WANALAMBALAMBA Azam FC jana walizidi
kudhihirisha kuwa wabishi na kuzidi kujikita kileleni baada ya kuilaza Simba
kwa mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom uliofanyika kwenye Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam.
Wakati Azam FC ikizidi kubaki njia
kuu na kulinda rekodi ya kutopoteza mchezo hata mmoja tangu ligi hiyo kuanza
msimu huu, mabingwa watetezi Yanga, walichepukia Tanga na kujikuta wakishindwa
kulimudu gwaride la Mgambo JKT kwa kukubali kichapo cha mabao 2-1 kwenye Uwanja
wa Mkwakwani katika pambano lililotawaliwa na imani za kishirikina.
Katika Dimba la Taifa, kila timu
ilianza kwa kasi na kushambuliana kwa zamu, ambapo dakika ya nane, Azam
walilifikia lango la Simba na kumlazimisha kipa Ivo Mapunda kufanya kazi ya
ziada kutokea na kumzuia Kipre Tchetche asifunge.
Simba walijibu mashambulizi dakika ya
12, kwa winga wake Ramadhani Singano ‘Messi’ kupiga shuti kali la mbali nje ya
boksi na kudakwa na mlinda mlango, Aishi Manula.
Kutokana na kosa kosa hiyo, ndipo
ilipobainika kuwa mashabiki wa Yanga walikuwa wakiishangilia Simba, tukio
lililojibiwa kwa kuzomewa na mashabiki wa Simba.
Dakika ya 14, Mapunda kwa mara
nyingine alifanya kazi ya ziada kupaa juu na kuokoa shuti la Khamisi Mcha
‘Vialli’ lililotokana na adhabu ndogo ‘free kick’.
Baada ya kosa kosa hiyo, Mcha
alisawazisha makosa kwa kuifungia Azam bao dakika ya 17 kwa shuti jepesi ndani
ya boksi, hivyo kuibua mgawanyiko miongoni mwa mashabiki wa Simba, ambao nusu
walilishangilia.
Mashabiki hao walilishangilia kama
ishara ya kushangilia anguko la Yanga, ambayo mashabiki wake walikuwa
wakiishangilia Simba ili iifunge Azam na kuwajengea mazingira ya kutetea taji
la Ligi Kuu.
Dakika ya 22, Singano alikosa bao la
kuisawazishia Simba kwa shuti lake kupaa sentimita chache juu ya lango, kabla
ya Amisi Tambwe naye kushindwa kufunga kwa kichwa, akiunganisha krosi ya
Singano dakika ya 30.
Mcha, dakika 10 kabla ya filimbi ya
mapumziko, aliikosesha Azam bao jingine, akishindwa kumalizia kazi maridadi ya
Kipre.
Wakati mashabiki wakiamini mpira
utaingia mapumziko Azam wakiwa mbele kwa bao 1-0, beki Joseph Owino
aliisawazishia timu yake kwa kichwa dakika ya 45, akiitendea haki krosi ya
Chanongo ambaye alikuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Wanalambalamba.
Kipindi cah pili nacho kilianza kwa
mashambulizi, kwa kila upande kusaka bao la ushindi, hivyo kushuhudiwa kosakosa
kadhaa.
Kipindi cha pili, Azam waliingia kwa
nguvu na dakika ya 57, walipata bao la pili lililofungwa na John Bocco
‘Adebayor’ kwa kichwa, akiunganisha mpira wa ‘tik tak’ ya Kipre iliyogonga
mwamba na kurudi uwanjani.
Baada ya kufunga bao hilo, Azam
ilionekana kupunguza kasi, hasa baada ya kutolewa Kipre ambaye alikuwa msumbufu
katika safu ya ulinzi ya Simba.
Simba ikiwatumia vijana wake
Chanongo, Mkude, Singano na wakongwe Uhuru na Tambwe, waliendelea kushambulia
bila mafanikio.
Jitihada za Simba kusaka bao la
kusawazisha nusura zizae matunda dakika ya 64, pale Tambwe alipokosa bao la
kichwa akiwa na nyavu, kuunganisha krosi ya Chanongo.
Hadi mwamuzi Israel Nkongo
akihitimisha dakika 90, Azam walitoka kidedea kwa mabao 2-1.
Kwa ushindi huo, Azam FC imefikisha
pointi 53 na kuzidi kuitimulia vumbi Yanga iliyosalia na pointi 46.
Azam FC: Aishi Manula, Erasto Nyoni,
Michael Gadiel, Aggrey Morris, David Mwantika, Kipre Balou, Himid Mao/ Bryson
Rafael, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Kipre Tchetche/ Bryan Umony, John Bocco na
Khamis Mcha ‘Vialli’/Kelvin Friday.
Simba: Ivo Mapunda, William Lucian,
Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Joseph Owino, Donald Musoti, Jonas Mkunde, Haruna
Chanongo/Awadh Juma, Henry Joseph/Abdulhalim Humud, Amisi Tambwe, Uhuru
Suleiman na Ramadhani Singano ‘Messi’/Badru Ally.
Jijini Tanga, Mgambo walianza
kujipatia bao dakika ya kwanza, likifungwa na Fully Maganga.
Dakika ya 30, Mohamed Neto alilimwa
kadi nyekundu na mwamuzi aliyejulikana kwa jina la Mahadhi, kwa madai ya
kukutwa na kinachodaiwa kuwa ni ‘hirizi’ ndani ya nyeti zake. Hadi dakika 45,
bao lilikuwa hilo moja.
Kupungua kwa Mgambo, kuliwaongezea
nguvu Yanga ambao walizidi kuliandama lango la wapinzani wao na kufanikiwa
kupata penalti dakika ya 52 baada ya beki mmoja kuunawa mpira eneo la hatari.
Penalti hiyo ilifungwa na Nadir Haroub ‘Canavaro’. Matokeo yaliyodumu hadi
mapumziko.
Kipindi cha pili, licha ya Mgambo
kuwa pungufu, ilicheza mchezo wa kujihami na kushambulia kwa kushtukiza na
dakika ya 64 Kelvin Yondani aliunawa mpira eneo la hatari na kuamriwa penalti
iliyofungwa na Malimi Busungu.
Huko Mbeya, Tanzania Prisons ilizidi
kukalia kuti kavu baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kwa Mbeya City,
likifungwa na Paulo Nonga, dakika ya pili.
Huko Kaitaba Kagera, maafande wa Ruvu
Shooting walilazimisha sare ya bila kufungana na wenyeji Kagera Sugar.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment