Mahakama yaruhusu mkenya afikishwe
Hague
Mahakama kuu nchini Kenya imepinga
agizo la kutokamatwa kwa mwandishi Walter Baraza baada ya
wakili wake Kibe Mungai kushindwa
kufika mahakamani ili kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Hatua hiyo inamaanisha kwamba waziri
wa usalama nchini Kenya Joseph Ole Lenku anaweza kuomba agizo la
kukamatwa kwa mwandishi huyo kabla ya
kuwasilishwa katika mahakama ya ICC anakotakikana.
Walter Baraza anatakikana na mahakama
hiyo kwa madai ya kuingilia ushahidi katika kesi inayomkabili makamu wa rais
wa kenya William Ruto.
Uamuzi wa Jaji wa Mahakama Kuu
Richard Mwongo ni pigo kubwa kwa Mwandishi wa habari Walter Barasa, ambaye
alikuwa aking'ang'ana kuhakikisha
kuwa hakamatwi na kusafirishwa hadi Hague kushtakiwa kwa kosa la kuwaingilia
mashahidi waliokuwa wameorodheshwa na
kiongozi wa Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.
Mwaka uliopita Kiongozi wa mashtaka
katika The Hague, Fatou Bensouda, alitoa ombi ambalo lilikubaliwa na
kuwasilishwa nchini Kenya ambapo
ilitakiwa Waziri wa Maswala ya Usalama Nchini Kenya Joseph Ole Lenku, amkamate
na kumfikishakatika The Hague.
Katika agizo hilo ilidaiwa kuwa Bwana
Barasa alitumia pesa kuwahonga mashahidi waliotarajiwa kutoa ushahidi dhidi
ya Naibu Rais wa Kenya, William Ruto
na mtangazaji Joshua arap Sang.
Wakenya hao wawili wameshtakiwa kuwa
walichangia pakubwa katika kuchochea ghasia za baada ya Uchaguzi wa
mwaka 2007 na 8, ambapo zaidi ya watu
1,300 waliuawa katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baada ya
upande wa upinzani kupinga matokeo ya
uchaguzi.
Tangu kutangazwa kuwa akamatwe Baraza
alikanusha kuwa alihusika katika njama hiyo na akadai kwamba Mahakama
ya Kimataifa ilikuwa ikitaka kumgandamiza
tu kwa sababu yeye alikataa kujitolea kutoa ushahidi dhidi ya Bwana Ruto
na mwenzake Bwana Sang.
Awali Jaji Mwongo alikuwa ametoa amri
kuwa Baraza akamatwe na kupelekwa Hague lakini Wakili wa Bwana Baraza
Kibe Mungai, akaomba utekelezaji wa
uamuzi huo uahirishwe ili yeye, Bwana Kibe ajitokeze mahakamani kutoa
ushahidi kwa nini Bwana Baraza
asikamatwe.
Wakili Kibe alitarajiwa kuwasilisha
sababu zake jana lakini hakuwepo, jambo ambalo lilimlazimisha jaji kurejesha
amri
ya awali kuwa Baraza akamatwe.
Tangu mashtaka kuwasilishwa dhidi ya
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, naibu wake William Ruto na Bwana Sang katika
Mahakama ya Kimataifa mashahidi wengi
wamejiondoa kutoa ushahidi wakidai kuwa wanatishwa ingawa Bi Bensouda
kwa upande wake anasema wengi wao
wanahongwa na wandani wa washtakiwa.
Chanzo: BBC Swahili
No comments:
Post a Comment