Mwalimu J. K. Nyerere Muasisi Wa Muungano Wa Tanzania
Dodoma/Dar. Kuna njama. Maneno haya
mawili ndiyo yametumiwa na pande mbili zinazopingana ndani ya Bunge Maalumu la
Katiba, kuelezea hali iliyojitokeza jana wakati wa kikao cha Bunge hilo kuhusu
mvutano wa mabadiliko ya kanuni.
Njama zinazoelezwa na pande hizo ni
za kuvuruga mchakato wa Katiba Mpya, zikirejea yaliyotokea jana jioni ikiwamo
zomeazomea hali iliyomlazimu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel
Sitta kuliahirisha Bunge hadi leo jioni.
Baada ya kuahirisha Bunge hilo, Sitta
alikutana na waandishi wa habari na kusema kwamba kuna njama za baadhi ya
wanasiasa kutumia vurugu kuhujumu mchakato wa upatikanaji wa Katiba, badala ya
kujenga hoja.
Bila kuwataja wanasiasa hao, Sitta
alisema ikiwa hawataki kuendelea na mchakato huo, basi waondoke na kuwaacha
wenye nia njema.
“Wanasiasa hawa wamedhamiria kuvuruga
mchakato wa Katiba, tuhuma ambazo tumetuhumiwa leo na Lissu (Tundu) ni uongo na
uzushi, mimi sihusiki na kupeleka marekebisho ya kanuni kwenye Kamati ya Kanuni
na Haki za Bunge,” alisema Sitta.
Sitta alikuwa anajibu mchango wa
mjumbe wa Bunge, Tundu Lissu alioutoa mapema kwenye kikao cha jioni, akipinga
kilichoelezwa ni njama za kutaka kubadili kanuni kinyemela ili kumsaidia
mwenyekiti kulidhibiti Bunge.
Sitta alisema kwa kuzingatia kanuni
ya 59 (1), Kamati ya Uongozi ina mamlaka ya kupeleka marekebisho ya kanuni ili
kuliwezesha Bunge kufanya kazi vizuri.
Alisema hoja kwamba haiwezekani
kufanyika mabadiliko hata kabla ya kuanza kutumika kanuni, siyo ya msingi kwani
kila kitu kinabadilika kutokana na mazingira yake.
“Kamati ya Uongozi ndiyo ilipeleka
waraka wa mabadiliko ya kanuni kwa Kamati ya Kanuni na Haki kwa kuzingatia
kanuni, lakini hata kabla ya kujadiliwa na kamati husika inaonekana kuna
wajumbe ndiyo wameichukua na kuifikisha bungeni,” alisema Sitta.
Alisema kwa kiasi kikubwa marekebisho
ambayo yangesomwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Pandu Ameir Kificho, yalilenga
kutoa ufumbuzi wa kanuni ya 37 na 38 juu ya upigaji kura ama uwe wa wazi au
siri.
Sitta alisema pamoja na hilo,
kulikuwa na marekebisho ya msingi kama kuweka utaratibu mzuri wa majadiliano
katika kamati pia kuweka utaratibu wa vikao vya Bunge kuanzia Jumatatu hadi
Jumapili.
“Mengi ambayo alikuwa anayasema Lissu
kama ni takataka hayakuwapo katika taarifa ya Kificho,” alisema Sitta.
Kauli ya Lissu
Lissu katika mchango wake alibainisha
kile alichoeleza kama ‘njama’ za kuchakachua kanuni, akihoji inawezekanaje
kasoro zikaanza kuonekana wakati kanuni hazijaanza kutumika.
Alisema kanuni zilipitishwa mapema
mwezi huu na kiporo pekee kilikuwa ni ile ya 37 na 38 kuhusu upigaji kura.
“Tumeletewa jedwali la marekebisho
ambalo linaonyesha kuna marekebisho katika kanuni ya 14 (1), 32, 33, 35 na zile
za 37 na 38 pamoja na 58(1) (d) zingine ni 63 (1) na 64 na kufutwa kwa kanuni
ya 85, jambo ambalo ni kinyume kabisa na kanuni zetu,” alisema Lissu.
Mbunge huyo wa Singida Mashariki,
alisema utaratibu wa kurekebisha kanuni umeelezwa katika kifungu cha 87 (2)
kwamba, mjumbe akiona kuna hitaji la kurekebisha kanuni awasilishe pendekezo
kwa mwenyekiti wa Kamati ya Haki na Kanuni na iwapo Mwenyekiti akiona inafaa
atawasilisha mapendekezo hayo bungeni.
“Kanuni hazina hata wiki tatu,
hazijaanza kutumika tayari mmeanza kuzichakachua hivi, kasoro mmezipataje
wakati bado hazijaanza kutumika,” alihoji.
Huku akionyesha marekebisho hayo,
Lissu alisema: “Hizi ni takataka ambazo hatutakubali ziingizwe ndani ya
mabadiliko.” Alisema Kamati ya Uongozi haina mamlaka yoyote juu ya kanuni za
Bunge.
Lissu kushtakiwa
Sitta alisema kutokana na lugha
alizotumia Lissu juu yake, anakusudia kumfikisha kwenye Kamati ya Kanuni na
Haki za Bunge. Alisema atatoa utetezi na wale ambao wanamtuhumu wataeleza ili
ukweli ujulikane.
Alisema vurugu za jana jioni,
zilipangwa hata kabla ya kuanza Bunge hilo, kwani hata wajumbe wanaotokana na
Ukawa walisusia kutoa maoni katika Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge.
“Wajumbe wao hata kwenye kamati
walikuwa hawazungumzi na wakati wanatoka walisikika wakisema wataendelea na
mkakati wao wa kufanya vurugu,” alisema Sitta ambaye pia ni Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Ilivyokuwa
Dalili za kuvunjika kikao hicho
zilionekana mapema baada ya wajumbe kuingia ukumbi kwani baadhi walikuwa kwenye
makundi yaliyoashiria kujipanga kwa jambo lililokuwa mbele yao.
Kwa muda kidogo ukimya ulitawala
bungeni baada ya Sitta kuzungumza, kisha ilisikika sauti ikiomba mwongozo.
Mwenyekiti alitoa nafasi kwa Lissu
akitimiza ahadi yake aliyokuwa ameitoa asubuhi kabla ya kuahirisha Bunge hilo.
Mapema jana asubuhi, Sitta alikuwa
ameahidi kuwa angetoa nafasi kwa miongozo hata kama ingekuwa 20 au 30 ili kila
mtu aweze kupata kile alichokuwa akikihitaji.
Baada ya Lissu kueleza tuhuma zake,
zomea zomea ilianza bungeni kiasi cha kuvuruga na kuondoa utulivu.
Waziri wa Sheria na Katiba wa
Zanzibar, Abubakar Khamis Bakary baada ya kuruhusiwa alisema Bunge linaendeshwa
na kanuni “haiwezekani huko aliko aandike mambo yake na kuyapeleka kwenye
kamati halafu yaletwe bungeni, jambo hili haliwezi kukubalika.”
Alisema Bunge hilo ni lenye hadhi na
heshima kubwa lakini kanuni kukiukwa kwa kanuni na sheria husika kunapunguza
hadhi yake.
Kauli za wajumbe hao ziliungwa mkono
na mjumbe mwenzao Ismail Jussa ambaye alisema waliopendekeza mabadiliko ya
kanuni walikaa mafichoni kutekeleza azma hayo.
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Jaji Frederick Werema, akizungumza huku akikatishwa na makofi yaliyochanganyika
na zomeazomea na yeye akielekeza maneno yake kwa kelele hizo alisikika akisema,
“sijazoea kuzomewa” na wakati mwingine akisema “sijazoea kupigiwa makofi.”
Baada ya utulivu kukosekana, Sitta
aliahirisha Bunge hilo ili kwanza wajadiliane kabla ya kuendelea.
Ukawa: Hatoki mtu
Wajumbe wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) wamesema wataendelea kupambana ndani ya Bunge Maalumu hadi
ipatikane Katiba nzuri na watakuwa wa mwisho kujitoa katika mchakato huo.
Pia wamebainisha kuwa kukimbia au
kujitoa katika mjadala huo ni sawa na kuwaachia CCM walio wengi kwenye Bunge
Maalumu watunge Katiba wanayoitaka wenyewe na hivyo kuzima mawazo ya wananchi.
Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe
alitoa msimamo huo jana katika mkutano na waandishi wa habari huku akiweka
tahadhari kuwa “Uvumilivu una mwisho wake, ukifika wakati huo tutawaambia
Watanzania nini kinachoendelea na sisi tunakusudia kufanya kitu gani.”
Imeandikwa na Mussa Juma, Habel
Chidawali na Editha Majura
Mbowe ambaye ni kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema kuna dalili zinavyoonyesha kuwa CCM hakina
nia njema ya kuwafanya wananchi wapate Katiba nzuri.
“Hakuna mwendawazimu ambaye anaweza
kufanikiwa kutugombanisha na kutusambaratisha, lazima katika jambo hili
tutashinda na matakwa ya wananchi yatachukua nafasi ndani ya Katiba.”
Kwa upande wake James Mbatia alisema
Ukawa haiwezi kwenda kinyume na wala haitakuwa tayari kuwasaliti wananchi
katika yale ambayo waliyapendekeza kwenye rasimu.
Hotuba za JK, Warioba kutojadiliwa
Matarajio ya wajumbe wa Bunge Maalumu
kujadili hotuba ya Rais Jakaya Kikwete na ile ya Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba yameyeyuka.
Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel
Sitta alisema amechukua uamuzi huo baada ya majadiliano ya kina na kuonekana ni
kama kutanguliza mjadala wa Rasimu ya Katiba kabla ya wakati wake.
“Kumbukeni waheshimiwa Rasimu ya
Katiba tutaijadili kwa mpangilio wa sura mbili kama haitafanyika marekebisho ya
kanuni hivyo, tukijadili hotuba hizi, wabunge watajadili mahala popote
panapowahusu na hivyo itaharibu kabisa utaratibu wa kanuni,” alisema Sitta.
Awali, ilipangwa hotuba hizo
kujadiliwa hasa kutokana na hoja mbalimbali za wajumbe kutaka kujadiliwa hutuba
hiyo.
Miongoni mwa wajumbe walioomba
kujadiliwa kwa hotuba hizo ni Julius Mtatiro ambaye pia aliomba kurejeshwa kwa
Jaji Warioba kutoa ufafanuzi kuhusu masuala yaliyoibuliwa na Rais Kikwete.
Mjumbe mwingine Tundu Lissu
aliwaeleza waandishi wa habari kuwa alikuwa anakusudia kumjibu neno kwa neno
Rais Kikwete katika kila hoja kwani hotuba yake ilikuwa na upungufu.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment