Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
limetoa idhini kwa nchi wanachama wa Umojawa Mataifa, kuzizuia meli
zinazoshukiwa kubeba mafuta ghafi kinyume cha sheria kutoka kwenye bandari
zinazodhibitiwa na waasi wa Libya.
Waasi wa Libya
Azimio hilo lililopitishwa jana
Jumatano kwa kauli moja na wanachama wote 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa, linayaruhusu mataifa wanachama wa Umoja huo kuingia ndani ya meli
wanazozishuku kubeba mafuta ghafi, ambazo zimeripotiwa na kamati ya baraza hilo
inayofuatilia vikwazo dhidi ya Libya na kuzikagua na kisha kuziamuru kurejesha
mafuta hayo nchini Libya.
Azimio hilo limepitishwa baada ya
Marekani kuizuia meli iliyokuwa na bendera ya Korea Kaskazini katika pwani ya
Cyprus, ambayo waasi wa Libya wamekuwa wakiitumia kusafirisha mafuta nje ya
nchi kinyume cha sheria.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power
Azimio hilo linalaani majaribio
yoyote ya kusafirisha nje ya nchi mafuta ghafi kutoka Libya, yanayofanywa
kinyume cha sheria. Katika taarifa yake, balozi wa Marekani kwenye Umoja wa
Mataifa, Samantha Power amewataka wanachama wa umoja huo kulitekeleza azimio
hilo haraka, ili kuzuia vitendo vinavyofanywa na watu wanaojaribu kuiba mafuta
ya Libya.
Samantha Power amesema utekelezaji wa
sheria hizo ni ishara kwa watu wa Libya pamoja na serikali ya nchi hiyo kwamba
jumuiya ya kimataifa inaunga mkono uhuru wa Libya na haki yake ya kusimamia
rasilimali zake.
Serikali ya Libya na waasi wazozana
Mvutano wa muda mrefu umekuwa
ukiendelea kati ya serikali ya Libya na kiongozi wa waasi, Ibrahim Jathran,
baada ya kiongozi huyo na wapiganaji wake kuchukua udhibiti wa bandari tatu
kubwa za mafuta mwaka uliopita, wakitaka kujitenga kwa eneo la mashariki mwa
Libya na kuwa na uhuru zaidi wa kujitawala pamoja na kupata sehemu kubwa ya
utajiri wa mafuta. Tangu wakati huo, waasi hao wamekuwa wakijaribu kuuza mafuta.
Kaimu Waziri Mkuu wa Libya Abdullah al-Thani
Serikali ya Libya imewapa waasi hao
muda wa wiki mbili kuondoka kwenye bandari hizo au kukabiliwa na mashambulizi
ya kijeshi kwa lengo la kumaliza mzozo huo. Kitendo cha waasi hao kudhibiti
bandari hizo kubwa za mafuta, kimesitisha uchimbaji wa mafuta kwa mapipa
bilioni 1.4 kwa siku na bajeti ya Libya kwa kiasi kikubwa inategemea mapato
yatokanayo na mafuta.
Kashfa ya waasi kupakia mafuta ghafi
kwenye meli hiyo na kufanikiwa kukikwepa kikosi cha jeshi la majini cha Libya,
ilisababisha bunge kumtimua Waziri Mkuu, Ali Zeidan, baada ya kupiga kura ya
kutokuwa na imani naye, tarehe 11 ya mwezi huu wa Machi.
Libya bado inapambana kujikwamua
kutokana na matatizo yaliyofuatia vuguvugu la mapinduzi ya mwaka 2011,
yaliyomuondoa madarakani kiongozi aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Moammar
Gaddafi.
Mwandishi: Grace
Kabogo/RTRE,AFPE,APE,DPAE
Mhariri: Gakuba, Daniel
No comments:
Post a Comment