Saturday, March 29, 2014

Kura mchanganyiko Bunge la Katiba

Dodoma.Wajumbe wa Kamati ya Maridhiano jana walinusuru Bunge Maalumu la Katiba kuvunjika, baada ya kukubaliana kutumika kwa utaratibu wa upigaji kura wa wazi na siri kama ilivyopendekezwa na Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge.

Wajumbe hao walitangaza uamuzi huo bungeni kutokana na makubaliano yaliyofikiwa katika kamati ndogo ya maridhiano iliyofanyika jana asubuhi baada ya kushindwa kuafikiana katika kikao cha awali kilichofanyika juzi kuanzia saa 3:00 usiku hadi usiku wa manane ili kunusuru kukwama kwa Bunge hilo.

Kabla ya uamuzi huo, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta alisema juzi usiku walikutana hadi usiku wa manane baada ya hapo, walikabidhi kamati ndogo yenye mchanganyiko wa wajumbe kutoka Kamati ya Kanuni na Kamati ya Maridhiano.

“Baada ya kukamilisha kazi, wajumbe wa kamati ndogo watatoa taarifa hapa ambao ni John Mnyika, Profesa Ibrahimu Lipumba, Vual Ali Vual na Askofu Donald Mtetemela,”alisema Sitta.

Akitoa taarifa ya maridhiano hayo, kwa niaba Freeman Mbowe, Mjumbe John Mnyika alisema, alianza kwa kunukuu kitabu kilichoandikwa na Mwalimu Nyerere, mwaka 1962 chenye ujumbe mahususi kwa Chama cha TANU akisema ujumbe huo kwa sasa ni sahihi kwa watu wengi na taasisi ikiwamo CCM.

Mnyika pia alisema Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) hawana nia yoyote ya kuvuruga mchakato wa katiba kama ambavyo imeelezwa katika siku za karibuni na viongozi, kwani wazo la kutaka Katiba Mpya imekuwa ni kilio chao cha muda mrefu.

Naye Profesa Lipumba alisema suala ambalo tumekuwa tukisimamia kwa muda mrefu suala ambalo lina utata, kati ambao wanapenda kura za uwazi na wale wa siri.

Alisema: “Tuliletewa mchanganyiko wa uwazi na siri, lakini maana yake ni kura ya uwazi, wenzetu wamekuwa na msimamo mkali hata hili la kufanya uamuzi ilikuwa tufanye kwa siri, lakini hata hivyo hawakukubali.”

“Tulifanya uamuzi ili tusonge mbele, basi tulipendekeza upigaji kura wa kuamua tupige kura kwa mfumo wa siri, lakini pia wenzetu walikataa,”alisema Profesa Lipumba.

Alisema kwa kuzingatia kutokwama kwa zoezi la kuanza kujadili rasimu, wameamua kukubali kutokubaliana.

“Ili kusonga mbele tunahitaji kusonga mbele tuanze kujadili Katiba, natoa wito kwa wenzangu wa chama tawala kwa kuwa mpo wengi mnadhamana kubwa, ni vyema mkawa na utaratibu wa kuwasikiliza wachache,” alisema.

Mjumbe Vuai Ali Vuai alisema, wamefikia maridhiano hayo, ili kuwezesha kuendelea na mchakato wa katiba mpya kwani kila upande uliendelea kutetea msimamo wake hata katika kikao cha maridhiano.

“Yapo mambo yalijitokeza kwenye kamati ambayo ni mengi, tulidhani hapa tunakuja kueleza yale ambayo tunakubaliana kulikuwa na hoja nyingi kuwa CCM hatutaki kuendeleza mchakato, lakini nilisema CCM tutakuwa wa mwisho kusitisha mchakato wa Katiba,” alisema.

Alisema kwa mustakabali wa taifa waliamua kupitisha uamuzi wa kukubali kura za siri na wazi kwa pamoja.

Naye Askofu Mtelemela aliomba wajumbe kukubali maridhiano ambayo, wamefikia ili kuweza kusonga mbele katika kuanza kujadili mchakato wa Katiba.

Askofu Mtetemela alisema baada ya majadiliano, wamekubaliana kurudi kwenye azimio la Kamati ili kuruhusu kuendelea na kazi ya kujadili rasimu ya Katiba.

“Jambo zuri ambalo limejitokeza sote tuna nia njema kwa ajili ya Bunge hili maalumu kuhakikisha mchakato wa kupatikana Katiba Mpya haukwami,” alisema.

Alisema kwa siku 40 sasa wamekuwa wakijadili suala moja tu la kanuni, kazi ambayo inasubiriwa ya kujadili rasimu ya Katiba.



Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge

Baada ya taarifa hiyo ya Kamati ya Maridhiano, Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, Pandu Ameir Kificho, pamoja na wajumbe wa kamati hiyo, Profesa Costa Mahalu na William Ole Nasha, walitoa ufafanuzi wa kisheria kuhusiana na kanuni hizo.

Hata hivyo, kwa pamoja walieleza kuwa uamuzi wa utekelezaji ya kanuni ya 37 na 38 yaliyokuwa ya yameachwa kama kiporo, yakikamilika kutawezesha kuendelea na mchakato ya Katiba.

Baada ya kamati kuridhia makubaliano hayo, zoezi la upigaji kura kuhusu uamuzi wa awali kama kura zipigwe kwa mfumo uliopendekezwa wa kura za siri na wazi ulianza.

Matokeo ya kura

Akitangaza matokeo haya, Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu alisema idadi ya wajumbe waliokuwa katika ukumbi ilikuwa 511, waliopiga kura walikuwa 509.

Alisema waliopiga kura ya wazi walikuwa 438 kati yao 351 walipiga kura ya ndiyo na 87 walipiga kura ya hapana.

Suluhu alisema waliopiga kura ya siri walikuwa wajumbe 71, kati yao 25 walipiga kura ya ndiyo huku wajumbe 46 wakipiga kura ya hapana.

Alisema jumla ya wajumbe waliopiga kura ya ndiyo ni 376 na waliopiga kura ya hapana walikuwa wajumbe 133. Katika matokeo hayo wajumbe wawili hawakupiga kura ingawa waliokuwamo bungeni.

Kutokana na matokeo hayo Bunge hilo sasa litatumia utaratibu wa kupiga kura ya wazi na siri kwenye uamuzi wake katika kupitisha vifungu vya rasimu.

Mjumbe awananga wenzake

Mjumbe wa Bunge la Katiba, Paul Gekul amewashambulia wabunge wa Katiba wanaotoka kundi la CCM kuwa ni wanafiki wanaojipendekeza kwa sauti, lakini matendo yao hayaendani nao.

Gekul alisema kitendo cha wabunge hao kulazimisha kupiga kura za wazi ili wasikike na wapiga kura wao ni sawa na unafiki kwa kuwa katika majimbo yao hakuna maendeleo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hivi juzi tulitoka katika Jimbo la Uchaguzi la Kalenga (Iringa) kati ya kata 17 ni kata tatu ndizo zenye umeme, leo hii wanaposema wanataka kura ya wazi siyo haki,” alisema Gekul.

Alipinga kauli za wabunge kuwa wapinzani ndiyo wanaotaka kupinga na kuvuruga mchakato wa Katiba kwa kusema wao ndiyo waliokuwa wa kwanza kuomba Katiba Mpya hivyo hawatakuwa tayari kuvuruga utaratibu huo.

Katika mchango wake mbunge huyo ambao ulionekana kujikita zaidi kwenye vijembe badala ya hoja ya kura za siri au wazi, alisema hakuna chochote ambacho viongozi wa CCM wamefanya kwa kipindi cha miaka 50.

Alitolea mfano wa majiji na miji mikubwa ambayo yanaongozwa na wabunge wa Chadema kuwa wanataka kura ya siri ili watafute mwafaka wa maendeleo ya nchi yao.

Wabunge CCM wajilipua

Wabunge wa watatu wa Chama Cha Mapinduzi, Mjumbe Kangi Lugola, Deo Filikunjombe na Ester Bulaya, kwa mara nyingine jana walijilipua kwa kukataa pendekezo la chama chao kuhusu upigaji wa kura wa aina mbili.

Filikunjombe alitoa kauli ya hapana kuonyesha anapinga kauli ya kupiga kura za ndiyo kwa wanaotaka na hapana kwa wanaotaka pendekezo lililokuwa limetolewa na Kamati ya Kanuni ambalo ndilo lililoungwa mkono na wajumbe wote wa CCM.

Hii siyo mara ya kwanza kwa Filikunjombe kwenda kinyume na msimamo wa chama chake, mwaka juzi alikataa kuunga mkono bajeti ya Serikali na hata katika mapendekezo mengi hupingana na wenzake kwa misimamo.

Filikunjombe

Filikunjombe akizungumza na gazeti hili alisema aliamua kupiga kura ya hapana kwa sababu ni uamuzi ambao hauna msimamo.

Walitakiwa kupitisha upigaji kura ama uwe wa wazi au wa siri.

Alisema yeye angekuwa mwenyekiti angetumia falsafa ya kidemokrasia ya kusikiliza maoni ya pande zote hasa wale wachache kusikiliza hoja zao kwa makini.

Mjumbe huyo alisema katika Bunge hili wanaotaka kura za wazi wapo wenge, ila hoja zao ni dhaifu na kwamba wanaotaka kura za siri ni wachache lakini hoja zao ni nzito na zina mashiko.

Awali wabunge wengi walionekana kupingana na uamuzi wa chama chao, lakini jana wengi waliamua kutoka nje bila ya kueleza misimamo yao hadharani.

Waliokuwa wamejipambanua kuwa wangepinga ni pamoja na mbunge wa Kahama James Lembeli, Ester Bulaya, Kangi Lugola na Mohamed Keissy.

Hata hivyo, muda mfupi jana kabla ya kuanza upigaji wa kura, ni Lembeli pekee ambaye hakuwapo katika Viwanja vya Bunge, lakini wajumbe wengine Keissy aliunga mkono kwa kauli ya ndiyo, huku Ester Bulaya alipiga kura ya siri na Lugola alisema alipiga kura ya wazi akisema hapana.

Wakati wabunge hao wakipinga, wabunge wengine kutoka vyama vya upinzani waliunga mkono azimio hilo kitendo kilichoibua mshangao mkubwa bungeni.

Waliounga mkono ni Augustine Mrema (TLP), Hamad Rashid Mohamed (CUF), Kuga Mziray (APPT), Fahmy Dovutwa (UPDP), huku John Shibuda aliomba karatasi apelekwe mahali alipo ili kupiga kura ya siri kwa sababu alisema anaumwa mguu.

Hata hivyo, wabunge wa upinzani walitofautiana wengine waliamua kupiga kura ya wazi kwa kusema hapana na wengine waliamua kupiga kura ya siri.

Moja wa wajumbe ambao hawakupiga kura ni Godbless Lema ambaye alisema hakupiga kura kwa sababu uamuzi wa Bunge hilo kutumia kura ya wazi na siri kwa pamoja hauna tija.


Mussa Juma, Habel Chidawali, Sharon Sauwa, Editha Majura na Beatrice Moses, Dar es Salaam. (Chanzo: Mwananchi)

No comments: