Kambi ya Dadaab
Serikali ya Kenya imewaagiza
wakimbizi wote wanaoishi nje ya kambi za Kakuma na Dadaab kurudi katika kambi
hizo haraka iwezekanavyo.
Halkadhalika imetangaza kusitisha
usajili wa wakimbizi zaidi katika maeneo ya mijini ikiwemo Nairobi, Mombasa,
Malindi, Isiolo na Nakuru.
Haya ni wakati maafisa mia tano zaidi
wa kikosi cha usalama wametumwa katika mji mkuu Nairobi na Mombasa, ambapo watu
sita waliuawa walipofyatuliwa risasi wakiwa kanisani na watu waliojihami kwa
silaha.
Wakenya wametakiwa kuripoti kwa
polisi wakimbizi wowote watakaosalia maeneo na mijini pamoja na raia wa kigeni
wasio na vibali halali vya kuishi nyumbani.
Waziri wa usalama nchini humo Joseph
Ole Lenku amesema kuwa mkimbizi yeyote atakayepatikana nje ya kambi atakabiliwa
vilivyo na polisi.
Shambulizi lililotokea mjini Mombasa
siku ya Jumapili lilitokea huku kundi la kigaidi la Al Shabaab likiendelea
kutishia usalama wa nchi hiyo.
Hii ni hata baada ya usalama
kuimarishwa nchini humo.
Hata hivyo hakuna mtu au kundi lolote
lililokiri kufanya shambulizi hilo dhidi ya waumini wa kanisani ambapo watu
sita waliuawa.
Kundi la wanamgambo la Al Shabaab
limetoa uonyo kwa Kenya kuwa ikiwa haitaondoa wanajeshi wake nchini Somalia,
basi itaendelea kushambuliwa.
Shambulizi la kanisani mjini Mombasa,
lilitokea baada ya polisi kuwakamata washukiwa wawili walipokuwa wamejihami kwa
mabomu mawili na vilipuzi vinginevyo ambayo maafisa wa usalama walisema kuwa
yalikuwa na uwezo wa kuangusha jengo kubwa.
Waziri Lenku amesema kuwa polisi
zaidi 500 watashika doria mjini Nairobi na Mombasa.
No comments:
Post a Comment