Zanzibar. Makamu wa Kwanza wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema chama chake
cha CUF hakiko tayari kujadili mfumo wa Muungano wa serikali mbili kama
inavyotetewa na wabunge wa CCM na Rais Jakaya Kikwete.
Amesema tayari amewaandikia barua
Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuwaeleza juu ya msimamo
huo.
Maalim Seif alitoa msimamo huo jana
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Kibandamaiti mjini Unguja.
Isitoshe, alisema CUF imebaini kuwa
kuna njama za kufuta kipengele katika Katiba ya Zanzibar kinachosema; “Zanzibar
ni nchi” na kwamba hiyo ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu kwa kuwa
Wazanzibari kamwe hawatakubali kufanya hivyo.
Maalim Seif alisema haikuwa mwafaka
kwa Rais Kikwete kukosoa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba yanayotaka mfumo wa
Muungano kuwa wa serikali tatu.
Alisema Jaji Warioba aliweka kando
itikadi yake ya CCM katika utendaji wake kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba na
kuja na uamuzi huo kwa vile ndiyo tiba ya kero za Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar.
“Mapendekezo yaliyowasilishwa na Jaji
Warioba hayakuwa maoni yake, yale ni maoni ya wananchi, Tanganyika imevaa koti
la Muungano, ametoa ushahidi wake ili kujenga mwafaka katika kuendeleza
Muungano wenye mfumo wa serikali tatu,” alisema Maalim Seif.
Alisema Muungano wa serikali mbili
hauvumiliki na kama kuna watu wanaendelea kuutetea mfumo huo, Zanzibar inaweza
kutumia sheria yake ya kura ya maoni kuwauliza wananchi wanaotaka na wasiotaka
jambo hilo.
“Nimemwandikia barua Rais Kikwete,
nakala nimempelekea Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, Tanzania Bara
wanataka Zanzibar iondoe kifungu cha Katiba kinachosema Zanzibar ni nchi, jambo
hilo halitapita...tutafanya kampeni wananchi walikatae,” alieleza Katibu Mkuu
huyo wa CUF.
Alisema ni jambo la kusikitisha
katika hotuba yake alijisahau kama ni mkuu wa nchi na analihutubia Bunge
Maalumu badala yake akaegemea kuwa mwenyekiti wa CCM.
Alisema haikuwa sahihi kutoa vitisho
na kutaja ikiwa Serikali ya Muungano chini ya Serikali tatu italegalega, jeshi
litachukua madaraka ya nchi.
“Rafiki na ndugu yangu Kikwete,
usifikiri huu ni wakati ule wa Julius Nyerere, akisema yeye hakuna wa kumpinga.
Mambo yamebadilika, usijifanye ni Nyerere mpya, hakuna atakayekusikiliza na
kubabaika,” alisisitiza Maalim Seif.
Alisema ikiwa viongozi wa Muungano
wanajiandaa kutisha watu na kusababisha ghasia katika nchi, mahakama ya
kimataifa ya makosa ya jinai ipo na watakaosababisha fujo na umwagaji wa damu
watafikishwa mbele ya mikono ya sheria bila ya kujali nyadhifa na madaraka yao.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment