MVUA zinazoendelea kunyesha jijini
Dar es Salaam zimesababisha uharibufu wa miundombinu ya barabara, nguzo za
umeme na mingine kuharibika, hali iliyokwamisha shughuli nyingi jana.
Mvua hizo zilizonyesha usiku mzima wa
kuamkia jana, ziliambatana na upepo mkali, radi na ngurumo nzito zilizowatia
hofu wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam.
Wakazi waishio mabondeni walikuwa na
kazi ya ziada kwani wengi nyumba zao ziliingia maji na kusababisha baadhi yao
kuhama makazi yao usiku, huku wengine wakipoteza vitu na samani mbalimbali.
Kutokana na barabara za Jiji la Dar
es Salaam kufurika maji, askari wa Usalaama Barabarani (Trafiki), walikuwa na
kazi ya ziada kuyaruhusu magari kupita njia ambazo ziko salama bila kujali
sheria.
Tanzania Daima ilishuhudia barabara
kuu zote na maeneo mengine kufurika maji na kusababisha wakazi wa jiji hilo
kupita kwa shida.
Aidha, baadhi ya wakazi waliokuwa wakitoka Pugu, walilazimika kupanda
magari ya kubeba ng’ombe yaliyokuwa yakitokea mnadani baada ya daladala nyingi
kusitisha safari zake.
Wakati hali ikiwa hivyo, eneo la
Jangwani maji hayo yalizoa miundombinu
ya mabomba ya maji ikiwemo yale yaliyojengwa hivi karibuni kupisha ujenzi wa
barabara ya magari yaendayo haraka (DART).
Pia kulikuwa na baadhi ya vijana
katika eneo hilo waliokuwa wakijiokotea vitu mbalimbali vilivyokuwa vikielea
juu ya maji.
Akizungumzia kufurika kwa maji kwenye
barabara hizo kuu, Sajenti James Walter, alisema ilibidi kuyaruhusu magari ya
abiria yapite njia nyingine kinyume cha
sheria, lengo likiwa kuwafikisha salama abiria kule wanakokwenda.
“Kwa kweli hali ni mbaya lakini
tumejipanga vizuri kuhakikisha abiria na watumiaji wa barabara hizi hawakwami
njiani,” alisema Walter.
No comments:
Post a Comment