Baada ya mahakama kuwahukumu kifo
wafuasi 529 wa Udugu wa kiislamu leo hii(Jumanne) kundi jingine la wafuasi 700
akiwemo kiongozi wao wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji katika mahakama hiyo.
Kesi dhidi ya kiongozi wa kundi la
Udugu wa Kiislamu Mohammed Badie na wafuasi 682 wa kundi hilo imekuja siku moja
baada ya mahakama hiyo ya mkoa wa Minya kutoa adhabu ya kifo dhidi ya wafuasi
wengine 529 wa kundi hilo,hukumu ambayo mashirika ya kutetea haki za binadamu
imesema ndiyo ya kwanza ya aina yake kushudiwa katika historia ya Misri,ikilihusisha
kundi kubwa la watu.Mawakili wa kundi hilo wanasema watadai kujiuzulu kwa jaji
aliyepitisha hukumu hiyo iliyofikiwa baada ya vikao viwili tu vya kuisilikiza
kesi dhidi ya kundi hilo la wafuasi wa Udugu wa Kiislamu.
Wataalamu wa masuala ya kisheria hata
hivyo wanasema hukumu hiyo huenda ikabatilishwa katika mahakama ya rufaa.Hukumu
hiyo iliyotolewa katika kipindi cha muda mfupi ilizusha malalamiko na
kukosolewa Kimataifa pamoja na kupigiwa kelele na wapinzani wa serikali
iliyowekwa madarakani na jeshi.
Marekani imehoji utendaji wa mahakama
hiyo iksema ni vipi mahakama inaweza kusikiliza kesi hiyo kwa njia ya haki
ikiwa kesi hiyo imeendeshwa kwa muda wa siku mbili tu?Kesi hiyo ilifunguliwa
Jumamosi na Jumatatu hukumu ikatolewa,hatua ambayo Marie Harf msemaji wa naibu
waziri wa mambo ya nje,anasema imesababisha wasiwasi mkubwa na kuishutuwa
serikali ya mjini Washington.
Halikadhalika Umoja wa Ulaya umepaaza
sauti kuikosowa hatua hiyo,mkuu wa sera za nje Catherine Ashton ameutolea mwito
Utawala wa Misri kuwatetendea haki washtakiwa katika kesi hiyo.Itakumbukwa
kwamba tangu serikali hiyo ilipoingia madarakani imewashtaki zaidi ya wafuasi
2000 wa kundi hilo la Udugu wa kiislamu,baada ya kupinduliwa mwezi Julai rais
aliyeingia madarakani kidemokrasia Mohammed Mursi.
Kwa ujumla wafuasi kiasi 1200
wanaoshtakiwa katika mahakama hiyo ya mkoa wa Minya wanatuhumiwa kuhusika na
mauaji,jaribio la kuwaua askari kadhaa wakati wa ghasia zilizoibuka mwezi
Agosti 14 wakati ambapo polisi ilihusika kuua mamia ya wafuasi wa rais Mursi
pale walipozivamia kambi mbili za wafuasi hao kwa lengo la kuwatawanya. Maelfu
ya wanachama wa Udugu wa kiislamu walikamatwa na viongozi wa juu wa kundi hilo
akiwemo Mursi wanakabiliwa na kesi.Na kama haitoshi serikali ililitangaza kundi
hilo kuwa la kigaidi ingawa Udugu huo wa kiislamu unasema umejitolea kutekeleza
harakati za amani.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri:Mohammed AbdulRahman
Chanzo: DW
No comments:
Post a Comment