Thursday, March 20, 2014

Kizungumkuti cha amani Sudan Kusini


Makamu wa Rais wa zamani wa Sudan Kusini Riek Machar analaumiwa kwa kupanga njama ya mapinduzi

Mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Sudan Kusini na waasi wanaoongozwa na aliyekuwa naibu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar yanatarajiwa kuanza tena leo mjini Addis Ababa Ethiopia.
Mazungumzo hayo yaliahirishwa mapema mwezi huu baada ya mazungumzo ya hapo awali kukwama.

Taarifa zinazohusiana
Sudan Kusini
Aidha, pande zote mbili zimetuhumiwa kwa kukiuka mkataba wa kusitisha mapigano uliotiwa saini mwezi Januari.
Mnamo siku ya Jumatano, mataifa ya magharbi yanayohusika na mgogoro huu wa Sudan Kusini katika kuutafutia suluhu la kudumu, walitishia kuwawekea vikwazo wahusika wakuu kwenye mgogoro huo ikiwa hawatausuluhisha.
Mazungumzo ya kuzipatanisha pande hizo hayajapiga hatua kwa wiki mbili zilizopita huku wahusika wakilaumiana.

Serikali na waasi wanalaumiana kwa kuyumbisha mazungumzo ya amani
Nao mkataba wa amani uliotiwa saini kusitisha vita pia haujafanikiwa katika kumaliza mgogoro huo.
Baadhi ya wanadiplomasia kutoka nchi za magharibi, wamehoji ikiwa viongozi wamejitolea kikweli kutafuta muafaka huku kila mhusika akimlaumu mwenzake kwa kizungumkuti kilichoko.

Mazungumzo hayo yanaanza tena baada ya wiki mbili ya kusitishwa kwake, ingawa wajumbe wamesema haijulikani ikiwa pande hizo mbili zitakuwepo.
Maswala makuu yanayoyumbisha mazungumzo hayo, ni matakwa ya waasi wa Sudan Kusni kwamba wafungwa wanne wa kisiasa ambao bado wanazuiliwa, sharti waachiwe huru.

Wanne hao walilaumiwa kwa kupanga njama ya mapinduzi dhidi ya serikali ya Rais Salva Kiir wakiongozwa na aliyekuwa makamu wa Rais Riek Machar
Chanzo: BBC Swahili

UN yaripoti uovu Sudan Kusini
Umoja wa Mataifa umesema mapigano yenye sura ya kikabila yaliyozuka katikati ya Desemba mwaka jana Sudan Kusini yamesababisha mauaji ya kikatili na unyanyasaji dhidi ya maelfu ya raia na kampeni ya kukashifu umoja huo.


Mkuu wa shughuli za kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa Herve Ladsous ameliambia baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa pamoja na makubaliano ya kusitisha mapigano ya Januari 23, lakini jeshi tiifu kwa rais Salva Kiir na wapiganaji waasi wanaoongozwa na makamo wa rais wa zamani alieondolewa madarakani Riek Machar wameendelea na harakati zao za kijeshi na kuyapa kisogo mazungumzo muhimu ya kisiasa kwa lengo la kupatikana suluhisho la mgogoro huo.

Kuzuka mapigano
Südsudan Rebellen 10.02.2014
Wapiganaji waasi katika baadhi ya miji
Mapigano Sudan Kusini yalizuka Desemba 15 miongoni mwa kikosi cha jeshi cha ulinzi wa rais mjini Juba, ambapo kwa kasi yakasambaa katika maeneo tofauti ya nchi hiyo na kuchukua sura ya mwelekeo wa mapigano ya kikabila kati ya kabila la Dinka, lenye kumuunga mkono rais Kiir na Nuer lenye utiii kwa Machar.

Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa, Ladsous amesema mgawiko wa kisiasa umesababisha mgogoro kwa hivi sasa kwa kuathiri maisha ya kila mtu mmoja mmoja pamoja na utendaji wa serikali ya Sudan Kusini na taifa lenyewe kwa ujumla. Amesema ripoti ya uchunguzi ya awali inaonesha mauwaji pamoja na ukiukwaji mbaya sana haki za binaadamu umetekelezwa na pande zote zinazohasimiana katika mgogoro huo.
Onyo la kuendelea mapigano
Konflikt im Südsudan Flüchtlinge 17.01.2014
Wakimbizi wakihangaikia maji safi

Aidha afisa huyo ameonya kwamba kuendelea kwa muda mrefu kwa mapigano hayo kunaweza kutoa nafasi ya majeshi ya kikanda kuingia zaidi katika taifa hilo. Ladsous vilevile ameonya kuwa hakutakuwa na hatua yoyote ya maana itakayofikiwa na mataifa yalio katika Jumuiya ya maendeleo mashariki na pembe ya Afrika- IGAD katika utatuzi wa mgogoro huo mpaka hitaji muhimu la upinzani la kutaka kuachiwa huru kwa wafungwa wanne walisalia gerezani litekelezwe. Watuhumiwa hao walipandishwa kizimbani Machi 11 kwa tuhuma za uhaini.

Ladsous amelitaka baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani kampeni yeyote dhidi ya operesheni ya ulinzi wa amani nchini Sudan Kusini ambao inatoa hifadhi kwa wakimbizi 75,000 kati ya watu 800,000 waliopoteza makazi yao kutokana na vurugu hizo. Na amemtaka rais Kiir kulaani na kuwalekeza maafisa wa serikali na chama chake kiachana na vitendo hivyo mara moja. Amesema vitendo hivyo dhidi ya ujumbe wa kusimamia amani Sudan kusini , vinaweza pia kuhatarisha maisha ya watoa huduma.

Baadae akizungumza na waandishi wa habari balozi wa Luxembourg katika Umoja wa Mataifa Sylive Lucas hali hiyo haikubaliki na amekubali kutuma ujumbe mkali nchini Sudan Kusini. Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amependekeza kwa baraza hilo la usalama kuongzea uwezo UNMIS katika kiwango kilichokubaliwa Desemba mwaka jana kufikia wanajeshi 12,500, shabaha ikiwa kuwalinda raia, kufanikisha kufikisha misaada ya kiutu na kuchunga vitendo vya ukiukaji wa haki za binaadamu.
Mwandishi: Sudi Mnette APE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

DW.DE

No comments: