DUH! Kifo. Ndicho unachoweza kusema
kwa Manchester United hii ya msimu huu baada ya kupangiwa Bayern Munich kwenye
robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wawakilishi wengine wa England,
Chelsea nao wanakabiliwa na kibarua kigumu baada ya kupangwa na matajiri wa
Ufaransa, Paris St-Germain.
Klabu hizo za England zimepangwa na
timu ngumu huku mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Man United, wakionekana
kuwa na mtihani mgumu zaidi mbele ya wababe wa Ujerumani, Bayern Munich ambao
msimu huu wamekuwa hatari sana chini ya kocha mpya, Pep Guardiola.
Katika ratiba iliyopangwa jana
Ijumaa, mechi nyingine za hatua hiyo ya robo fainali, Barcelona wataanzia
nyumbani dhidi ya Wahispaniola wenzao, Atletico Madrid katika mechi inayotarajiwa
kuwa ngumu zaidi wakati Real Madrid watachuana na wabaya wao wa msimu uliopita,
Borussia Dortmund kutoka Ujerumani.
Mechi za kwanza zitafanyika Aprili 1
na 2, wakati mechi za marudiano zitafanyika Aprili 8 na 9 mwaka huu, huku
fainali ya michuano hiyo ikitarajia kufanyika Mei 24 katika Uwanja wa Estadio
da Luz mjini Lisbon, Ureno.
Gumzo zaidi ni Man United, ambao
walitinga hatua hiyo kwa staili ya aina yake baada ya kuyapangua matokeo ya
kichapo cha mabao 2-0 mbele ya Olympiakos na kisha kushinda 3-0 uwanjani Old
Trafford. Lakini, mtihani wa sasa unaowakabili ni mgumu katika harakati zao za
kutinga nusu fainali.
Kocha Mkuu wa Man United, David
Moyes, anaamini kikosi chake kitasonga mbele baada ya kuitupa nje Olympiakos,
lakini sasa atamvaa Guardiola ambaye aliitupa nje Arsenal kwenye mechi za
mtoano hatua ya 16 bora.
Bayern Munich, ambao waliitupa nje
Man United kwenye michuano hiyo mwaka 2010 baada ya bao safi la Arjen Robben,
msimu huu ilizibwaga Manchester City, CSKA Moscow na Viktoria Plzen kwenye
kundi lake.
Chelsea inakabiliwa na mtihani mzito
mbele ya Zlatan Ibrahimovic, wakati Barcelona itacheza dhidi ya wapinzani wao
kwenye La Liga, Atletico Madrid, ambao msimu huu wamekuwa hatari zaidi chini ya
kocha wao Diego Simione.
Real Madrid itakuwa na nafasi ya
kulipa kisasi cha kutupwa nje msimu uliopita baada ya kupangwa na Borussia
Dortmund kwenye hatua hiyo ya robo fainali.
Msimu uliopita, Real Madrid iliyokuwa
chini ya Jose Mourinho ilitupwa nje kwa jumla ya mabao 4-3.
Chanzo: Mwanasipoti
No comments:
Post a Comment