Dodoma. Siku moja baada ya Rais
Jakaya Kikwete kuzindua Bunge na kuponda ripoti ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph Warioba amesema jukumu walilopewa
kwa mujibu wa sheria wamelikamilisha na wanawaachia wananchi waamue.
Akizungumza na Mwananchi jana
asubuhi, Jaji Warioba alisema alichokizungumza Rais Kikwete ni maoni yake na
kwamba hawezi kuyajadili.
“Rais Kikwete alichozungumza ni maoni
yake, kwa sasa sipendi kuyazungumzia hayo, ” Jaji Warioba alieleza.
Alisema wamemaliza jukumu walilopewa
na kwamba sasa jukumu lote lipo mikononi mwa Bunge.
Jaji Warioba alisema Tume yake
ilikusanya maoni kutoka kwa wananchi, mabaraza ya wilaya ya Katiba na Taasisi
mbalimbali, wakatengeneza rasimu ambayo sasa wameikabidhi kwa Bunge Maalumu la
Katiba.
Jaji Warioba pia alikataa kuzungumzia
zogo lililoibuka bungeni na kusababisha rasimu kuwasilishwa Jumatano, baada ya
kikao cha Jumanne kuvunjika.
Hali hiyo ilitokana na UKAWA kudai
muda wa saa 1:30 uliokuwa umepangwa Jaji Warioba ahutubie bungeni uongezwe na
kanuni inayoelekeza Rais Jakaya Kikwete ahutubie kabla Jaji Warioba
hajawasilisha rasimu izingatiwe, baada ya kutangazwa kuwa Rais angehutubia
baada ya rasimu kuwasilishwa.
Profesa Baregu
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Profesa Mwesiga Baregu alisema alitarajia Rais Kikwete angezindua Bunge
Maalumu na siyo kutoa maagizo na vitisho kwa wajumbe.
Alisema hajui lengo la Rais kufanya
alichofanya lakini ana hakika kwa kutoa ufafanuzi wa hoja zilizotokana na maoni
ya wananchi ndani ya rasimu, ameingilia kazi za Tume na hivyo amevunja Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba (Sura ya 83 toleo la mwaka 2012), inayosema:
“21.-(b) atakayejifanya kuwa mjumbe
wa Tume au Sekretarieti; au (c) atakayeendesha programu ya elimu juu ya
mabadiliko ya katiba kinyume na masharti ya sheria hii, atakuwa ametenda kosa.
(3) atakayetiwa hatiani kwa kutenda
kosa kinyume na Sheria hii, atawajibika kulipa faini isiyopungua Sh2,000,000
(milioni mbili) na isiyozidi Sh5,000,000 (milioni tano) au kifungo kwa muda
usiopungua mwaka mmoja na usiozidi miaka mitatu au adhabu zote mbili.
Sheria hiyo inaendelea kuelekeza, (4)
Hatua zozote zilizochukuliwa chini ya kifungu hiki hazitachukuliwa kuwa
zimefikia ukomo na zitaendelea kuwa na nguvu ya kisheria hata baada ya Sheria
hii kukoma kutumika.”
Profesa Baregu alisema sheria
imezungumzia mtu yeyote, hajui kwa Rais inakuwaje.
“Sijui ameona Bunge halitoshi,
haliwezi kung’amua mambo au limepungukiwa kiasi cha kushindwa kumudu majukumu
yake? Sielewi ila amevunja sheria na amelivunjia Bunge hadhi yake kiasi kwamba
hata kazi yake inaweza isiaminike,” alieleza.
Profesa Baregu alisema Rais Kikwete
amejipa jukumu la kujibu na kujadili hoja za rasimu na hivyo kuwa sehemu ya
Bunge Maalumu.
Alisema wakati wabunge wanahimizwa
kutumia mfumo wa maafikiano katika kuamua mambo, Rais amewajengea msingi wa
mgawanyiko na chuki, hali itakayoathiri mpango wa kulipatia taifa Katiba
inayotokana na wananchi.
Profesa Baregu alitaja baadhi ya
kauli za Rais Kikwete ambazo zinaweza kuathiri mchakato kuwa ni kujirudia kwa
kauli; “Nyie ndiyo mnaotunga Katiba (Wabunge wa Bunge Maalumu) kazi imebaki
kwenu.” na maelekezo kwamba serikali tatu zitapatikana, lakini labda baada ya
yeye (Rais Kikwete) kuondoka madarakani.
Jaji Ramadhan
Jaji Ramadhani alisema wao Tume
wamemaliza kazi yao na kwamba sasa wanawaachia wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba na wananchi waamue.
“Tumemaliza kazi yetu na sasa
tunawaachia wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi,” alisema.
Hata hivyo, alisema ikitokea wajumbe
wa Bunge hilo wakihitaji ufafanuzi wa jambo lolote, yeye binafsi anaahidi kutoa
ushirikiano.
Kuhusu hotuba ya Rais Kikwete bungeni
juzi, alisema yeye alikuwa Arusha akishughulika na vikao vya Mahakama ya
Kimataifa ya Haki za Binadamu na kwamba hakuwa amepata muda wa kuipitia na
kuitafakari kwa kiwango cha kuizungumzia.
“Ninasoma na kuitazama kupitia vyombo
vya habari na ninafahamu nyie wanahabari huwa mnalenga pale palipowakuna. Hivyo
nikitulia na kupata hotuba halisi aliyotoa nikaitafakari; nitaizungumzia,”
alieleza.
Rais Kikwete akizindua Bunge juzi
mjini Dodoma, alisema rasimu ya pili iliyowasilishwa bungeni na Jaji Warioba
ina makosa mengi ya kiuandishi.
Alisema ina mambo mengi, baadhi
yalitakiwa kuwekwa kwenye Sheria.
“Mbolea, mbegu, pembejeo vyote
vimewekwa humo, hata umri na haki ya mtoto kupewa jina vinawekwa humo,
yakiwekwa yote kama yalivyo, serikali haitaweza kuyatekeleza itashtakiwa
mahakamani kila wakati,” alieleza.
Rais Kikwete aliwataka wajumbe wa
Bunge Maalumu kusoma neno kwa neno, mstari kwa mstari na kujiridhisha na mambo
watakayoidhinisha yaingie kwenye Katiba itakayopendekezwa.
Alisema watakachoona kinafaa
kurekebishwa, kuboreshwa au kufutwa wasisite kufanya hivyo kwa sababu inatakiwa
Katiba bora, inayotekelezeka na ambayo haitalalamikiwa kiasi cha kulazimika
kuibadilisha muda mfupi baada ya kupitishwa.
Huku akishangiliwa na baadhi ya
wajumbe, alisema wakichagua Serikali tatu watatakiwa kuondoa mambo yote
yanayoweza kukanganya utendaji wa Serikali za washirika na ile ya Muungano.
Lakini wakichagua Serikali mbili, mengi yatatekelezeka.
Rais Kikwete alisema serikali zote
mbili zimeamua kwa dhati kutumia fursa ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba
kutatua mambo matatu kati ya sita ambayo bado hayajatatuliwa kutoka kwenye
orodha ya kero 31 za Muungano zilizoainishwa na Zanzibar.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment