RAIS Jakaya Kikwete ameagiza mali
zote za serikali zikiwemo nyumba, zirasimishwe kwenye miliki ya serikali kwa
kutafutiwa, kupatiwa hati na nyaraka muhimu.
Taarifa iliyotolewa juzi jioni na
Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilisema, Rais Kikwete alitoa agizo hilo ili
kuweka rekodi sahihi ya mali za serikali.
Alitoa agizo hilo alipokuwa
akizungumza na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick
Utouh, aliyekwenda Ikulu kuwasilisha Ripoti ya Hesabu za Serikali kwa mwaka wa
fedha ulioishia Juni 30, mwaka jana.
Rais Kikwete aliagiza kazi hiyo ianze
mara moja na ikamilike haraka kwakuwa utaratibu huo utasaidia kuzuia baadhi ya
watu wasiokuwa waaminifu kupora na kuchukua mali hizo, zikiwamo nyumba.
Kikwete alitoa agizo hilo baada ya
kuelezwa na Utouh, kuhusu changamoto mbalimbali walizokumbana nazo wataalamu wa
Ofisi ya CAG katika kufanya ukaguzi wa Hesabu za Serikali Kuu, Serikali za
Mitaa, mashirika ya umma na miradi mbalimbali.
Alibainisha kuwa historia inaonyesha
kuwa, tangu enzi za ukoloni, mali za serikali hazina hati wala nyaraka rasmi za
kuthibitisha umiliki wa serikali, hali iliyotoa mwanya kwa watu wasio waaminifu
kuvamia, kudai na hata kuzipora.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment