyo kwa kuwa
na takwimu ya watembeleaji wa blog yako, siyo tu itakuwezesha kujua mtiririko
wa wasomaji, bali wanapotoka, wanatumia muda gani kwenye blog yako nk.
Takwimu zitakusaidia kupanga mikakati
ya kujitanua na kujitangaza zaidi, pia zitakuwezesha kuthaminisha harakati zako
za ukuaji. Na takwimu hizi zinapatikana kwa kwenda Google Analytics.
7. Usisahau watumiaji wa simu
Takwimu zinaonesha, watumiaji wa
intanet wengi hutumia simu za mkononi kufungulia website, na idadi hii
huongezeka siku hadi siku. Hivyo, kama wewe ni mmiliki wa Blog, hakikisha blog
yako inaonekana vyema kwa watumiaji wa simu.
Kama website yako haifunguki kwenye
simu, basi jua kwamba unapoteza mamia ya watembeleaji siku hadi siku. Hivyo
wakati ndiyo huu, nenda kisimusimu zaidi.
Makala zaidi za IT, tembelea
Web: www.dudumizi.com Facebook: www.facebook.com/dudumizi
No comments:
Post a Comment