MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba,
Kingunge Ngombere-Mwiru, alisema kuwa aliwahi kuvuliwa wadhifa wa ukuu wa mkoa
kwa sababu ya kutofautia kimtazamo na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere.
Kingunge ambaye anawakilisha kundi la
waganga wa tiba asili, alikumbushia tukio hilo juzi katika semina ya waandishi
wa habari iliyofanyika mjini hapa katika Ukumbi wa Msekwa, naye akiwa mmoja wa
watoa mada.
Akijibu swali la mwandishi wa gazeti
hili la kwanini amegeuka mlalamishi wa kukosoa viongozi wenzake wa sasa wakati
amekuwa sehemu ya serikali kwa awamu zote nne bila kutimiza wajibu wake,
Kingunge alisema kuwa amekuwa akikosoa na wakati fulani iliwahi kumgharimu.
“Wakati fulani nikiwa mkuu wa mkoa,
nilipingana na Mwalimu Nyerere nikikataa katiba isibadilishwe kwa manufaa ya
watu fulani, basi nikafukuzwa ukuu wa mkoa. Hivyo si kweli kwamba sikukosoa,
hata sasa naendelea,” alisema.
Katika mada yake kuhusu mapendekezo
ya rasimu ya Katiba mpya, alisema kuwa nchi zinazopata fursa ya kuandika upya
katiba zake, zinapaswa kujikita kuandika katiba bora zitakazoweza kuwa na
misingi ya kukuza uchumi wa kujitegemea.
“Maisha yetu yameegemea uamuzi wa
wenzetu. Tumepigania uhuru ili tujitawale lakini bado ni tegemezi na kama nchi
iko hivyo halafu nafasi ya kuandika Katiba mpya inakuja mnapanga safu za vyeo
haina maana,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment