VITISHO vya watendaji wa serikali kwa
vyombo vya habari vimezidi kushika kasi, safari hii Naibu Waziri wa Habari,
Michezo na Utamaduni, Juma Nkamia, akitishia kuvifungia au kuvifuta.
Nkamia amebainisha kuwa magazeti
yanayowachafua watu, serikali na kuhatarisha usalama wa nchi yatakumbana na
kifungo.
Itakumbukwa mwaka jana serikali
ililifungia gazeti la Mtanzania kwa miezi mitatu na Mwananchi kwa wiki mbili,
kwa madai ya kuandika habari za kichochezi.
Nkamia, alitoa vitisho hivyo jana jijini hapa kwenye tamasha la vijana lililoandaliwa na
Taasisi ya Voice of Youth (VOYC) lililokuwa likijadili masuala mbalimbali
yahusuyo vijana.
Miongoni mwa mambo yaliyokuwa
yakijadiliwa ni ujira, uzalendo, ujasiriamali na ajira,
Nkamia alisema hatakubali siku moja
asutwe kwa kutotimiza wajibu wake katika wizara anayoisimamia, kwa kuwaachia
waandishi wasiofuata maadili ya taaluma yao.
“Mimi sitaki kufanya kazi na
waaandishi wa habari makanjanja, ambao si makini na wanaofanya kazi kwa
masilahi ya kundi fulani la watu.
“Tutakifuta, kukifungia chombo
chochote cha habari pamoja na waandishi wake wanaokwenda kinyume cha maadili ya
uandishi wa habari, sitaruhusu wanaoendekeza kuwachafua wengine, umbea,” alisema.
Alisema amefanya kazi hiyo kwa
kuzingatia maadili ya taaluma hiyo kabla ya kuingia kwenye siasa ambako sasa
anasimamia wizara inayoshughulika na waandishi wa habari.
Nkamia pia alitumia fursa hiyo
kuwasihi vijana waache kushiriki kwenye maandamano yanayoitishwa na vyama vya
siasa alivyoviita havina malengo mema kwa taifa.
Alibainisha kuwa vijana hawawezi
kupatiwa fedha kama hawafanyi kazi yoyote, kwani hata mataifa yaliyoendelea
ambayo ni Marekani na Uingereza hawafanyi hivyo.
Hata hivyo katika mkutano huo,
viongozi wa halmashauri na mkoa walikacha kuhudhuria na hawakutuma wawakilishi
katika tamasha hilo licha ya kualikwa.
Kukacha kwao huko kulisababisha gumzo
kubwa na Afisa Tarafa ya Nyamagana, Maximilian Kailanga, alibeba jukumu la
kumkaribisha Nkamia.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment