Rais wa Marekani Barrack Obama leo
yuko nchini Italia katika ziara ya siku sita barani Ulaya. Obama amekutana kwa
mara ya kwanza na kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis katika makao makuu
ya kanisa hilo ya Vatikani
Viongozi hao wawili wanatarajiwa
kufanya mazungumzo kuhusu ajenda kadhaa ikiwemo kutokuwepo kwa usawa katika
jamii.
Mazungumzo hayo ya kwanza kati ya
Papa wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini na Rais wa kwanza wa Marekani mwenye
asili ya Afrika yataangazia pengo kubwa lililko kati ya maskini na matajiri
duniani na pia wanatarajiwa kugusia masuala nyeti kama uavyaji mimba,ushoga ,
matumizi ya mbinu za kupanga uzazi,mchakato wa amani Mashariki ya Kati na
uhamiaji.
Obama amesema amefurahishwa kukutana
na Papa ambaye amemtaja kielelezo chema kwa watu wengi ulimwenguni akiwemo
yeye.Obama anaandamana na waziri wake wa mambo ya nje John Kerry katika ziara
hiyo ya Vatican miongoni mwa maafisa wengine wa ngazi ya juu wa serikali
yake.Obama ndiye rais wa tisa wa Marekani kufanya ziara rasmi katika makao
makuu ya kanisa Katoliki.
Obama kukutana pia na viongozi wa
serikali ya Italia
Obama pia atakutana na waziri mkuu
mpya wa Italia Matteo Renzi na Rais wa Italia Giorgio Napolitano.Uhusiano wa
kidiplomasia kati ya Marekani na Italia ni mzuri licha ya Italia kuhitaji
kushawishika zaidi kuhusu athari za kuiwekea Urusi vikwazo kwa uchumi wake.
Hapo jana akiwa mjini Brussels,Rais
huyo wa Marekani alizihimiza nchi za magharibi kusimama kidete katika kuipinga
hatua ya Urusi kulidhibiti eneo la Crimea akisema baada ya muda Urusi itatambua
kuwa matumizi ya nguvu hayawezi kushinda.
Akiuhutubia umati wa kiasi ya watu
2,000 mjini Brussels,nchini Ubelgiji, Obama alisema hatua ya Urusi imekiuka
imani kuwa haki za kimataifa zinazingatiwa,mipaka haiwezi kubatilishwa na
kwamba watu wanaweza kuamua hatma ya maisha yao ya baadaye.
Nchi za magharibi ziungane
Mapema mjini Brussels,Obama alifanya
mkutano wa dakika tisini na maafisa wakuu wa Umoja wa Ulaya ambapo alitoa wito
kwa Ulaya na Marekani kuungana kama kitu kimoja.
Ziara hii ya Obama barani Ulaya
inaonekana kuwa muhimu sana kutokana na mzozo unaoendelea kuihusu Ukraine na
mkutano huo na viongozi wa Umoja wa Ulaya ulikuwa mkutano wa kwanza wa kilele
uliofanywa na Obama pamoja na Rais wa tume ya Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy
na Jose Manuel Barosso.
Kiongozi huyo wa Marekani alisema
mzozo wa Ukraine umefichua suala la kuwa nchi kadhaa za umoja wa Ulaya
zinaitegemea pakubwa Urusi kwa ajili ya nishati na kusema kuna haja ya kutafuta
njia mbadala kukidhia mahitaji hayo ya gesi na nishati.
Suala jingine ambalo lilijadiliwa
katika mkutano huo wa Brussels ni madai ya kuwa shirika la kitaifa la usalama
la Marekani lilidukua mawasiliano ya raia wa Ulaya. Italia ndiyo kituo cha mwisho cha
ziara ya wiki nzima ya Rais huyo wa Marekani,ziara ambayo ilianzia Uholanzi na
kisha kuelekea Ubelgiji.Obama anatarajiwa kuondoka Italia hapo kesho kuelekea
Saudi Arabia.
Mwandishi:Caro Robi/Afp/dpa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman
DW.DE
No comments:
Post a Comment