Lori la mizigo aina ya Fusso likiwa limegongana na gari ndogo aina ya Toyota Hilux Pick Up katika eneo la Hedaru, wilayani Same, Kilimanjaro, juzi na kusababisha vifo vya watu 12. Picha na Alex Shirima
Moshi. Mji wa Hedaru uliopo wilayani
Same mkoani Kilimanjaro, jana ulizizima kwa vilio na simanzi baada ya
waombolezaji 12 wote ndugu, kufariki dunia kwa ajali ya barabarani.
Waombolezaji hao wanawake, walipewa
lifti ya gari na Diwani wa Kata ya Hedaru, Gerard Mgwena (CCM), kwa ajili ya
kuwapeleka msibani eneo la Majengo ambako mtu mmoja alifariki kwa kusombwa na
maji.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro
(RPC), Robert Boaz alithibitisha ajali hiyo akisema ilitokea juzi saa 2:00
usiku na kwamba ilikuwa mbaya zaidi tangu kuanza kwa mwaka 2014.
“Ni ajali iliyohusisha magari matatu
kwa wakati mmoja…; watu 11 walifariki pale pale na mwingine alifariki dunia leo
(jana), asubuhi Hospitali ya Rufaa ya KCMC,”alisema Boaz.
Hata hivyo, alisema hakuwa na nafasi
nzuri ya kufafanua kwa undani ajali hiyo kwa vile alikuwa nje ya Mkoa wa
Kilimanjaro na kuelekeza atafutwe Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa
(RTO), Joseph Mwakabonga.
Akizungumza kwa niaba ya RPC,
Mwakabonga alisema, lori aina ya Mitsubish Fusso lililokuwa likitokea Moshi
kwenda Dar liligonga kwa nyuma gari aina ya Toyota Hilux Pick-Up.
Alisema kuwa baada ya kuligonga gari
hilo lililowabeba waombolezaji hao, nalo lilisukumwa na kwenda kuligonga lori
aina ya Scania lililokuwa na tela lake.
Lori hilo aina ya Scania lilikuwa
likitokea Dar es Salaam kwenda Moshi likiendeshwa na dereva wake, Gabriel
David. Madareva wawili wa Toyota Pick-Up na Toyota Fusso wote hawajulikani
waliko.
Taarifa zilizopatikana baadaye,
zilisema dereva wa Fusso alikuwa amelazwa katika Hospitali ya KCMC, wakati
Kigogo wa CCM aliyekuwa amewabeba waombolezaji akilazwa hospitali moja jijini
Arusha.
Mwakabonga aliwataja waliofariki kuwa
ni Stella John(45), Salma Kizoka (33), Marry Senzige (49), Neema Daniel (52),
Rehema George (29) na Sophia Mbike (51).
Wengine ni Ritha Kalani (55), Mama
Kalani Stephano (55), Kolina Mmatha(55), Bahati Daud(25) na Farida Kiondo
mwenye umri wa miaka 25.
Majeruhi mmoja, Maria John (33)
ambaye ni miongoni mwa watu 10 waliojeruhiwa, alifariki dunia jana asubuhi
katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC alikolazwa kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia
ajali hiyo, watu hao walipata ajali hatua 10 kutoka katika eneo ambalo ndugu
yao aliosombwa na maji na kufa, ambapo maiti yake iliokotwa eneo hilo.
Alex Shirima mmoja wa mashuhuda
alisimulia kuwa gari la diwani lilikwama kweye tope katikati ya Barabara ya
Moshi Dar es Salaam.
Alisema, kabla ya kushuka kuangalia
namna ya kulinasua gari lake, likatokea lori gari aina ya Fuso kwa nyuma ambalo
liliigonga gari lake iwani na kulisukuma mita kadhaa mbele ambako lilikutana
uso kwa uso na lori lingine aina ya Scania lililokuwa likitokea Dar es Salaam.
Alisimulia kuwa kutokana na ukubwa wa
ajali hiyo, eneo hilo lilitapakaa viungo vya binadamu na damu.
Shirima ambaye ni dereva aliyefika
katika eneo hilo dakika mbili baada ya ajali kutokea, alisema eneo hilo ni
hatari kwa madereva kwa kuwa mvua zikinyesha, barabara hujaa maji na matope.
Hali ilivyo kijijini
Mmoja wa watoto ambaye mama yake
mzazi amefariki katika ajali hiyo, Sebali Mkwizu alisema kuwa kijiji chao
kimekumbwa na ukimya na majonzi, huku wakishindwa kuamini kilichotokea.
Alisema kuwa ajali hiyo imechukua
maisha ya ndugu zake wanane na kati ya hao, saba walikuwa wakiishi kijijini
hapo kwenye nyumba tofauti zinazofuatana.
“Nimepoteza mama yangu mzazi, mama
mdogo, shemeji zangu watatu, mke wa ndugu yangu na watoto wawili. Hapa nyumba
saba zina msiba,” alisema Mkwizu.
Alibainisha kwamba mazishi ya
wanawake hao yanatarajiwa kufanyika leo katika eneo la pamoja kijijini hapo.
“Tumeambiwa watazikwa eneo moja,
lakini bado hatujajua ni sehemu gani, hadi kesho (leo) ndiyo tutapata taarifa
kamili,” alisema.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment