Dar es Salaam. Wasomi na wachambuzi
wa masuala ya kisiasa wameikosoa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa
bungeni juzi, huku wengine wakisema inaweza kulivunja Bunge Maalumu la
Mabadiliko ya Katiba.
Akifungua Bunge Maalumu la Katiba
juzi mjini Dodoma, Rais Kikwete alichambua hotuba iliyowasilishwa na Mwenyekiti
wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na kuwataka wajumbe kuukwepa muundo wa
Serikali tatu kwa kuwa hautekelezeki.
Kauli ya Rais Kikwete imekuja wakati
ambapo tayari CCM imeshaweka wazi msimamo wa kupinga muundo wa Serikali tatu
uliopendekezwa katika Rasimu ya Katiba.
Akizungumzia hotuba ya Rais Kikwete,
Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Gaudensia Mpangala,
alisema maoni ya Rais yametolewa katika wakati usiofaa.
Akifafanua, Mpangala alisema Rais
alipaswa kupinga muundo wa Serikali tatu wakati wa kutoa maoni kwenye Rasimu ya
Kwanza ya Katiba na siyo sasa.
“Yaani hotuba imefumua rasimu yote,
sijui itakuwaje. Ameleta utata zaidi. Alitakiwa kutoa uchambuzi wa mazuri na
changamoto za Serikali mbili na tatu wakati ule, siyo sasa mjadala umepamba
moto,” alisema Mpangala.
Aliongeza kuwa hotuba ya Rais
imewaacha njia panda wajumbe wanaounga mkono Serikali tatu, kwa kuwa ilionekana
kutekeleza maoni ya CCM ambayo ‘inapigania’ serikali mbili.
Pia, alikosoa sababu zilizotolewa na
Rais kuwa Serikali tatu itaua utaifa na kuanzisha uhasama miongoni mwa wananchi
na kwamba serikali hiyo haitakopesheka.
“Uhasama utatoka wapi wakati kutakuwa
na katiba na sheria zinazofuatwa?…siyo kweli kwamba Tanganyika haitakopesheka,
kwani itakuwa ndiyo nchi ya kwanza kufanya hivyo?” alihoji Mpangala.
Mchambuzi mkongwe wa masuala ya
kisiasa nchini, Dk. Ezavel Lwaitama alisema hotuba ya Rais ililenga kufuta
maoni yaliyokuwa yamewasilishwa na Jaji Warioba.
“Hotuba ile ilipangwa makusudi ili
kufuta walioshawishiwa na Jaji Warioba, ingawa siamini kama wanaotaka
Tanganyika watakuwa wamebadilisha msimamo wao,” alisema Dk. Lwaitama.
Dk. Lwaitama alisema mchakato wa
kutaka Serikali mbili unashabikiwa na baadhi ya watu wenye nia ya kugombea
urais.
“Ukiangalia kwa makini utagundua kuwa
hata wanaopigania kura ya wazi bungeni ni wale ambao wanataka kugombea urais wa
Zanzibar na Tanzania,” aliongeza.
Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema iwapo Bunge la Katiba
litaichukulia hotuba ya rais kama ni mwongozo, bunge hilo linaweza kuvunjika.
Alisema alichokifanya Rais ni kutoa
dukuduku lake, hivyo kama kuna mtu anahoja anaweza kuzijibu ili kupata katiba
inayokubalika na wengi.
“Rais alichelewa kutoa maoni kwenye
Tume ya Warioba, alichokisema wasikichukulie kuwa dira, wasome hotuba yake
sentensi kwa sentensi na ibara kwa ibara kama yeye mwenyewe alivyosema ndiyo
wataielewa,” alisema Bana.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment