Wapinzani wapinga hotuba ya JK
Dodoma. Wenyeviti wa vyama vya
Upinzani vya Chadema, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha NCCR-Mageuzi, jana
usiku walikutana ili kutoa kauli ya pamoja, kutokana na hotuba ya ufunguzi wa
Bunge kwa maelezo kuwa tayari Rais amevuruga mchakato mzima wa kupata Katiba
Mpya.
Wakati viongozi hao wakikutana,
Mwenyekiti wa Chama cha DP Mchungaji, Christopher Mtikila alisema, Rais
ameingilia mchakato na kutoa maelezo jinsi ya
kuandika Katiba.
Wakizungumza na gazeti hili jana mara
baada ya hotuba hiyo, Freeman Mbowe, James Mbatia na Profesa Ibrahim Lipumba,
walisema wameipokea kwa masikitiko makubwa hotuba hiyo.
“Tunakwenda kujadili hotuba ya Rais
na tutatoa msimamo wetu,” alisema Mbowe.
Awali Katibu wa muda wa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), Julius Mtatiro alisema Rais Jakaya Kikwete
amevuruga mchakato wa Katiba, kwani walitarajia angetumia mamlaka yake kama
Rais kuwaunganisha.
“Rais tulitarajia angeongea kama mkuu
wa nchi, lakini amezungumza kama Mwenyekiti wa CCM na kutoa msimamo juu ya
muundo wa Muungano jambo ambalo hatukulitegemea,” alisema Mtatiro.
Alisema kwa Rais kutoa msimamo ni
sawa na mwongozo jambo ambalo limevuruga mchakato mzima.
Hofu ya kuvunjika Bunge
Wakizungumza nje ya Bunge, baadhi ya
wajumbe wameeleza kuwa hotuba ya Rais Kikwete kama ikitekelezwa uwezekano wa
kupata Katiba Mpya utakuwa mgumu.
Mjumbe Luhaga Mpina alisema kwa jinsi
rasimu ilivyoandikiwa na kama muundo wa serikali mbili ukipita basi rasimu ya
Katiba itabidi iandikwe upya.
“Rasimu yote imetengenezwa kwa mfumo
wa serikali tatu sasa hapa kuna hatari ya Bunge kukwama ,” alisema.
Mtatiro kwa upande wake alisema sasa
kuna hofu ya kushindwa kupatikana Katiba Mpya kwani Rais amewachanganya wajumbe
na kama watapitisha maoni yake itabidi rasimu kuandikwa upya.
Mjumbe Mustapha Akoonay, alisema
upatikanaji wa katiba upo shakani kwani sasa upinzani utakuwa mkubwa juu ya
muundo wa muungano.
“Kwa sasa nadhani itabidi turudi upya
kwa wananchi kupata kura ya maoni juu ya muundo wa muungano,” alisema.
Lucy Owenya alisema Rais amegeuza mkutano wa Bunge kuwa ni
mkutano wa Chama Cha Mapinduzi, kwani ameshindwa kabisa kutoa mwelekeo wa nchi
na badala yake ametoa msimamo wa CCM.
“Kutokana na hili, naamini kabisa
Bunge halitakuwapo na ni bora iwe hivyo kwa kuwa amejibu hotuba ya Warioba na
kwa maana hiyo amepingana na mawazo ya wananchi.”
Godbles Lema alisema kuwa Rais hakuja
kuhutubia taifa bali alikuja kufanya semina na kujibu hotuba ya Warioba.
Mjumbe huyo ambaye ni mbunge wa
Arusha Mjini alionyesha shaka kuwa baada ya muda wa wiki tatu hakutakuwa na
Bunge la Katiba kwa kuwa wako baadhi ya watu ambao hawatakubali kilichofanywa
na Rais Kikwete.
“Waliochukua fedha ni vyema wakaenda
kumalizia nyumba zao kwa kuwa kiongozi wetu amefanikiwa kwa kiasi kikubwa
kuwafurahisha wanaCCM lakini kwa Watanzania hatutakubali,” alisema Lema.
John Cheyo alisema, “Mimi
ninachokiona ni maridhiano tu, suala la kufumua rasimu halinipi shida kwa kuwa
vitu vyote vinavyoletwa bungeni huwa ni mali ya Bunge na hivyo tutafanya
tunavyoona sisi inafaa.”
Mchungaji Peter Msigwa, alisema kuwa
kosa kubwa ambalo lilifanywa na upinzani ni kukubali na kuruhusu Jaji Warioba
atangulie kuwasilisha rasimu yake akasema hilo ndilo lililowagharimu.
Alitaka Bunge livunjwe mara moja ili
warudi kwa wananchi wakaamue na kuwahukumu kutokana na kile ambacho walikifanya
katika Bunge ambalo kwa maoni yake wamekula fedha za walipa kodi bure.
Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Edward
Lowassa aliipongeza hutuba ya Rais Jakaya Kikwete ya uzinduzi wa Bunge la
Katiba.
Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge
la Katiba, alisema kwa kifupi hotuba ya Rais Kikwete ni nzuri. Lowassa alitoa
kauli hiyo, wakati akitoka nje ya Bunge, muda mfupi baada ya Rais Jakaya
Kikwete kumaliza hotuba ya uzinduzi wa Bunge hilo.
Naye Mjumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba, Mchungaji Ernest Kadiva, alisema hotuba ya Rais imetoa mwanga kwa
wajumbe.
“Rais ameonyesha upungufu wa hoja
mbalimbali hasa katika mfumo wa serikali tatu na sasa ameacha kazi ya kuamua
tuwe na mfumo wa serikali mbili au tatu ni ya wajumbe,” alisema Mchungaji
Kadiva.
Hata hivyo, mjumbe mmoja ambaye
hakupenda kutaja jina lake alisema Rais alizungumza kama si mkuu wa nchi bali
Mwenyekiti wa CCM kwa sababu amesimamia hoja za chama chake.
Alisema hata kama mapendekezo ya Rais
Kikwete yatatekelezwa, kamwe hayatakuwa mwarobaini wa muungano. Mbunge wa
Mwibara, Khangi Lugora alisema hotuba hiyo waliitarajia na ndio maana kulikuwa
na ubishi wa nani atangulie kati ya Jaji Joseph Warioba na yeye kwa mujibu wa
kanuni.
“Hotuba ilikuwa ikijaribu kumjibu
Jaji Warioba na kwangu mimi nilikuwa naona kuwa Rais naye alikuwa anachangia
katika kuitunga Katiba kwa kupitia hotuba yake hiyo. Tumeyasikia na sisi
tutakwenda kutafakari katika kutunga Katiba ambayo itakuwa ya Watanzania wote,”
alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti
Maalumu (Chadema) Mkiwa Kimwanga, alisema kilichofanyika ni Rais kwenda kutoa
uamuzi juu ya mchakato uliokuwa ufanywe na Bunge hilo.
Kwa upande wake, Profesa Ibrahim
Lipumba, alisema hakuitendea haki Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba Bunge
hilo haliwezi kutengeneza Katiba ambayo inalenga katika mfumo wa serikali la
mbili.
“Itakuwa ni vigumu zaidi kupata
Katiba Mpya, alikuwa anapinga mambo ya msingi yaliyoelezwa katika rasimu ya
kwanza. Hayo angeyaeleza katika hatua ya awali ili rasimu hiyo ibadilishwe na
si katika hatua hii ya mwisho kabla ya kwenda kupigiwa kura na wananchi,”
alisema.
Alisema ndani ya siku 70 haiwezekani
kubadili rasimu hiyo ambayo imejikita katika muundo wa serikali tatu kwenda
katika muundo wa serikali mbili.
Ezekiah Olouch alitahadharisha
wajumbe wenzake kutodharau maoni ya wananchi waliyoyatoa katika rasimu hiyo ya
pili.
Alisema haiwezekani tume zote ambazo
zimeundwa kuangalia aina ya muundo wa serikali zije na jibu moja kuwa namna ya
kuimarisha muungano ni kuwapo kwa serikali tatu.
Jussa Ismail Ladu alisema kwa ufupi
kwamba hotuba ya Rais Kikwete imekuwa yenye sura ya CCM zaidi.
Naye Mbunge wa Lulindi, Jerome
Bwanausi, aliielezea hotuba ya Rais kuwa imeibua mambo mengi ambayo baadhi ya
watu walikuwa wakiyaelewa tofauti, hivyo imeweka uelewa mzuri katika baadhi ya
maeneo.
Profesa Costa Mahalu alisema ni
hotuba ambayo imewaachia changamoto, hasa katika eneo la muungano kwa sababu
wanahitajika kuunda muungano usiotetereka.
Sharon Shauwa, Habel Chidawali, Mussa
Juma, Editha Majura.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment