Dar es Salaam. Mjadala wa Mabadiliko
ya Katiba jana ulihamia nje ya Bunge wakati Jaji Joseph Warioba alipomchambua
mhadhiri maarufu nchini, Profesa Issa Shivji akimueleza kuwa si mkweli bali
mpotoshaji wa Rasimu ya Katiba.
Jaji Warioba, ambaye ni mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, pia amemtuhumu Profesa Shivji kuwa ndiye
mwanzilishi wa chokochoko za Zanzibar za kudai serikali tatu, jambo ambalo sasa
analigeuka kutokana na kuona hali imekuwa mbaya.
Kauli ya Warioba imekuja baada ya
Profesa Shivji kuichambua Rasimu ya Katiba jana asubuhi kwenye Kongamano la
Vijana lililoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
lililokuwa na dhima ya Vijana Katika Kuimarisha na Kuendeleza Muungano Baada ya
Miaka 50. Tamasha hilo lilifanyika kwenye hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza
jijini Dar es salaam.
Akiwasilisha mada kwenye kongamano
hilo, Profesa Shivji alisema katika kujadili Muungano, wananchi hawana budi
kuzingatia mambo mawili ambayo ni nchi zinazozungumziwa kwenye Rasimu kuwa ni
Zanzibar, Tanganyika au Tanzania, ambayo alisema haina mamlaka katika pande
hizo mbili za Muungano.
Pia alisema suala la maadili kwa
viongozi halina budi kuangalia kuwa linazungumzia maadili ya viongozi wa
Zanzibar, Tanganyika au Tanzania na kwamba rasimu inazungumzia viongozi wa
Tanzania ambao hawana mamlaka kwa Tanganyika na Zanzibar.
Katika majumuisho yake, Profesa
Shivji, ambaye aliikosoa Rasimu kuwa haiwakilishi matakwa ya Watanzania kwa
kuangalia sampuli zilizotumika, alisema kwamba wajumbe wa Tume ya Jaji Warioba
walikuwa na nia njema.
Lakini Shivji akaenda mbali zaidi kwa
kusema “the road to hell is paved in good intention,” akimaanisha kuwa njia ya
kuzimu imetengenezwa kwa nia njema.
Akijibu hoja hizo, Jaji Warioba
alisema Profesa Shivji amegeuka maandishi yake yaliyokuwa yanachochea utaifa wa
Zanzibar na sasa anaona Tanganyika ndiyo hatari kwa Muungano.
“Shivji ni msomi na mimi najua
anaelewa matumizi ya takwimu,” alisema Jaji Warioba, ambaye aliwahi kuwa Waziri
Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakati alipozungumza na gazeti hili
nyumbani kwake jana jioni.
“Nasema hapa, Shivji akiwa msomi,
amekuwa intellectually dishonest (si mkweli kiusomi). Anapotosha kwa makusudi.”
Jaji warioba alisema Shivji ndiye
amekuwa chanzo cha uchochezi wa kitaifa Zanzibar kupitia maandishi yake.
Alisema waliokuwa wanadai serikali tatu kwa muda mrefu walikuwa wananchi wa
Zanzibar.
“Shivji alikuwa anasema Tanganyika
imejificha kwenye Muungano ili inufaike. Kwa hiyo anasema Tanganyika iwe wazi
isijifiche,” alisema Jaji Warioba.
“Na Shivji amechochea hilo… wote wale
waliokuwa wanamnukuu walikuwa wanatoa hayo kwenye maandishi yake na kwamba
mpaka leo hii kuna watu wa Zanzibar wanaamini Muungano huu si halali kisheria
kutokana na Shivji ambaye alisema Baraza la Mapinduzi halikuridhia articles
(ibara) za Muungano.”
Alipoulizwa jana usiku kuhusu tuhuma
hizo za uchochezi na chanzo cha hisia za utaifa wa Uzanzibari na Utanganyika,
Profesa Shivji alisema hawezi kujibu tuhuma hizo kwa kuwa hajamsikia Jaji
Warioba akizungumzia hilo.
“Hey, amezungumza lini?” alihoji.
“Siwezi kujibu kwa kuwa sijamsikiliza mwenyewe.”
Lakini Jaji Warioba alisema watu
walitumia msingi huo kudai utaifa wa Zanzibar na kusisitiza kuwa Shivji
amesababisha hisia za utaifa na kwamba haya yanayoendelea sasa yanatokana
uchochezi huo.
“Hata kabla ya sisi kuanza mchakato
huu, Shivji alikwenda Zanzibar akazungumza na Baraza la Wawakilishi na
akawaambia issue kwa Zanzibar ni self determination (kujitambua), Sasa leo
anaona kama hatari ni Tanganyika, lakini yeye ndio amechochea nationalism
(utaifa),” alisema Jaji Warioba.
Kuhusu takwimu, Jaji Warioba alisema
mara ya kwanza Profesa Shivji alizungumzia takwimu za Zanzibar kuhusu muundo wa
Muungano akisema kuwa waliozungumzia suala hilo walikuwa 47,000, huku watu
27,000 wakitoka Tanzania Bara na 19,000 kutoka Zanzibar.
“Safari hii ametaja zile za Tanzania Bara na
kusema hiyo ni figure (namba) ndogo sana ukilinganisha na watu 300,000 waliotoa
maoni,” alisema Warioba.
Alisema Tume ilitumia takwimu
zinatokana na watu waliozungumzia suala ambalo wameliwekea asilimia na si kwa
ujumla na ndio maana anaona Profesa Shivji anataka kupotosha kwa makusudi.
Warioba alimuelezea Profesa Shivji
kuwa sasa ameamua kueneza propaganda za serikali mbili kwa kuponda Rasimu ya
Katiba ambayo inaonyesha kuwa muundo wa serikali tatu ndio unaoifaa Tanzani kwa
sasa.
Aidha, Warioba alisema msimamo wa
Profesa Shivji ni kwamba Zanzibar haikukosea kubadilisha Katiba mwaka 2010.
“ Nimeshangazwa na Shivji kusema
kwamba kitendo cha Zanzibar kubadili Katiba yao kuwa ‘Zanzibar ni Nchi’
halikuwa jambo la ajabu,” alisema Warioba.
Alisema Shivji ni msomi ambaye
anafahamu kitendo cha kubadilisha Katiba kilikuwa na madhara makubwa katika
muundo wa Muungano.
“Nadhani mnakumbuka Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda alipoulizwa Bungeni kama Zanzibar ni nchi au siyo nchi, alijibu
kuwa Zanzibar siyo nchi, vurugu zake mnakumbuka,” alisema.
Alisema lakini msomi kama Shivji
haoni kama suala hilo la ‘Zanzibar ni nchi’ lina madhara makubwa katika
mstakabali wa taifa letu.
Jaji Warioba alisema kama serikali
tatu hazitakiwi, basi kinachotakiwa kufanywa ni kwa Zanzibar kubadili Katiba
yake ili iseme kwamba Zanzibar ni sehemu ya Muungano, vinginevyo haiwezekani.
“Maana kama ni kusahihisha, ni lazima
kwanza Katiba ya Zanzibar itumie maneno yale yale yaliyo kwenye Katiba ya
Muungano. Yaani Zanzibar iwe sehemu ya nchi. Zanzibar wakubali hilo,” alisema.
“Zanzibar wakubali Rais wa Muungano
ana madaraka nchi nzima maana mabadiliko ya 2010 yamemuondolea Rais wa Jamhuri
ya Muungano madaraka yake.”
Akitoa mfano wa mbunge wa Simanjiro,
Christopher Ole Sendeka, Jaji Warioba alisema amekuwa akidai takwimu
hazionyeshi uhalisia wa maoni ya wananchi.
“Kwa mfano, Jimbo la Simanjiro
linakuwa na watu 100,000 lakini waliojiandikisha kupiga kura ni watu 20,000 na
waliopiga kura ni watu 15,000. Hii ina maana ushindi wake utakuwa katika watu
waliopiga kura na siyo idadi ya watu wa Simanjiro,” alisema Warioba.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment