WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu, amemfukuza kazi Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii (TTB), Dk. Aloyce Nzuki,
kwa madai ya kutokuwa na imani naye katika utendaji kazi wake.
Akitangaza hatua hiyo jana mbele ya
waandishi wa habari, Waziri Nyalandu alisema kabla ya kuchukua uamuzi huo,
wajumbe wa Bodi ya Utalii walimwandikia barua ya kutokuwa na imani na Nzuki.
Waziri huyo ambaye tangu awe waziri
kamili kuongoza wizara hiyo amekuwa katika harakati za kusafisha watendaji
wabovu na wabadhirifu, alisema ameamua kuchukua hatua hiyo haraka ili kunusuru
sekta ya utalii nchini ambayo imekuwa ikisuasua kwa muda mrefu.
“Baada ya kuletewa barua ya
malalamiko hayo, nilijipa muda kufanya uchunguzi na kujiridhisha kwamba
mkurugenzi huyo ana matatizo, ndipo nikachukua uamuzi huo,” alisema Nyalandu.
Waziri Nyalandu ameagiza kutangazwa
mara moja kwa nafasi hiyo, ambapo Mtanzania yeyote mwenye sifa bila kujali yupo
ndani au nje ya nchi, anaruhusiwa kutuma maombi ndani ya siku 21, kuanzia leo.
Aidha, alisema uteuzi wa
mkurugenzi huyo utafanywa na taasisi
zenye utaalamu katika masuala ya utalii ambapo watatakiwa kupendekeza majina
tisa kabla ya yeye kuyafikisha kwa Rais Jaka Kikwete kwa hatua zaidi za uteuzi.
Wakati mchakato wa kumpata mkurugezi
mpya ukiendelea, Waziri Nyalandu alisema katika kipindi kilichobaki, Mkurugenzi
wa Masoko, Devota Mdachi, atakaimu nafasi hiyo.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii,
Charles Sanga, alisema kabla ya uamuzi huo, tayari wajumbe walikuwa wameridhia
kujiuzulu nafasi zao kutokana na mkurugenzi huyo kwa muda mrefu kuyumbisha kazi
za kitalii.
Hata hivyo pamoja na matamko hayo,
Waziri Nyalandu alikataa kuulizwa swali lolote na waandishi wa habari ambao
walibaki eneo hilo wakiwa na maswali mengi, ikiwemo kama ana mamlaka ya kufanya
hivyo, ukizingatia kwamba mwenye mamlaka
ya uteuzi huo ni rais.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment