Kansela Angela Merkel na Rais Xi Jinping wa China katika
mkutano na waandishi wa habari Berlin.(28.03.2014).
Ujerumani na China zimeahidi
kuimarisha mkakati wao wa kibiashara wakati wa ziara ya kihistoria ya Rais Xi
Jinping wa Chinannchini Ujerumani ambayo imeshuhudia kusainiwa mikataba kadhaa
ya kiuchumi Ijumaa.
Kampuni kuu ya kutengeneza magari
nchini Ujerumani imechukuwa nadhari kuu katika kituo cha tatu cha ziara ya Xi
barani Ulaya ambapo kampuni kuu ya magari ya Daimler ikitangaza kufikiwa kwa
mkataba wa kutengeneza magari na wenzao wa China wenye thamani ya euro bilioni
moja.
Ushirika huo na Shirika la Magari la
China la (BAIC Group) unapanga kuongeza uwezo wa uzalishaji katika mradi wao wa
pamoja wa Beijing Benz (BBAC) ifikapo mwaka 2015.
Miongoni mwa mikataba mengine
iliosainiwa hapo Ijumaa Benki ya Ujerumani Bundesbank na Benki ya Watu wa China
zimekubaliana juu ya nia ya kuanzisha kituo cha fedha kushughulikia malipo ya
shughuli za kibiashara kwa kutumia sarafu ya China ya yuan katika mji wa
Frankfurt.
Ujerumani ni mshirika mkuu wa
biashara wa China katika Umoja wa Ulaya wakati taifa hilo kubwa kabisa la Asia
ni soko kuu wa mashine za Ujerumani,teknolojia na magari.
Ukraine yajadiliwa
Viongozi wa nchi hizo mbili wamesema
wamejitolea kuimarisha uhusiano wao kwa mashauriano ya kila mara kuhusu masuala
ya dunia na kanda na uratibu wa karibu zaidi katika Umoja wa Mataifa,Kundi la
Mataifa 20 ya nchi zilizoendelea na zinazoinukia kiuchumi na mashirika mengine
ya kimataifa.
Wote wawili Merkel na Xi ambaye ni
rais wa kwanza wa China kuitembelea Ujerumani katika kipindi cha miaka minane
wamelizungumzia suala la Ukraine.
China ambaye kwa kawaida ni mshirika
wa Urusi ilijitowa katika kura ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya
rasimu ya azmio lenye kuilani kura ya maoni inayoungwa mkono na serikali ya
Urusi ambayo imepelekea kunyakuliwa kwa jimbo la Crimea na Urusi.Pia imejitowa
katika kura ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo Alhamisi ambayo haijifungi
kisheria yenye kutangaza kujitenga kwa Crimea sio halali.
Rais Xi amesema China haina maslahi
binafsi katika suala la Ukraine na kwamba pande zote zinazohusika zinatakiwa
kushirikiana kutafuta ufumbuzi wa kisiasa na kidiplomasia kwa mzozo huo.
Kansela Merkel amesema Ujerumani
imekuwa wazi katika suala la kutetea kuheshimiwa kwa mamlaka ya dola na sheria
ya kimataifa.
Haki za binaadamu muhimu
Wakati Rais Xi hakugusia masuala ya
haki za binaadamu Merkel amesema suala hilo ni sehemu muhimu katika mazungumzo
kati ya China na Ujerumani na kusisitiza umuhimu wa uhuru wa kuzungumza katika
dunia inayoendelea kubadilika.
Ziara ya Xi inakuja kabla ya wiki ya
kufunguliwa kwa maonyesho makubwa kabisa kuwahi kufanyika ya msanii mpinzani wa
Kichina Ai Wenwei kufunguliwa mjini Berlin.Msanii huyo mwenye kuikosoa serikali
hawezi kuhudhuria maonyesho hayo kutokana na kutaifishwa kwa paspoti yake na
serikali ya China hapo mwaka 2011 baada ya kuwa kizuizini kwa takriban miezi
mitatu.
Akiandamana na mke wake muimbaji Peng
Liyuan ,Rais Xi alilakiwa kwa heshima za kijeshi katika viwanja vya Kasri la
Rais na mwenyeji wake Rais Joachim Gauck wa Ujerumani mwanaharakati wa haki za
binaadamu wa zamani wa Ujerumani Mashariki.Nje ya viwanja hivyo kulikuwa na
kama wanaharakati 50 wa Tibet waliokuwa wakiandamana kwa amani.
Baada ya kumaliza ziara yake ya siku
mbili nchini Ujerumani Rais Xi anatembelea makao makuu ya Umoja wa Ulaya
yalioko Brussels Ubelgiji.Hii ni ziara ya kwanza ya Xi barani Ulaya tokea awe
rais wa China na imejikita zaidi katika uwekezaji wa kigeni ambapo alipokuwa
nchini Ufaransa alisaini makubaliano ya kuagizia ndege kutoka kampuni kubwa
kabisa ya ndege barani Ulaya ya Airbus yenye thamani ya euro bilioni 10. Ziara
yake nchini Brussels pia inaonekana kama ni hatua ya kuimarisha uhusiano wa
kiuchumi na umoja huo wenye nchi wanachama 28.
Mwandishi: Mohamed
Dahman/AFP/Reuters/dpa
Mhariri : Caro Robi
Chanzo: DW Swahili
No comments:
Post a Comment