KWA UFUPI
- Wakizungumza nje ya Viwanja vya Bunge Freeman Mbowe, Silyvester Kasulumbai na Paul Kimiti, walisema alichowasilisha Jaji Warioba bungeni,siyo maoni yake binafsi.
Na Mussa Juma, Mwananchi
Baadhi ya Wajumbe wa Bunge la Katiba,
wamewataka wenzao kuacha kutoa tuhuma za kumlaumu, Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kutokana na Rasimu ya pili
aliyoiwasilisha bungeni, badala yake wajiandae kutetea misimamo yao.
Wakizungumza nje ya Viwanja vya Bunge
Freeman Mbowe, Silyvester Kasulumbai na Paul Kimiti, walisema alichowasilisha
Jaji Warioba bungeni,siyo maoni yake binafsi.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo
la Hai, alisema ni makosa makubwa kuanza kumlaumu Jaji Warioba, kwani
alichowasilisha ni maoni ya wananchi yaliyokusanywa yana tume nzima ya
Mabadiliko ya Katiba.
“Mzee Warioba pia ametumia taarifa za
tume ambazo iliundwa na Serikali na pia uamuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
hivyo kumtupia lawama yeye ni kumvunjia heshima yake”alisema
Mjumbe Kasulumbai ambaye pia ni
Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, alisema hakubaliani na wanaomlalamikia Jaji
Warioba kwani anaamini ametoa Rasimu ya umma.
Alisema kama angekuwa na uwezo ,
Rasimu ya Jaji Warioba ingepita kama ilivyo kwani inawakilisha maoni ya umma.
“Kama ni mimi ningeipitisha yote kama
ilivyo kama kurekebisha ni mambo madogo sana na nashangaa wanaomtuhumu na
kumpinga na wafuasi wenzake wa CCM,”alisema
Kwa upande wake Kimiti alisema
anamheshimu jaji Warioba na alichofanya ni kuwasilisha bungeni maoni ya
wananchi.
“Binafsi najua mzee Warioba ameeleza
kwa uwazi bila kuficha na haya ni maoni ya wananchi na utafiti wa uliofanywa
naTume hivyo muhimu ni kutafakari na kujiandaa kwa mjadala”alisema.
Tangu Jaji Joseph Warioba kuwasilisha
rasimu bungeni, kumeibuka mjadala mzito miongoni mwa wajumbe wa bunge la Katiba
na baadhi wamekuwa wakimpinga kwa madai
sehemu kubwa ya maoni ni ya Jaji Warioba.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment