Dodoma. Rais Jakaya Kikwete kesho
ataambatana na ujumbe mzito wa marais wastaafu wa pande zote za Muungano, wake
wa waasisi wa taifa na mawaziri wakuu wastaafu atakapokwenda kuzindua Bunge
Maalumu la Katiba.
Hatua ya Rais kuambatana na ujumbe
huo imepongezwa na viongozi wa vyama vikuu vya upinzani nchini, Mwenyekiti wa
CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na mwenzake wa Chadema, Freeman Mbowe.
Mbali na viongozi hao, Rais Kikwete
pia ataambatana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Makamu wa Rais, Dk
Mohamed Gharib Bilal na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif
Hamad.
Wanaotarajiwa kuwamo katika msafara
huo ni Rais wa pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa tatu, Benjamin
Mkapa na marais wastaafu wa Zanzibar, Dk Salmin Amour na Amani Abeid Karume,
Mama Maria Nyerere na Mama Fatma Karume.
Miongoni mwa mawaziri wakuu wastaafu
wanaotarajiwa kuwamo ni pamoja na Jaji Joseph Warioba, ambaye juzi aliwasilisha
bungeni hapo Rasimu ya Katiba kwa kutoa hotuba iliyoliteka Bunge kwa jinsi
alivyofafanua mambo mengi yenye utata kuhusu muundo wa Muungano.
Mawaziri wakuu wengine ni Cleopa
Msuya, John Malecela, Dk Salim Ahmed Salim, Frederick Sumaye pamoja na Edward
Lowassa na Mizengo Pinda ambao ni wajumbe wa bunge hilo.
Wengine walioalikwa ni mabalozi wa
nchi mbalimbali, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, viongozi wa dini, vyama
vya wafanyakazi, vyama vya siasa, wafugaji, wakulima, wavuvi na wawakilishi wa
sekta binafsi.
Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba,
Yahaya Khamis Hamad aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Rais Kikwete
atahutubia Bunge hilo kwa mujibu wa Kanuni ya 75 (1).
Rais Kikwete atapokewa katika Viwanja
vya Bunge na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta na baadaye
kukagua gwaride maalumu kabla ya kuhutubia Bunge kuanzia saa 10:00 jioni.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa
jana, baada ya Rais kuhutubia saa 11:35 jioni, aliyekuwa mwenyekiti wa muda wa
bunge hilo, Pandu Ameir Kificho atatoa neno la shukurani kabla ya Rais kupiga
picha za kumbukumbu na wajumbe wa Bunge hilo.
Suala la hotuba ya Rais Kikwete
limekuwa sehemu ya mjadala katika Bunge hilo kutokana na baadhi ya wajumbe
kuhoji sababu za Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu kabla ya Rais kuzindua Bunge
kwa mujibu wa kanuni.
Mjadala huo uliwafanya baadhi ya
wajumbe kumzuia Jaji Warioba Jumatatu iliyopita kuwasilisha rasimu hiyo kama
ilivyokuwa imepangwa hadi kilipofanyika kikao cha maridhiano siku hiyohiyo
usiku na kufikia mwafaka kwamba Mwenyekiti huyo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
awasilishe Rasimu juzi na Rais ahutubie kesho.
Lipumba, Mbowe na Mtatiro
Akizungumzia ujumbe huo, Profesa
Lipumba alisema hiyo inaonyesha jinsi mkuu huyo wa nchi alivyolipa uzito bunge
hilo.
Profesa Lipumba ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ulioundwa na baadhi ya
wajumbe wa bunge hilo alisema ni jambo jema kwa Rais kulizindua Bunge hilo kwa
kuwa ndiye mwasisi wa mchakato wa Katiba Mpya... “Ujio wake utasherehesha Bunge
hili na nasaha zake zitatusaidia.”
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani bungeni alisema tendo la kuandika Katiba ni kubwa na
linalohusu wananchi wote hivyo ni dhahiri kuwa marais wastaafu na wake wa
waasisi wa Muungano wana fursa ya kipekee kuhudhuria uzinduzi huo.
“Nina hakika wapo viongozi wengine
walioalikwa. Kwa msingi huu, sina tatizo na ushiriki au ualikwa wao kwani bado
wana heshima katika jamii kama viongozi wastaafu,” alisema na kuongeza:
“Ni matumaini yangu kuwa hotuba ya
Rais itasaidia kupunguza hofu na hisia hasa kwa makundi yanayohasimiana katika
Bunge hili na siyo kuongeza hofu na ufa.”
Alisema wapo viongozi wa Bunge ambao
wamekuwa wakiwaona baadhi ya viongozi kama ni wafanya fujo... “Bunge la Katiba
ni tofauti na Bunge la kawaida na linahitaji kuvumiliana na kustahimiliana sana
wanachokitazama kama fujo kwa wengine ni staili muhimu ya kudai kusikilizwa.
Walichokiona kama fujo kimesaidia wabunge wote na hata Watanzania kusikia kwa
kina taarifa ya mheshimiwa Warioba. Fujo zile ndizo zilizozaa saa nne alizopewa
mheshimiwa Warioba na timu yake na kuleta utulivu mkubwa katika nchi.”
Alisema kilichoonekana kama rabsha na
fujo kwa Rais wakati alipozindua Bunge la 10 ndicho kilichozaa mchakato huu wa
Katiba. Katika Bunge hilo, wapinzani walisusia hotuba ya Rais Kikwete ambayo
pamoja na mambo mengine, alitangaza kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya.
Mjumbe wa Bunge hilo, Julius Mtatiro
alisema anatarajia Rais atasisitiza umuhimu wa maridhiano, maelewano,
kuheshimiana baina ya wajumbe na kuwataka watilie maanani masilahi ya taifa
badala ya kundi mojamoja au vyama.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment