CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezidi
kuilaumu iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuandika rasimu iliyojaa
mawazo ya wajumbe wake waliotaka muundo wa serikali tatu.
Lawama hizo zilitolewa jana na Katibu
Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, katika mkutano wa hadhara uliofanyika
katika viwanja vya Mwembeyanga jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliandaliwa kwa lengo la
kumpongeza Rais Jakaya Kikwete, kwa hotuba aliyoitoa bungeni Machi 21, ambapo
Kinana alisema tume hiyo iliyokuwa chini ya kada wao Jaji Joseph Warioba,
haikueleza ni makundi mangapi yalitaka serikali tatu.
Kinana alisema Tume ya Mabadiliko ya
Katiba walisubiri Mwalimu Julius Nyerere afe ndipo waseme serikali tatu, kwani
walikuwepo enzi hizo.
“Muungwana angesema nani kasema nini
wakati wa kuchukua maoni, tume haijasema katika mabaraza 171 ni mangapi
yalitaka serikali tatu, ukiwauliza mara makaratasi yamepotea, hatukumbuki.
“Tusitoane meno na macho kwa ajili ya
Katiba, kwani ikishatengenezwa itawekwa kabatini na viongozi wataendelea kula
kuku, umaskini upo palepale, ufisadi upo palepale, alichokisema Rais Jakaya
Kikwete ni tahadhari tu, yapo maisha baada ya Katiba,” alisema.
Kinana alibainisha kuwa wamepata
taarifa kuwa baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka upinzani wamedhamiria
kuvuruga vikao vya Bunge ili Katiba mpya isipatikane.
Alisema wajumbe hao wanafanya hivyo
baada ya kuona hawawezi kuingiza matakwa yao, kwakuwa wingi wa wajumbe wa CCM
unawatisha.
Katika hatua nyingine, Kinana alisema
kuwa ziara yake ya siku nne jijini Dar es Salaam ya kukagua miradi imeonyesha
namna CCM ilivyopiga hatua katika utekelezaji wa ilani.
Alisema kuhusiana na suala la maji
alitembelea Ruvu Chini na Juu na kubaini kuwa ifikapo mwaka 2015 asilimia 72 ya
wakazi wa Dar es Salaam watapata maji ingawa Wizara ya Maji inakabiliwa na uhaba
wa fedha.
Akizungumzia masuala ya umeme, Kinana
alisema anayetaka umeme wa bei nafuu ahamie kijijini, kwani gharama za umeme
mijini na vijijini ni tofauti.
Kuhusu mji mpya wa Kigamboni, alisema
kuwa watalizungumza suala hilo ili kulipatia ufumbuzi.
“Hatujawahi kuona mji mpya unajengwa
kwa kuhamisha watu, kama serikali imeamua mbona hawakuuliza wananchi?” alihoji.
Alisema kuwa matatizo ya walimu
yataendelea kutatuliwa ikiwemo serikali kuendelea kujenga nyumba za walimu na
kuwapunguzia makali ya ugumu wa maisha.
Kawa upande wa tatizo la ajira,
aliitaka serikali kutafuta mbinu zisizo za kawaida za kutengeneza ajira nyingi
zaidi ili watu wengi waajiriwe, hasa watu wa chini kwa kutengeneza viwanda
vingi.
“Watu wanaojiajiri wapewe nafasi, si
mgambo kuwasumbua na kuwadai kodi zisizo na msingi, kodi ndogondogo zinasumbua
watu na kupoteza muda,” alisema.
Kuhusiana na tatizo la wizi wa dawa
hospitalini, Kinana alisema kuwa serikali imepata suluhisho ambapo dawa zote
zitaandikwa Serikali ya Tanzania.
Kinana alisema ifike mahali matatizo
yanayoikabili nchi yatatuliwe, kwani wao kazi yao ni kuisimamia serikali na
kuwajibishana pale panapokosewa.
Naye Mbunge wa Ilala, Idd Zungu,
alisema Bunge halikutunga sheria kandamizi kwa bodaboda na wafanyabiashara bali
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) ndio waliotunga kanuni kandamizi.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment