Saturday, March 22, 2014

Mazungumzo ya amani Sudan Kusini yacheleweshwa

Duru ya  pili ya mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini imecheleweshwa   juu ya suala la nani anaweza kushiriki.

Serikali ya Sudan Kusini imeweka wazi kuwa haitaki kushiriki katika utaratibu wa amani kama kundi la viongozi wa zamani wa  kisiasa wenye vyeo vya juu ambao serikali iliwakamata baada ya mapigano kuzuka mwezi Disemba  watajiunga na mazungumzo kama kundi la  tatu.

Waziri wa zamani na mfungwa wa kisiasa, Deng Alor alisema bila ya kundi hili migawanyiko ya kisiasa katika serikali ya Juba ambayo ilisababisha mapigano kuendelea  basi hakutakuwa na amani. “ tatizo lilianza ndani ya mfumo wa kisiasa, lilianza na sisi kundi la tatu. Tunatofautiana juu ya masuala ya mageuzi na demokrasia katika chama. Tulisisitiza juu ya mageuzi. Kama unataka kutatua mzozo huu  unatakiwa kusuluhisha tofauti  ndani ya chama tawala”.

Baada ya zaidi ya miezi mitatu ya mapigano mafanikio pekee ya utaratibu wa amani yaliyopatikana  ni sitisho la  mapigano  ambalo limekuwa likikiukwa mara kwa mara  tangu mwezi Januari.

Wanadiplomasia wa kimataifa wanaishiwa  na ustahmilivu na  wiki hii waliwaonya wadau wote huko kutakuwa na madhara kwa wale ambao wanavuruga maendeleo. Alisema mwakilishi maalumu wa Marekani kwa Sudan Kusini, Donald Booth. “Kama serikali au mtu mwingine yeyote anajaribu kudumaza utaratibu wa amani na kuwakejeli  viongozi wa nchi  wanachama wa  IGAD, watakabiliwa na madhara. Watu wa Sudan Kusini wanatarajia kufanyika tena  kwa mashauriano. Wanatarajia sauti zao zitasikika  katika  kusukuma mbele amani endelevu. Biashara kama kawaida siyo njia muafaka ya kusonga mbele”.

Jenerali Taban Deng Gai anaongoza mashauriano kwa upande wa upinzani unaomtii Makamu Rais wa zamani, Riek Machar. Anasema kwamba kinyume na  serikali ya Rais Salva Kiir wao wapo tayari kwa mazungumzo na wahusika wote.

Chanzo: VOA Swahili

No comments: