Mwandishi wa gazeti la Daily Mail la Uingereza, Martin Fletcher akiwa katika
chumba cha kuhifadhi meno ya tembo katika Wizara ya Maliasili na Utalii jijini
Dar es Salaam ambako zaidi ya meno 34,000 yamehifadhiwa. Picha ya Daily Mail.
Mwandishi Wetu:
Dar es Salaam. Licha ya Rais Jakaya
Kikwete kutoa ahadi ya kuteketeza maelfu ya meno ya tembo yaliyo kwenye ghala
la Serikali, imeelezwa kuwa uwezekano huo ni mdogo.
Mwandishi wa gazeti la Daily Mail la
Uingereza, Martin Fletcher ameeleza kushtushwa na hali ya ulinzi kwenye ghala
hilo lililosheheni meno 34,000 ya tembo ambayo kwa biashara ya magendo nchini
China yanagharimu Pauni 150 milioni za Kiingereza (Sh403.5 bilioni)
Fletcher, ambaye aliandika habari ya
kuhusika kwa wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa wa Tanzania katika biashara
haramu ya meno hayo kiasi cha kuifanya nchi kuwa muuzaji mkuu wa nyara hizo,
aliandika hayo kwenye taarifa kuhusu ziara yake nchini iliyochapishwa na gazeti
hilo jana.
Habari ya awali ilitikisa ulimwengu
ambao unapambana kulinda viumbe walio hatarini kutoweka ikiwatuhumu wanasiasa
na wafanyabiashara wakubwa nchini kuhusika, huku Serikali ikishindwa
kuwadhibiti.
Habari hiyo iliifanya Serikali ya
Tanzania kufungua milango kwa vyombo vya habari vya nje kuja nchini kupata
habari sahihi kuhusu tatizo hilo, akiwamo Fletcher wa Daily Mail.
Katika ziara yake, Fletcher alipata
nafasi ya kutembelea ghala la nyara hizo, kuzungumza na maofisa wanyama pori
pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
“Nyalandu pia aliweka bayana kuwa
uteketezaji wa shehena ya Tanzania ni kitu ambacho kiko mbali na uhalisia,
licha ya ahadi ya Kikwete jijini London,” Fletcher alimkariri Nyalandu kwenye
habari hiyo ambayo imeambatana na picha alizozielezea kuwa za kushtua za ghala
hilo, lenye idadi kubwa ya meno ya tembo kuliko maghala yote duniani.
“Alisema Rais alikuwa na nia ya
kuteketeza (shehena hiyo), lakini Tanzania ilitaka ilipwe takriban Pauni 30
milioni za Uingereza kutoka Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya Mfuko wa Hifadhi
ya Tembo.”
Hata hivyo mwandishi huyo anaripoti
kuwa; “Wahisani ambao wangeweza kutoa fedha hizo, walikejeli kiwango hicho
wakisema hakina uhalisia.”
Alipoulizwa kuhusu kauli hiyo jana,
Nyalandu alisema baadhi ya mambo kwenye habari ya mwandishi huyo yamekuzwa,
lakini alisema uamuzi wa kuteketeza nyara hizo haujafikiwa.
Alisema Serikali ilichofanya hadi
sasa ni kupiga marufuku biashara zote za meno ya tembo, hivyo haitauza yaliyopo
na haitaomba kibali tena cha kufanya biashara hiyo na kwamba kinachoendelea
sasa ni mazungumzo ya namna ya kushughulika na shehena iliyopo.
“Meno mengine yaliyopo ni ya
kihistoria. Ni marefu kuliko mengine na tembo wa aina hii hawapo tena, hivyo
kuwa nayo pia ni kitu kizuri. Haya meno ni mali ya Watanzania wote, uamuzi wa
kuyateketeza lazima uchukuliwe kwa busara,” alisema.
Kwa mujibu wa Fletcher meno mengine
yana urefu wa futi 7, uzito wa tani 125 na moja linaweza kubebwa na watu
kuanzia watatu, huku jino fupi likiwa na uzito wa kilo 0.4500 na kwa mujibu wa
jangili aliyekiri kuua tembo 30 kwa siku, jino hilo dogo liling’olewa kutoka
kwa tembo mtoto.
Mara tatu katika kipindi cha miaka
minane, Tanzania imeomba bila mafanikio kibali cha kuuza shehena yake kutoka
katika nchi 180 zilizosaini makubaliano ya kudhibiti biashara ya kimataifa ya
viumbe walio hatarini kutoweka, Cites, licha ya ushahidi mkubwa kuwa kitendo
cha kuuza mara moja tu, kitazidisha tamaa ya China kupata meno hayo.
Akizungumzia ziara yake nchini,
mwandishi huyo anaelezea udhaifu katika ulinzi wa ghala hilo lililo nyuma ya
jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dar es Salaam.
“Ghala hilo niligundua siyo kama
ngome (yenye ulinzi mkali). Lina milango ya chuma ya kusukuma ikiwa na kufuli
nzito tano ambazo funguo zake zimegawanywa kwa maboharia wawili, lakini milango
ilifunguliwa yote nilipofika,” makala hiyo inaeleza. “Kila jino limewekwa alama
na namba na ghala ina kamera za ulinzi wa ndani, lakini sikuona mlinzi mwenye
silaha nje.”
Mwandishi huyo anaeleza kuwa habari
yake ya kwanza iliyohoji kama mtoto wa Mfalme wa Wales na Waziri Mkuu wanaweza kushikana
mkono na Rais Kikwete wakati alipotembelea Uingereza, ilizua kizaazaaa kiasi
cha Rais Kikwete kuitisha kikao na maofisa waandamizi wa Maliasili na kutoa
maelekezo kuwa wafanye kazi.
Mwandishi huyo alitembelea maghala ya
meno ya tembo, Hifadhi ya Selous ambayo mwaka 2006 ilikuwa na tembo 70,000
lakini hadi sasa wamesalia 13,000 tu. Baadhi ya meno yalichukuliwa kutoka tembo
waliokufa na mengi kukamatwa kutoka kwa majangili na hayawezi kuuzwa kwa sababu
ya biashara hiyo kuzuiwa duniani.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment