Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Esther Bulaya ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) akipiga kura ya siri juzi wakati Bunge hilo lilipokuwa likipitisha utaratibu wa kupiga kura za aina mbili ya siri na wazi. Picha na Salim Shao
Dodoma/Dar. Wakati Bunge Maalumu la
Katiba linatarajia kuanza kujadili Rasimu ya Katiba kesho, baadhi ya wajumbe wa
Bunge hilo wameanza kuondoka bungeni, kupinga mwenendo wa Bunge hilo.
Hatua hiyo ya wabunge hao inakuja
wakati Bunge Maalumu la Katiba juzi lilipitisha azimio la kutumia kura ya siri
na wazi katika kuamua vifungu vya rasimu.
Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la
Katiba, Samia Saluhu alisema baada ya kupitishwa kwa utaratibu wa kupiga kura
za siri na wazi katika Bunge hilo, kuanzia Jumatatu wataanza kujadili sura ya
kwanza na sita ambayo inahusu Muundo wa Muungano.
Katika sura ya kwanza, mambo ambayo
yanatakiwa kujadiliwa ni Jina, Mipaka, Alama, Lugha na Tunu za Taifa wakati
sura ya sita mambo ambayo yanapaswa kujadiliwa ni Muundo wa Muungano.
Lema atangaza kurudi jimboni Arusha
Mjumbe wa Bunge hilo, Godbless Lema
alisema anakusudia kuondoka bungeni, kutokana na kutoridhishwa na maridhiano ya
kupiga kura za siri na wazi katika kufikia uamuzi katika Bunge hilo.
Akizungumza na Mwananchi jana, Lema
alisema hakubaliani na utaratibu uliopitishwa, kwani unalenga kulazimisha kila
jambo ambalo chama tawala kinalitaka lipitishwe.
“Huu utaratibu wa kura kupigwa kwa
wazi na siri katika kitu kimoja, haupo sehemu yoyote duniani. Sasa sisi
kukubali ni kuwasaliti wananchi, kwani hata Dodoma tunaandaa rasimu ya Katiba
ya wananchi wote siyo ya CCM pekee,” alisema Lema.
Alisema pia hakubaliani na utaratibu
wa kujadili rasimu ya Katiba, ambao umetolewa na Kamati ya Uongozi kwa kuanza
na sura ya kwanza na ya sita, kwani vinalenga kufumua Rasimu ya Jaji Warioba.
“Hapa CCM wanataka kulazimisha
Serikali mbili kwa kujadili kwanza vifungu hivi, kama vitapita basi watakuwa na
uwezo wa kubadili rasimu yote kitu ambacho mimi siwezi kukaa kwenye Bunge hili
na kusaliti wananchi waliotoa maoni kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba,” alisema Lema.
Jussa atabiri Bunge kuvunjika.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa
Mjimkongwe, Ismail Jussa, alisema uchaguzi wa vifungu hivyo ambavyo ndivyo
vinabeba Rasimu ya Katiba, vinaashiria kuvunjika kwa Bunge hilo katika hatua za
awali.
“CCM msimamo wao ni Serikali mbili na
sisi ni Serikali tatu na tunaanza kujadili vipengele vinavyobeba Katiba na
hakuna atakayekubali kuachia msimamo wake na hapo ndipo Bunge litakapovunjika,”
alisema.
Kuhusu utaratibu wa kupiga kura za
wazi na siri, Jussa alisema utaratibu huo utaleta mgawanyiko mkubwa, kwa sababu
ya msimamo wa CCM ni kura za wazi na hivyo hakuna mjumbe wa chama hicho
atakayethubutu kupiga kura ya siri.
Mnyika
Naye mjumbe mwengine wa Bunge hilo,
John Mnyika, alisema, CCM ina mpango wa kubadili rasimu kutoka Muungano wa
Serikali tatu kuwa wa Serikali mbili ili kufanikisha msimamo wao na maelekezo
ya Rais kwenye hotuba yake bungeni.
Mnyika alieleza kuwa kwa mazingira
hayo, Ukawa unahitajika kutetea maoni ya wananchi na kwamba CCM wakiendelea na
njama zao wakati wa kujadili sura ya kwanza na ya sita, itawalazimu kurudi kwa
wananchi ambao ndiyo wenye nchi.
“Hatua ya kurejea kwa wananchi
inatarajiwa kuchukuliwa kabla ya kuendelea na sura zingine mbili za Rasimu ya
Pili ya Katiba,” alisema Mnyika.
Mnyika alisema mpango huu ulianza kwa
wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka CCM wakati wa kujadili rasimu ya kanuni
waliwasilisha majedwali ya marekebisho kutaka ibara zipangwe mbili mbili
zinazofanana.
Katibu wa Bunge
Hata hivyo, Katibu wa Bunge Yahya
Khamis Hamad akizungumzia kuondoka kwa baadhi ya wabunge alisema, suala hilo
amelipata jana kupitia Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge lakini si msimamo wa
kundi.
“Taarifa hii tulipata kwenye kamati,
lakini tukaulizana kama kuna kundi linataka kuondoka, ikabainika hakuna kundi.”
Kuhusu uamuzi wa kuanza kujadili sura
ya rasimu ya kwanza na sita alisema tayari yalifikiwa na Kamati ya Uongozi na
kwamba kwa mujibu wa kanuni ya 58 kifungu kidogo cha tatu, Kamati ya Uongozi
ndiyo yenye jukumu la kupanga utaratibu wa kujadiliwa rasimu.
Kuhusu CCM kuwa na rasimu yake
Akizungumzia taarifa kuwa CCM ina
rasimu yake ambayo ndiyo wanataka ijadiliwe alisema hakuna suala hilo.
“Mimi binafsi sijalisikia hilo na
sitegemei kuwapo, kwani wajumbe watajadili rasimu iliyo mbele yao ambayo ni ya
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Hamad.
Wasomi
Wasomi nchini wamesema mfumo wa
kupiga kura ya wazi na siri uliopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba,
hautapunguza nguvu ya mijadala katika Bunge hilo katika vipengele muhimu ikiwa
ni pamoja na aina ya muundo wa Serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
jana, wasomi hao walisema kuwa badala yake mfumo huo utawalazimisha baadhi ya
wajumbe wasiokubaliana na misimamo ya vyama vyao kupiga aina ya kura
wasiyoitaka.
Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu
cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho alisema mjadala mkali unatarajiwa
kuendelea bungeni hasa katika hoja ya aina ya muundo wa Serikali, kwa kuwa
hotuba ya Rais Jakaya Kikwete iliashiria kutotaka muundo wa Serikali tatu.
Profesa Shumbosho alisema kuwa kuna
baadhi ya wajumbe wa CCM hawakubaliani na muundo wa Serikali mbili, lakini
watalazimika kupiga kura ya wazi ili kukiridhisha chama chao.
“Kuna watu hawana ujasiri. Ndani ya
CCM wapo wanaopenda Serikali tatu lakini wanaogopa,” alisema Profesa Shumbusho.
Pia, alisema kuwa kwa namna hali
inayoonekana kuendelea bungeni, kuna dalili kuwa maoni ya rasimu ya CCM kuhusu
Katiba ndiyo yatakayopita na hivyo kurudisha mambo mengi yaliyopo katika Katiba
ya sasa.
Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala alisema kuwa upigaji kura wa wazi
au siri hautazuia wajumbe kuendelea na misimamo yao na kwamba badala yake
mjadala utakuwa mkali zaidi kuliko ilivyokuwa awali.
Alisema ingawa yapo baadhi ya mambo
ambayo wajumbe wanaweza kukubaliana bila kupiga kura, suala la Muungano
litakuwa na mvutano kwa kuwa tayari hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Katiba,
Jaji Joseph Warioba na Rais Kikwete bungeni, zimeshaleta ‘msuguano’.
“Mjadala utakuwa mkali, suala lenyewe
tu limeanza kuwa kali tangu mwanzo. Warioba alieleza Serikali tatu, Rais
Kikwete akapinga,” alisema Profesa Mpangala.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria,
Hamad Salim alisema suala la kupiga kura ya siri au wazi limechukua muda mrefu
kujadiliwa bila sababu za msingi.
Akifafanua, Salim alisema kuwa
wanaotaka kura ya wazi wanajenga hoja kuwa wanataka masuala yote yawe wazi kwa
wananchi, lakini wanashindwa kusema ni lini walipewa maoni hayo na wananchi.
“Sikubaliani na kura ya wazi,
hawakutumwa na wananchi, walitakiwa kuridi kwao na kuwauliza aina gani ya kura
wanataka,” alisema Salim na kuongeza:
“Kwa muda mrefu upigaji kura ulikuwa
wa siri, sasa imekuwaje leo wanataka kura ya wazi?”
Sendeka
Mjumbe wa Bunge hilo, Christopha Ole
Sendeka alisema matokeo ya kura za kupitisha kanuni ya 37 na 38 ya upigaji kura
yamewashangaza Ukawa, lakini muhimu kwao ni kukaa bungeni na kujenga hoja.
“Matokeo ya jana (juzi) yamewakatisha
tamaa kwa ushindi wa idadi nzuri ya kura, walidhani CCM haina theluthi mbili,
lakini licha ya wabunge wengi hatohudhuria tumeshinda,” alisema Sendeka.
Alisema wingi wa CCM siyo ndani ya
Bunge tu, kwani hata nje wengi wanakiunga mkono chama hicho.
“Vizuri wangekaa tu kwani CCM inaweza
kupitisha mambo kwa kura nyingi zaidi, lakini wakiwepo tunaweza kufikia
maridhiano katika baadhi ya mambo,” alisema Sendeka.
Umoja wabunge Wanawake
Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa
Wanawake Wabunge, (TWP), Suzan Lyimo alisema utaratibu wa kura za wazi na siri
utaleta vurugu na utekelezaji wake ni mgumu.
“Utaratibu huu ni mgumu kutekelezeka
sasa sijui wanaopiga kura za wazi watakaa upande wao na wale wa siri upande
wao, lakini ni mgumu kutekelezeka na hakuna nchi ambayo umeshawahi kutumika,”
alisema.
Akizungumza na vyombo vya habari kwa
niaba ya wabunge wanawake kutoka vyama vya upinzani, Suzan Lyimo alisema hotuba
ya Rais Jakaya Kikwete imeleta madhara makubwa kwa wananchi hasa wale ambao
hawana itakadi za vyama.
“Hotuba hiyo imeleta mpasuko mkubwa
miongoni mwa Watanzania..., sisi kama wajumbe wa Bunge hili tunawahakikishia
wananchi kwamba tutajadili Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayotokana
na maoni ya wananchi,” alisema.
Kwa upande wake, Sabrina Sungura
alisema mchakato huo wa Katiba unaweza usifike mwisho na kwamba mtu wa kwanza
wa kulaumiwa ni Rais Kikwete ambaye alitoa hotuba ya kuwagawa wabunge.
“Tulipaswa kuambiwa kuwa Rais
anatumia nafasi yake kama sehemu ya Bunge kuleta maoni yake na si kulizindua
Bunge kama tulivyoambiwa katika ratiba,” alisema.
Naye Moza Abeid ametaka kurekebishwa
upungufu uliojitokeza katika mchakato wa Katiba ili wananchi waweze kupata
Katiba waitakayo.
Mussa Juma,Sharon Sauwa na Edith
Majura, Goodluck Eliona. Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment