Jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alizindua rasmi mfumo mpya wa ulipaji ada katika
vyuo vya elimu ya juu, huku akisema utasaidia kudhibiti viwango vya ada
vinavyotozwa kwa wanafunzi.
Akizindua mfumo huo jijini Dar es
Salaam, Dk. Kawambwa alisema Serikali imeanzisha mfumo huo unaotarajiwa kuanza
kutumika mwaka huu katika vyuo vyote, kwa lengo la kudhibiti ada kulingana na
fani zinazotolewa.
“Sasa natarajia nitapata usingizi wa
kueleweka maana kelele za viwango vya ada zilikuwa ni kubwa, kila chuo kilikuwa
na ada yake. Niliulizwa vigezo vinavyotumika kupanga sikuwa na jibu, lakini
sasa nitakuwa na majibu tena yanayoeleweka,” alisema.
Suala la viwango vya ada katika shule
na vyuo binafsi liliwahi kuzungumziwa kwa kina siku za nyuma, huku Rais Jakaya
Kikwete na Waziri Kawambwa wakinukuliwa kwa nyakati tofauti kutaka taasisi za
elimu kupunguza viwango vya elimu. Aprili 2013 akifungua Mkutano Mkuu Maalumu
wa Chama cha Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyokuwa vya Serikali
(Tamongsco) uliofanyika mkoani Mbeya, Rais Kikwete alisema: “Elimu ni huduma
muhimu na haki kwa mtoto. Siyo vyema kugeuzwa kuwa biashara ya kuleta faida
kubwa.’’
Aliongeza kuwa Serikali ilikuwa
katika mchakato wa kutathmini ada zinazotozwa vyuoni na sekondari ili
kupendekeza viwango halisi vinavyopaswa kutozwa.
Kwa sasa udadisi wa gazeti hili
umebaini kuwa wanafunzi walioanza masomo katika mwaka wa fedha 2013/2014
wanatozwa ada kuanzia Sh360,000 kwa mwaka hadi Sh9,900,000.
Kwa mujibu wa Dk. Kawambwa, mfumo huu
ambao baadaye utaendelea hadi shule za sekondari na msingi, umepatikana kupitia
kikosi kazi cha wataalamu ambacho pamoja na majukumu mengine kilipewa kazi ya
kutathmini gharama.
Dk. Kawambwa alisema moja ya faida ya
utaratibu huo mpya ni kudhibiti taasisi zinazotoza ada kubwa kwa sababu za
binafsi ikiwamo biashara.
Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha
Tumaini Makumira cha Dar es Salaam (Tudarco), Profesa Uswege Minga alisema
endapo gharama hizo zitakuwa sawa, vyuo binafsi vitaathirika kwa sababu ni
gharama kubwa kuendesha chuo kikuu.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment