FALSAFA ya Mwenyekiti wa Bunge
Maalumu la Katiba, Samuel Sitta ya kuongoza Bunge hilo kwa kasi na viwango,
jana iliingia doa; na kulazimika kuahirisha Bunge hilo baada ya kiti chake
kutuhumiwa kuyumba katika kutetea kununi zilizopitishwa na Bunge hilo wiki tatu
zilizopita.
Hali hiyo ilijitokeza bungeni mjini
Dodoma jana muda mfupi baada ya Bunge hilo kuanza, ambapo Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu, alianza kuchangia kwa kutuhumu kiti cha Mwenyekiti wa
Bunge hilo kutetereka na kushindwa kusimamia kanuni.
Alisema ndani ya Bunge hilo viporo
vya kanuni vilivyokuwa vimebaki bila kutolewa maamuzi vilihusu kanuni ya 37 na
38 zinazohusu utaratibu wa upigaji kura, lakini inashangaza kuona wamepewa
jedwali lingine lenye mabadiliko ya kanuni kinyume cha utaratibu.
"Mheshimiwa Mwenyekiti hapa
tumeletewa jedwali lenye marekebisho ya kanuni maalumu ambazo tayari
zilipitishwa na Bunge Maalumu na kuridhiwa," alisema Lissu.
Alitaja kanuni ambazo tayari zilikuwa
zimeridhiwa na Bunge hilo, lakini zilipelekwa zikiwa kwenye jedwali hilo kwa
ajili ya kufanyiwa mabadiliko kuwa ni kanuni ya 14 (1), 32, 33,35 na 51 (1) D.
Alitaja kanuni nyingine kuwa ni 63
(1), 64 (1) ambayo ilipitishwa na azimio la Bunge na ile ya 85 (4). Lissu
alisema mabadiliko hayo ya kanuni yamesainiwa na Katibu wa Kamati ya Uongozi ya
Bunge badala ya mwenyekiti.
Alisema kuwasilishwa kwa jedwali hilo
la mabadiliko ya kanuni ni kinyume cha kanuni ya 87 (2) ambayo inaeleza
utaratibu na mapendekezo ya marekebisho ya kanuni.
"Sasa kanuni hazina hata wiki tatu
mnaanza kuzichakachua... hiki mnachotaka kukiingiza hapa kisiingizwe mpaka
yatakapoletwa mapendekezo ya kanuni ya 37 na 38," alisema Lissu na
kuongeza kuwa; "Kamati ya uongozi haina mamlaka na mambo ya kanuni."
Lissu alienda mbali zaidi na
kusisitiza kuwa; "Hii ni takataka isiingizwe ndani ya Bunge hili, huu ni
ubatili." Akikazia zaidi msimamo wake, Lissu alisisitiza; "Hatuwezi
kuruhusu uchafu wa namna hii, hii ni takataka."
Lissu wakati akitoa hoja zake alikuwa
akishangiliwa na baadhi ya wabunge na wengine kuzomea. Baada ya Lissu kumaliza
kuwasilisha hoja hiyo ya kupinga jedwali hilo la marekebisho ya kanuni, ndipo
alipofuata zamu ya Mwenyekiti wa Bunge, Sitta ambapo alisema; "Hizi ni tuhuma nzito kwa
mwenyekiti wa Bunge (Sitta) na zinaelekezwa kwake wakati hicho kinachoongelewa
hajakiona." Alisema maelekezo yalitoka kwa Kamati ya Uongozi kwenda kwenye
Kamati ya Kanuni ni halali.
Sitta, alielezea kushangazwa kabisa
na hali iliyokuwa inatokea bungeni. Wakati hali ya mvutano ikiendelea, huku
kukiwa na hali ya kutoelewana na wabunge wengine kuzungumza bila kupewa nafasi
na kiti, Sitta alikuwa alitumia busara kuwatuliza wabunge hao bila ya
mafanikio.
Baadaye Sitta, alitoa nafasi kwa
Mwanasheria wa Serikali y a Mapinduzi Zanzibar, Abubakari Hamis, ambaye alianza
akishangazwa na msingi wa kutaka kufanyika kwa mabadiliko hayo ya kanuni katika
Bunge hilo.
Alisema kifungu cha 87 (2) cha kanuni
walizozipitisha kinaeleza utaratibu wa kubadili kanuni, hivyo mtu hawezi
kujifunga na kufanya mabadiliko bila kufuata utaratibu. "Hatukubali kanuni kubadilishwa
badilishwa kinyemela, chochote ambacho kitaenda kinyume cha taratibu
hatutakubali, fuata kanuni, ukishafuata kanuni tutaheshimu lakini kinyume
hatutakubali," alisema.
Baada ya hapo Sitta, alimpa nafasi
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano, Jaji Frederick Werema, ambaye kabla
ya kuanza kutoa hoja zake alikumbana na zomeazomea kiasi cha yeye kukiri kuwa
hajazoea kuzomewa. Alisema analoliona yeye ni kuwahisha
hoja bila kusoma kanuni vizuri na kuzielewa. Alisema kanuni ya 87 fasihi ya
kwanza inaeleza vizuri jinsi ya kuzifanyia marekebisho kanuni hizo.
Mbunge wa Bunge hilo, Ismail Jussa
Ladhu, alisema inashangaza kuona kanuni ambazo hazijaanza kutumika kasoro zake
zinaanza kuonekana. "Kasoro yake yameonekana wapi?" Alihoji?
Baada ya kumaliza kusikiliza hoja za
wabunge, Sitta alisema migogoro ya kanuni huamuliwa na Kamati ya Kanuni za
Bunge. Alisema yote yaliyosemwa yawe mazuri au mabaya anayapeleka kwenye kamati
ya kanuni za Bunge yawe mazuri au mabaya.
Hatimaye mwenyekiti aliahirisha Bunge
hadi leo jioni.
Chanzo: Majira
No comments:
Post a Comment