MAHAKAMA ya Rufaa Dar es Salaam,
imetengua adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela na faini ya sh bilioni 22
iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Februari 23 mwaka 2012,
dhidi ya raia wa Taiwan na China.
Nahodha wa meli, Hsu Chin Tai,
na wakala wa meli ya Tawaliq 1, Zhao
Hanquing walikata rufaa baada ya kubaini sheria zilikiukwa wakati wa
uendeshwaji wa kesi hiyo katika mahakama za chini.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na jopo la
majaji watatu Salum Masati, Semistocles Kaijage ambao walisema dosari ya kwanza
ambayo Mahakama ya Rufaa imebaini ni kwamba kesi hiyo ilifunguliwa bila kibali
cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Hata hivyo, Mahakama Rufaa imempa
ruhusa DPP ya kuwafungulia kesi upya warufani hao na wale walioachiliwa na
Mahakama Kuu, kama ataona kuna haja ya kufanya hivyo.
Wakili wa warufani hao, John
Mapinduzi, alisema amefurahishwa na hukumu hiyo na kwamba hivi sasa anajiandaa
kufungua kesi ya madai dhidi ya serikali kutaka wateja wake walipwe fidia.
Pia alisema ataiomba Mahakama iilipe
meli iliyokuwa ikitumiwa na watuhumiwa hao kuvua samaki ambayo kwa sasa
imechakaa kutokana na vyuma vyake kukatwa kama chuma chakavu.
Machi 2009 washtakiwa hao
walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kisha kesi hiyo
ikahamishiwa Mahakama Kuu wakikabiliwa na makosa ya kuvua samaki bila leseni,
kuharibu mazingira katika kina kirefu cha ukanda wa Bahari ya Hindi eneo la
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment