Wakati kikao cha Bunge Maalum la
Katiba nchini Tanzania kikiahirishwa tena, dalili zinaonesha hali ni ngumu na
uwezakano wa kufikia muafaka kwa hatima ya taifa hilo la mashariki ya Afrika
uko mbali kupatikana.
Asubuhi ya leo, Spika Samuel Siita
anayeongoza bunge hilo maalum alitumia dakika zisizodi 20 kuongoza kikao na
baadaye kukiahirisha, licha ya jioni ya jana (25 Machi 2014) kusema kwamba
ajenda za leo zingejumuisha ruhusa ya mjadala wa hotuba ya wiki iliyopita iliyotolewa
na Rais Jakaya Kikwete kwenye bunge hilo na kuzua utata mkubwa.
Mmoja wa waasisi wa Muungano wa Tanzania ambao umekuwa mada kuu kwenye Katiba Mpya, Marehemu Mwalimu Julius Nyerere.
Pia ilikuwa imekubalika kuwa hata
hotuba ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, nayo
ingelijadiliwa na wajumbe wa Bunge hilo la kwanza la aina yake ndani ya kipindi
cha miaka 50 ya Muungano wa Tanzania.
Bunge lagawika tena
Hata hivyo, wakati akiahirisha kikao
cha leo, Spika Sitta alitangaza kwamba hotuba hizo zisingelikuwa tena sehemu ya
mjadala wa sasa.
"Baada ya hoja mbalimbali
kujitokeza hapa (bungeni) nilikuwa nimeridhika kwamba kungelikuwa na uwezekano
wa kujadili hotuba zile mbili nzito (ya Rais Kikwete na Jaji Warioba), lakini
baada ya mashauriano ya kina na makundi mbalimbali, imeonekana kwamba kufanya
hivyo ni kama kutanguliza mjadala kuhusu rasimu yenyewe ya katiba kabla ya
wakati wake." Alisema Spika Sitta akiongeza kwamba badala yake wajumbe wa
Bunge Maalum la Katiba wanapaswa kuzichukulia hotuba hizo mbili kama nyenzo za
kuwaandaa kuijadili Rasimu ya Katiba na sio kuzijadili hotuba zenyewe.
Kauli hiyo ya Spika Sitta ilipokelewa
vyema na wajumbe wanaotokana na Chama tawala cha Mapinduzi (CCM) kwenye bunge
hilo, lakini wajumbe kadhaa wanaowakilisha upinzani na makundi mengine
yasiyokuwa ya kisiasa walionekana wakiinuka kuomba muongozo.
Hata hivyo, Spika Sitta alitangaza
kwamba kikao hicho kifupi kabisa cha asubuhi kisingelipokea muongozo wowote na
kwamba miongozo yoyote ingelipata nafasi baadaye jioni ya leo wakati
litakaporudi kwenye mjadala.
UKAWA kuendelea kushiriki
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi
(CUF) na mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Profesa Ibrahim Lipumba.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi
(CUF) na mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Profesa Ibrahim Lipumba. Ajenda nyengine ambayo ilikuwa
iamuliwe asubuhi ya leo ni ile ya upigaji kura kwenye bunge hilo, iliyowahi
kuzua utata kabla ya kuwasilishwa kwa rasimu.
Katika wiki mbili nzima za mwanzoni,
bunge hilo lilikwama kwenye vifungu namba 37 na 38 vya kanuni za uendeshaji
ambavyo vilihusu upigaji wa kura ama ya siri au ya wazi.
Kwa sasa, bunge hilo limekwama juu ya
ama wajumbe wa kile kinachotambuliwa kama Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
wengi wao kutoka vyama vya upinzani, wataendelea kushiriki kwenye vikao hivyo
ama la.
Hii ni baada ya hapo jana kujiuzulu
nafasi ya ujumbe kamati ya uongozi wa bunge kwa mwenyekiti wa Chama cha
Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, baada ya kuteuliwa na Spika Sitta.
Hata hivyo, akizungumza na DW mapema
leo, Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, amesema kwamba bado wataendelea
kushiriki kwenye vikao, ingawa wataendelea kupigania mageuzi ya msingi kwenye
uendeshaji wa Bunge hilo ambalo linatakiwa kutoka na Katiba Mpya itakayopigiwa
kura ya maoni ndani ya kipindi kisichozidi miezi miwili kutoka sasa.
Mwandishi: Mohammed Khelef/DW
Kiswahili
Mhariri: Mohamed Abdulrahman
DW.DE
No comments:
Post a Comment