Kificho jana alikana maoni hayo ya kutaka serikali tatu na kwamba kilichoelezwa na Jaji Warioba siyo tafsiri sahihi ya mapendekezo yao. PICHA|MAKTABA
Dodoma.Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) juzi jioni walipata
wakati mgumu katika kikao cha ndani cha wabunge wa chama hicho wakituhumiwa kwa
‘usaliti wa Muungano’.
Kilichowaponza wajumbe hao ni
kupitisha mabadiliko ya Katiba mwaka 2010 yanayoitaja Zanzibar kuwa ni nchi na
hivyo kuvunja Katiba ya Muungano na kitendo cha baraza hilo kupendekeza
Serikali tatu mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kikao hicho kilifanyika muda mfupi
baada ya Jaji Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba akieleza kuwa
changamoto kubwa za Serikali mbili ni uvunjaji wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano, uliotokana na Mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Katika hotuba yake, Jaji Warioba
alisema pia kuwa baraza hilo lilipendekeza mfumo wa Serikali tatu kutokana na
maelezo kuwa linataka Zanzibar huru, Tanganyika huru na Serikali ya Muungano
huru na kila chombo kuwa na mamlaka yanayotambuliwa.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho
kilichoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, zinaeleza kuwa wabunge wa CCM
hasa wa Bara walielekeza lawama kwa viongozi wa Zanzibar hasa Baraza la
Wawakilishi kutokana na kuwasaliti.
Chanzo chetu kimemtaja mmoja wa
wazungumzaji, Christopher Ole Sendeka kwamba alieleza kwa uchungu kuwa
mabadiliko yaliyofanywa na Zanzibar ni usaliti mkubwa kwa Serikali ya Muungano.
“Sendeka aliongea kwa uchungu kuhusu
Zanzibar kuvunja Katiba ya Muungano na alisema lazima chama kichukue hatua ili
kunusuru Muungano,” alisema mjumbe mmoja wa kikao hicho.
Alipoulizwa kuhusu kauli hizo,
Sendeka hakukanusha wala kukubali, bali alisema hayo ni masuala ya kikao cha
ndani na hawezi kuyazungumzia.
Mbunge mwingine aliyetajwa kuzungumza
ni Silivester Mabumba wa Jimbo la Dole, ambaye alieleza wazi kuwa ni vyema
kuacha unafiki kuwa mnataka Serikali mbili wakati kuna mabadiliko ambayo
mmepitisha kuwa Zanzibar ni nchi. Hata hivyo, Spika wa Bunge la Baraza la
Wawakilishi, Pandu Amir Kificho baada ya kushambuliwa alieleza kutofautiana na
kile ambacho kimeelezwa katika hotuba ya Jaji Warioba.
Kificho, licha ya kukiri kuwa mmoja
wa waliosaini taarifa ya baraza hilo, alisema bado msimamo wa baraza ulikuwa ni
Serikali mbili. Kauli hiyo ilithibitishwa jana baada ya kufafanua katika kituo
kimoja cha televisheni kuwa msimamo wa baraza haujawahi kuwa ni Serikali tatu.
Baada ya lawama nyingi, inadaiwa
wajumbe hao, walifikia azimio la kuandaa utaratibu wa kufanyia mabadiliko ya
Katiba ya Zanzibar kupitia kura ya maoni.
“Tumewaambia waone uwezekano wa
kuifanyia marekebisho Katiba yao kama ukipitishwa muundo wa Serikali mbili,”
alisema mjumbe mmoja.
Wawakilishi CUF wapinga
Hata hivyo, akizungumza na mwananchi
jana, Ismail Jussa, ambaye ni mwakilishi kutoka CUF, alisema wamesikia maazimio
ya kikao cha CCM lakini hawatakubali Katiba kufanyiwa marekebisho.
Jussa alisema mabadiliko ya 10 ya
Katiba ya Zanzibar, yalifuata sheria na kanuni na siyo rahisi kubadilishwa kama
viongozi wa CCM wanavyofikiri.
Naye Mbunge wa Ole (CUF), Mohamed
Mbaruku alisema iwapo CCM ikishinikiza kufanyika mabadiliko ya Katiba ya
Zanzibar, suala hilo watalifikisha mahakamani.
“Tumepata taarifa ya kikao chao,
lakini tunawaonya wasilete vurugu Zanzibar. Makubalino ya mabadiliko ya Katiba
ni sehemu ya mwafaka wetu, sasa wakileta hoja zao tutafika mahakamani,” alisema
Mbaruku.
Hotuba ya Warioba yawatibua
Kinachoonekana wazi ni kuwa hotuba ya
Jaji Joseph Warioba imelivuruga baraza hilo hasa baada ya kueleza kwamba kiini
cha tume kupendekeza Muungano uwe wa Serikali tatu ni pamoja na maoni ya Baraza
la Wawakilishi Zanzibar. Kificho jana alikana maoni hayo ya kutaka serikali
tatu na kwamba kilichoelezwa na Jaji Warioba siyo tafsiri sahihi ya mapendekezo
yao.
“Hii inaonyesha kwamba Tume yenyewe
ilishakuwa na mwelekeo wa serikali tatu kwa sababu kama alivyoeleza Jaji
Warioba kwamba walitafsiri maoni yetu kuwa ni yenye kuhitaji serikali tatu, na
wakati mwingine, tafsiri inaweza kukupa maana tofauti na maana halisi,”
alieleza Kificho alipohojiwa na TBC1.
Kificho alisema baraza hilo linaundwa
na wawakilishi kutoka vyama mbalimbali – CCM na CUF na msimamo wa CCM ni
serikali mbili na hana uhakika kwa upande wa CUF, ingawa anadhani ni msimamo wa
serikali tatu. Hivyo ni vigumu kudai Baraza la Wawakilishi limepeleka
mapendekezo yenye msimamo mmoja.
Maoni ya Kificho yalipingwa na
Mwakilishi Rufai Said Rufai aliyesema kuwa alichosema Jaji Warioba ndicho
kilichomaanishwa na baraza.“Ingawa sikuwa mjumbe katika Kamati ya Uongozi, kwa
nafasi yangu ya uwakilishi, naafikiana kuwa maoni yaliyosomwa na Jaji Warioba
bungeni ndiyo haswa tuliyopeleka na jinsi alivyoyatafsiri ndivyo
tulivyomaanisha,” alieleza Said.
“Unaweza vipi kukana kudai serikali
tatu, wakati unatoa maoni yanayodai kuwapo kwa mamlaka huru ya Zanzibar,
mamlaka huru ya Tanganyika na mamlaka ya Muungano yaliyowekwa wazi maeneo,
uwezo, nguvu, utendaji na mipaka ya kila mamlaka? Wanaokataa, wanakataa
wanachokubali,” alifafanua Said.
Mjumbe mwingine ambaye yumo kwenye
Kamati ya Uongozi, Abdallah Juma Abdallah alisema anayekana kauli ya Jaji
Warioba hana akili na anajikanyaga.
Imeandikwa na Sharon Sauwa na Mussa
Juma.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment