Polisi wa Uganda wameimarisha usalama
baada ya kupokea habari za kijasusi kwamba wanamgambo wa Al-Shabaab wanapanga
kuishambulia malori yanayosafirisha mafuta.
Al-Shabaab mara kwa mara imekuwa
ikionya kwamba itaishambulia Uganda kwa sababu ina majeshi yake nchini Somalia
kulinda usalama.
Wanamgambo wa Al-shabaab
waliishambulia Uganda mwaka wa 2010. Takriban watu 76 waliokuwa wamekusanyika
kwenye uwanja wa Raga wa Kyadondo kutizama fainali za Kombe la Dunia
waliyapoteza maisha yao baada ya mabomu mawili kulipuka.
Tokea wakati huo, kundi la Al-Shabaab
limekuwa likitishia kuzishambulia nchi zote ambazo zimeyatuma majeshi yake
nchini Somalia kulinda usalama chini ya mwavuli wa Umoja wa Afrika. Uganda ndio
iliyokuwa nchi ya kwanza kutuma majeshi mwaka wa 2007.
Baada ya kupokea taarifa kwamba
huenda Al-Shabaab ikayashambulia magari yanayosafirisha mafuta, polisi imeanza
kuyashindikiza magari ya mafuta yanayoingia nchini Uganda. Wanayazindikisha
kutoka kwenye mipaka ya Kenya na Uganda ya Busia na Malaba.
Siku ya Jumanne, polisi ilifanya
kikao na wafanyibiashara wanaosafirisha mafuta kuwaelezea hatua ambazo
wamezichukua. Kila mfanyibiashara anafaa sasa kuipa polisi jina la dereva wake
na nambari ya gari anayoiendesha. Ikizingatiwa kuwa wanamgambo huwa wajanja na
wanaweza kuwatuma watu wao kuomba kazi kama madereva wa magari ya mafuta,
polisi itafanyaje kuhakikisha kwamba madereva wanaowasajili sio magaidi.
Waganda wamekuwa na uoga kwamba bei
ya mafuta huenda ikapanda ikiwa gharama ya polisi ya kuyazindikisha magari ya mafuta italipwa na wafanyibiashara
wanayoyamiliki magari haya. Polisi imesema wao ndio watakaogharamika kwa hivyo
bei ya mafuta itabakie ilivyo sasa.
Polisi inasema itaendelea
kuyashindikiza magari ya mafuta hadi pale watakapopata taarifa kwamba hamna
tisho tena la kushambuliwa hata kama ni miaka mitatu kutoka leo.
Chanzo: VOA Swahili
No comments:
Post a Comment