Dodoma. Mwenyekiti Mteule wa Bunge
Maalumu la Katiba, Samuel Sitta amezungumzia uwezekano wa kutumia kura ya siri
katika kuamua ibara nyeti katika Rasimu ya Katiba.
Sitta aliyechaguliwa juzi kushika
wadhifa huo, alisema atashirikiana na kamati ya uongozi itakayoundwa ya
wenyeviti wa Kamati 15 za Bunge hilo na kamati ya ushauriano kupata jawabu la
suala hilo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu
nyumbani kwake mjini Dodoma juzi, Sitta alisema: “Unajua kuna baadhi ya vifungu
na ibara za Rasimu ya Katiba ni vizuri vipigiwe kura ya wazi na vingine ambavyo
ni nyeti zaidi vipigiwe kura ya siri.”
Alisema si vizuri vifungu vyote
vipigiwe kura sawa, yaani si lazima zote ziwe za siri au ziwe za wazi.
Alitoa mfano wa ibara inayosema
kutakuwa na Mahakama Kuu ya Tanzania na kusema: “Hatuwezi kushindana katika
suala la kuwapo kwa Mahakama na ni wazi kuwa jambo hilo mnaweza kupiga kura ya
wazi. Nasema hivyo kwa sababu Katiba yoyote lazima ionyeshe mihimili yote
ambayo ni Bunge, Serikali na Mahakama.”
Sitta ambaye pia ni Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki alishinda kiti hicho katika uchaguzi uliofanyika
juzi kwa kura 487 kati ya 563 (sawa na asilimia 85).
Mbunge huyo wa Urambo Mashariki
ambaye kaulimbiu yake ni ‘kasi na viwango’, alisema vifungu na ibara za Rasimu
ya Katiba vinavyoweka misingi ya Katiba, ni vizuri vikapigiwa kura ya siri.
“Unajua tuna viongozi wa dini na
halitakuwa jambo la busara kama tukizijua hisia zao. Kama wewe uko karibu na
imamu au askofu halafu anapiga kura ya wazi ya kutaka Serikali tatu wakati wewe
muumini unataka Serikali mbili ni wazi kuwa jambo hilo linaweza kuleta hisia
tofauti na kuwanyima watu haki na uhuru wa kuamua,” alisema Sitta.
Alitoa mfano wa Sura ya Sita ya
Rasimu ya Katiba inayozungumzia Serikali na muundo wa madaraka katika Jamhuri
ya Muungano na kufafanua kuwa katika sura hiyo atapendekeza ipigiwe kura ya
siri.
Kuhusu suala hilo la muundo wa
Serikali alisema: “Kikubwa ni wajumbe kujenga hoja, hatuwezi kwenda na misimamo
isiyobadilika kwa sababu tunataka maridhiano. Nitatenda haki na nitatoa muda
mrefu zaidi kwa wajumbe kujadili sura ya kwanza na ya sita ambazo zina uzito
mkubwa kuliko sura nyingine ambazo ni za maelezo tu. Mfano suala la haki za
binadamu ambazo wote tunakubaliana nazo.”
Alisema wakati wa kujadili muundo wa
Serikali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukifika, ataishauri kamati ya
uongozi, kutenga muda wa ziada katika suala hilo na mengine yenye utata.
Mwenyekiti huyo alisema suala la
upigaji kura linatakiwa kuamuliwa kwa busara na atatumia hekima zake na za
wajumbe wa Bunge hilo, kutatua mgogoro wa kura ya siri au ya wazi.
Wakati wa kujadili rasimu ya kanuni
za Bunge hilo, kulizuka mvutano mkali katika vifungu vya 37 na 38
vinavyozungumzia aina ya kura itakayopigwa wakati wa kufanya uamuzi na
kulazimika kuviweka kando. CCM kimekuwa kikinadi kura ya wazi kikisema ni ya
haki huku wapinzani wakitaka kura ya siri.
Hata hivyo, kamati ya muda iliyoandaa
kanuni za Bunge hilo, ilipendekeza kuwa Bunge Maalumu ndilo litakaloamua aina
ya kura itakayopigwa.
Akizungumzia suala hilo Sitta
alisema: “Pamoja na kuwapo kwa hali hiyo, lazima ifikie wakati tuamue. Hatuwezi
kuwa na kanuni ambazo hazielekezi namna ya kupiga kura kwa sababu upigaji wa
kura unaweza kuanza kufanyika wiki ya kwanza tu baada ya kuanza kujadili Rasimu
ya Katiba.”
Samia Makamu Mwenyekiti
Wakati huohuo, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan jana alichaguliwa kuwa Makamu
Mwenyekiti wa Bunge hilo baada ya kumshinda mpinzani wake, Amina Abdallah
Amour.
Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa
Uchaguzi, Dk Thomas Kashililah alisema kati ya kura 523 zilizopigwa, Suluhu
alipata kura 390 sawa na asilimia 74.6, Amina kura 126 sawa na asilimia 24.1.
Kura saba ziliharibika.
Kukamilika kwa uchaguzi huo
kunafungua milango kwa Yahya Hamad Hamis kuapishwa kuwa Katibu wa Bunge la
Katika na Dk Thomas Kashililah kuwa Naibu Katibu kwa mujibu wa sheria.
Makatibu hao wataapishwa leo saa nne
asubuhi na Rais Jakaya Kikwete katika Ikulu ndogo ya Dodoma. Baada ya
kuapishwa, Katibu atawaapisha Sitta na Samia katika Ukumbi wa Bunge kuanzia saa
10 jioni leo.
Awali wakati wakijieleza Amina alizua
gumzo baada ya kueleza kuwa licha ya kuwa na watoto watano, ameachika na kwa
sasa hana mume.
“Mimi ni mama wa watoto watano, nina
shahada ya uzamili ya masuala ya fedha, nina stashahada ya sheria na nimefanya
kazi katika Benki ya Biashara kwa miaka 23 ila kwa bahati mbaya nimeachika,”
alisema na kusababisha wajumbe kuangua kicheko.
Baada ya kuchaguliwa, Suluhu alisema:
“Nitafanya naye (Sitta) kazi kwa ushirikiano na uadilifu mkubwa. Pia
ninawaahidi wajumbe wote kuwa nitawapa ushirikiano.”
Mbowe amuonya Sitta
Wakati huohuo; Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe amemtumia salamu za pongezi Sitta huku akimtaka kuachana na
masilahi ya chama chake.
“Ningependa kutuma salamu kwa Samuel
Sitta ambaye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, nataka
aelewe kuwa alichokabidhiwa ni majukumu si cheo,” alisema na kuongeza:
“Mamilioni ya Watanzania watakuwa
wanamfuatilia na kumtazama kwa makini mno... maana wananchi kwa sasa wanajua
mchakato wa Katiba Mpya umebeba matumaini ya Taifa lao kwa miaka 50 hadi 100
ijayo.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment