Saturday, March 22, 2014

Mkapa, Sumaye wakosa uzinduzi Bunge la Katiba

Dodoma. Rais mstaafu, Benjamin Mkapa na mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Cleopa Msuya, jana hawakuhudhuria uzinduzi wa Bunge la Maalumu la Katiba kama ambavyo ilitangazwa na Katibu wa Bunge la Katiba.

Katibu wa Bunge la Katiba Yahaya Khamis Hamad, alitangaza juzi kuwa viongozi wote wastaafu, wamealikwa katika shughuli za uzinduzi  huo wa kihistoria wa Bunge hilo.

Wengine ambao hawakuhudhuria ni Rais mstaafu wa Zanzibar Dk Salmin Amour na Waziri mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim na mke wa Rais wa kwanza wa Zanzibar,  Fatma Karume.

Viongozi walio madarakani waliohudhuria uzinduzi huo ni Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein aliyefika saa 9:23, Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Rais na Dk Mohamed Gharib Bilal aliyewasili Viwanja vya Bunge saa 9:28 alasiri.

Rais Jakaya Kikwete alifika katika viwanja hivyo saa 9:42 ambapo alipokewa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta na baadaye kukagua gwaride lililoandaliwa maalumu kwa ajili ya uzinduzi wa Bunge la Katiba.

Baadhi ya viongozi wakuu wastaafu waliohudhuria ni Ali Hassan Mwinyi, aliyewasili Viwanja vya Bunge saa 9:10 na Rais mstaafu wa Zanzibar, Aman Karume,  aliyewasili saa 9:06.

Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu John Malecela, ambaye aliwasili Viwanja vya Bunge saa 9:13, mke wa Baba wa Taifa Maria Nyerere na Spika wa Bunge mstaafu Pius Msekwa.

Pia alikuwapo mke wa Rais, Salma Kikwete, mke wa Makamu wa Rais, Asha Bilal, mke wa Rais wa Zanzibar, Mwamwema Shein na mke wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Tunu Pinda.

Katiba inayotumika sasa ya mwaka 1977 imefanyiwa marekebisho mara 14.  Bunge hilo la Katiba linatarajiwa kuanza kazi zake Jumatatu ijayo.

Chanzo: Mwananchi

No comments: