Wednesday, March 26, 2014

LUGOLA: NITAKUWA WA MWISHO KUISALITI RASIMU YA WARIOBA


Mjumbe wa Bunge la Katiba, Kangi Lugola ameapa kuwa atakufa na tai shingoni kwa kuitetea hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kwa kuwa ndiyo iliyobeba mawazo ya watu wengi.

Kutokana na hilo, Mbunge huyo wa Jimbo la Mwibara anaonekana kutofautiana waziwazi na Mwenyekiti wa chama chake cha CCM, Rais Jakaya Kikwete ambaye aliipinga baadhi ya vipengele vya rasimu hiyo.

Akizungumza baada ya kupangwa kwenye kamati, Lugola alisema kuwa haoni tatizo katika hotuba ya Warioba na kwamba atakuwa wa mwisho kuisaliti.
Alisema kuwa mawazo ya Tume ya Jaji Warioba ndiyo mawazo ya Watanzania walio wengi ambao walipendekeza kuhusu Katiba wanayoitaka.

"Sasa mkisema napingana na Mwenyekiti wangu, nadhani siyo dhambi kufanya hivyo kama tunapingana kwa misingi ya hoja, lakini msimamo wangu mimi ni Serikali tatu ambayo ndiyo hotuba ya Warioba aliyesimama pale kwa niaba ya watu wote," alisema Lugola.

Alisema kuwa Katiba anayoitaka ni ile iliyotoka kwa wananchi na wala siyo Katiba inayotoka kwa viongozi na kuongeza hata Mwenyekiti wa CCM (Rais Kikwete) atakuwa analijua hilo.

Mbunge huyo machachari alisema kuwa mbali na kupangwa katika kamati ambayo imejaa vigogo wakubwa wa CCM hatajali na kuapa atapambana hadi mwisho.
Mwenyekiti wa Bunge Samuel Sitta alitangaza orodha ya majina kwa kila kamati jana na Lugola amepangwa kamati namba 6.

Hata hivyo, huenda akapata upinzani mkubwa kutokana kamati hiyo kuwa na vigogo wa CCM, Sophia Simba, Stephen Wasira, John Magufuli.
Vigogo wengine wa CCM walioko kwenye kamati hiyo ni pamoja na Margareth Sitta, Dk. Fenela Mukangara. Pia yumo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema jambo linalodhihirisha atapata wakati mgumu.

Tangu kuanza kwa Bunge la Katiba, Lugola amekuwa na msimamo wa kuunga mkono Serikali tatu yeye pamoja na Mbunge wa Nkasi, Ali Keissy.

Chanzo:Mwananchi

No comments: