Baadhi ya wananchi, wasomi na
wanasiasa huko visiwani Zanzibar wamesema muundo wa Serikali tatu
uliopendekezwa katika rasimu ya pili ya katiba utachangia kuudhofisha Muungano
wa Tanzania na kuondokana na uzalendo uliodumu na kuimarika kwa miaka 50 tangu
kuasisiwa kwake na hayati Mwalimu Julius kambarage Nyerere na marehemu Sheikh
Abeid Amani Karume.
Ripoti ya Munir Zakaria, Zanzibar
Mara baada ya kuwasilishwa kwa rasimu
ya pili ya katiba katika bunge maalum la katiba, huko visiwani Zanzibar
kumekuwepo na gumzo kubwa kuhusu mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu hiyo,
ambapo pia biashara ya CD zenye hotuba na masuala ya rasimu ya katiba zinauzwa
kwa wingi katika soko kuu la Darajani.
Wakizungumza katika mahojiano maalum
baadhi ya wasomi na wanasiasa wamesema mfumo wa serikali mbili ulipaswa
kufanyiwa marekebisho na kutatua changamoto pamoja na kero zote za muungano,
badala ya kuanzisha utaratibu mpya wa kuwa na serikali tatu ambao unaweza
kudhoofisha Muungano.
Miongoni mwa waliotoa maoni yao ni
pamoja na mwanasheria mkongwe hapa nchini Hamid Mbwezeleni, pamoja na baadhi ya
wanasiasa na wananchi ambao wamesema kuwa muungano wa serikali mbili ndio
unaofaa kuendelea kutumika kwa vile umeijengea heshima Tanzania na kuwa mfano
bora mbele ya jumuiya ya kimataifa kwa kuwa na Muungano uliodumu kwa miaka 50.
Chanzo: VOA Swahili
No comments:
Post a Comment