KOCHA Mkuu wa Simba, Zdravko
Logarusic ametamka mambo mawili. La kwanza inawezekana lisiwe zuri sana kwa
mashabiki wa Msimbazi lakini la pili ni la maana.
Kwanza amewaambia mashabiki wasiwe na
matumaini makubwa kutokana na hali
halisi ya ufanisi wao wa uwanjani lakini pili, amewahakikishia kwamba atashusha
Msimbazi mashine sita mpya za maana ambazo zitabadili kila kitu na kurejesha
heshima ya klabu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti jana
Jumatatu, Logarusic alisema Simba inahitaji nyota wapya wenye uwezo na uzoefu
mkubwa wasiopungua sita ambao ndiyo watakaoweza kuleta matokeo mazuri
wakichanganywa na baadhi waliopo sasa lakini akasisitiza kwamba atafanya
mabadiliko makubwa ambayo yatarejesha heshima ya Simba msimu ujao.
Alisema atasajili mabeki wawili wa
maana, viungo wawili viwango pamoja na mashine nyingine mbili za kufunga
magoli. Alisema Simba inahitaji viungo
wawili wenye uwezo wa kuchezesha timu ikiwa ni pamoja na kutoa pasi za mwisho
kwa washambuliaji ambazo sasa ni wazi zimepungua.
“Kwasasa ni kama kila kitu
kimemalizika msimu huu, huu ni wakati wa kuanza kujipanga kwa msimu ujao,
tunatakiwa kufanya marekebisho makubwa kwa kuleta nyota wapya wasiopungua sita
ambao watachanganywa na baadhi ya waliopo sasa,” alisema Logarusic ambaye Simba
bado haijampa mkataba mpya kwani ule wa awali unamalizika mwisho wa msimu huu.
“Hawa waliopo sasa sio kwamba wote
hawafai, wapo wanaofaa kwa kubakia katika timu hii, wapo wengine wanaotakiwa
kukaa benchi kujifunza kutoka kwa wengine au kuwarudisha nyuma kidogo katika
kundi la vijana na pia wapo ambao wanatakiwa kuondolewa kabisa,”alisisitiza.
Tayari Simba imeshaanza mikakati hiyo
ya kuboresha kikosi ambapo Mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hans Pope
alimuagiza mkurugenzi wao wa ufundi,
Moses Basena kwenda nchini Uganda kuangalia nyota wapya wanaowataka.
Basena alisharudi nchini kurudisha
ripoti ya awali ambapo katika ripoti yake hiyo inasemekana amekuja na mikataba
ya nyota hao ambao wamemvutia kulingana na vigezo alivyopewa na Logarusic
akisubiri kumkabidhi Hanspope ambaye yupo safarini kikazi.
Simba imepoteza matumaini ya ubingwa
ambapo sasa inasaka nafasi ya pili ingawa bado inakumbana na ugumu wa Mbeya
City ambayo imekomaa kwenye nafasi ya tatu ikaziba njia ya Simba kupenya.
Chanzo: Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment