Kavumbagu.PICHA|MAKTABA
By
WILBERT MOLANDI NA KHATIMU NAHEKA
MBUYU Twite na Didier Kavumbagu wa
Yanga wana siku 30 tu za kuitumikia klabu hiyo kabla ya kufanya uamuzi mgumu wa
kubaki au kuondoka Yanga. Siku hizo zinaanza leo mpaka Aprili 19 msimu
utakapomalizika na Aprili 20 watakapokuwa na kikao Jangwani kutathmini msimu
ikiwemo kupongezana kama watafanikiwa kutetea ubingwa wao.
Mastaa hao ni miongoni mwa wachezaji
wanane wa Simba na Yanga ambao wapo sokoni na wanaweza kusaini mkataba na klabu
yoyote muda wowote kuanzia sasa na siku ambazo klabu zao zitawamiliki kihalali
hazizidi 30 kuanzia sasa.
Ingawa klabu zao zimekuwa bize
kuwania nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, baadhi ya wachezaji hao
wameanza nyodo na kusisitiza kwamba hawatasaini na klabu hizo mpaka mwisho wa
msimu huku ikionekana kama wanataka kutingisha kiberiti wapewe dau nono.
Uchunguzi wa Mwanaspoti ambao
umethibitishwa na wachezaji hao umeonyesha kwamba wachezaji wa Yanga ambao
mikataba yao inamalizika mwezi Aprili 19 Ligi ya Bara itakapomalizika ni kipa,
Ali Mustapha ‘Barthez’ ambaye habari za uhakika zinaeleza mazungumzo yake ya kurejea
Simba yanakwenda vizuri, beki wa pembeni Mbuyu Twite, washambuliaji Didier
Kavumbagu na Said Bahanuzi aliyegoma kutolewa kwa mkopo kwenye usajili wa
dirisha dogo msimu huu.
Kwa upande wa Simba wachezaji wanne
ambao mikataba yao ipo ukingoni ni viungo, Uhuru Selemani na Ramadhani Chombo
‘Redondo’, kipa raia wa Ghana Yaw Berko ambao wote hata hivyo hawajawahi kuwa
na uhakika wa namba kwenye kikosi cha kwanza tangu kuanza kwa mzunguko wa pili
wa Ligi Kuu Bara.Mchezaji mwingine ni beki wa pembeni Haruna Shamte.
Twite amesisitiza kwamba hatasaini
mkataba mpya na Yanga mpaka msimu utakapomalizika huku ikitafsiriwa kwamba
anataka kutingisha kiberiti ili kurekebishiwa baadhi ya vipengele kwenye
mkataba wake na amewaambia marafiki zake wa karibu kwamba hana raha kwa jinsi
anavyoishi na vigogo wa Yanga kwa sasa.
Habari za ndani zinadai kwamba
mchezaji huyo amewahi kufanya mazungumzo na viongozi wa Azam miezi michache
iliyopita hivyo ana imani kwamba huenda wakampa ofa.
Kavumbagu ambaye amekuwa tegemeo
kwenye fowadi ya Yanga alisema: “Bado sijasaini mkataba mwingine wa kuichezea
Yanga, mkataba wangu unamalizika mwishoni mwa msimu huu (Aprili 19), ingawa
tayari nimeanza mazungumzo ya awali ambayo bado hatujafikia muafaka wa kusaini
mkataba mpya.”
Uhuru wa Simba ambaye amekuwa hana
wakati mzuri kikosini alisema: “Nikikubali kubaki Simba naamini nitaua soka
langu, hata kama wakinihitaji nibaki kwa kweli sibaki. Sasa nafikiria kuchezea
timu nyingine tofauti na Simba kwani zipo nyingi zinazoweza kunisajili maisha
popote na hilo linawezekana kutokana na kiwango changu nilichokuwa nacho,
nikimaliza mkataba wangu niondoke.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya
Yanga, Abdallah Bin Kleb alisema hawana presha na usajili wa wachezaji hao na
kwamba wanachofanya sasa ni kupigana kiume kutetea ubingwa wao kwanza na
wakishamaliza tu msimu watatatua suala la mastaa hao.
“Kwa sasa tunafikiria ubingwa kama
unavyoona ligi imefikia katika hatua ngumu,” alisema Bin Kleb ambaye ana
ushawishi mkubwa ndani ya Yanga kuanzia kwa wachezaji, wanachama mpaka viongozi
wenzake.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya
Simba, Zakaria Hanspope hayupo nchini lakini wiki iliyopita aliisisitizia
Mwanaspoti kwamba wana mpango wa kuipanga upya timu hiyo.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Simba,
Ezekiel Kamwaga alisema: “Muda wa usajili ukifika nitaweka wazi kila kitu.”
Kwa kawaida mwezi Juni ndio klabu za
Tanzania huanza kutema wachezaji zisiowahitaji tayari kwa usajili unaoanza
Julai mpaka Agosti.
Chanzo: http://www.mwanaspoti.co.tz
No comments:
Post a Comment