WACHEZAJI 29 kati ya 34,
waliochaguliwa katika programu maalumu ya marekebisho ya timu ya Taifa,
inayoendeshwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wameshaanza
mazoezi ya nguvu wilayani Tukuyu, Mbeya.
Wachezaji hao, ambao wametokea katika
mikoa mbalimbali nchini, waliingia kambini Jumamosi wakiongozwa na kocha Salum
Mayanga akisaidiwa na Patrick Mwagata, ambaye ni kocha wa makipa, Meja Joakim
Mashanga daktari wa timu na Fred Chimela Meneja Vifaa.
Taifa stars, inayodhaminiwa na Bia ya
Kilimanjaro Premium Lager kwa mwaka wa pili mfululizo sasa, inatarajiwa kupata
mabadiliko makubwa ndani ya miezi miwili ijayo ili ipatikane timu bora
itakayoshiriki mechi za kufuzu kucheza Kombe la Afrika.
Makocha wazoefu walikusanyika Lushoto
takriban wiki mbili zilizopita na kufanya zoezi la kuwachagua vijana 34, ambao
baadaye watachujwa na kubali 20.
Watakaochaguliwa watajiunga na Taifa
Stars ya siku zote na kutengeneza timu ya wachezaji 45 ambao watachujwa tena,
ili ipatikane timu ya wachezaji 25.
Kazi hiyo inatarajiwa pamoja na mambo
mengine kuimarisha uzalendo miongoni mwa wachezaji watakaochaguliwa na hili
linafanyika kwa kuhakikisha wachezaji wote, wanaimba wimbo wa taifa kila
asubuhi na jioni kabla ya kuanza mazoezi.
Kila chumba cha wachezaji pia kina
bendera ya taifa, taratibu za kambi na wimbo wa Tanzania Tanzania ambavyo
vinasaidia kuimarisha uzalendo miongoni mwa wachezaji.
Kwa upande wake kocha, Mayanga
alisema vijana wote wako salama na wanategemea kuwapata wachezaji wazuri, baada
ya kambi hiyo.
ìTunawapongeza wadhamini wetu
Kilimanjaro Premium Lager, ambao wamefanikisha shughuli hii kwani tuna imani
tutapata vipaji vikubwa mno baada ya zoezi hili na timu yetu ya taifa itakuwa
bora zaidi,î alisema.
Timu hiyo imepiga kambi katika hoteli
ya Landmark, mjini Tukuyu na wanafanya mazoezi katika Chuo Cha Ualimu.
Shughuli hiyo imeleta msisimko mkubwa
mjini Tukuyu, huku mashabiki wa soka wakisema wana imani sasa itapatikana timu
bora zaidi kwa sababu ya utaratibu uliotumika.
No comments:
Post a Comment