Mkutano wa kilele wa viongozi wa
Umoja wa Ulaya unaanza leo mjini Brussels ambako viongozi hao wanatarajiwa
kuliimarisha shinikizo dhidi ya Urusi.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya walikuwa
wayajadili masuala ya ustawi wa uchumi ,nishati na mabadiliko ya sera ya tabia
nchi.
Lakini badala yake suala la Ukraine
ndilo litakalopewa kipa umbele kutokana na kuzidi kwa mvutano baina ya nchi za
Umoja wa Ulaya na Urusi baada ya Rais Putin kuitia saini rasimu juu ya
kuliingiza jimbo la Krimea katika shirikisho la Urusi.
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya
Hermann Van Rompuy na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja huo Jose Manuel Barroso
wamethibitisha kwamba suala la Ukraine ndilo litakalokuwa la kipaumbele kwenye
mkutano.Naye Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Cathrine Ashton amesisitiza
kwamba suala la Ukraine litakuwa mbele katika ajenda.
Mazungumzo na Urusi hayatafanyika
Umoja wa Ulaya umeshayafuta
mazungumzo ya kisiasa na Urusi na wiki hii ulitangaza vikwazo dhidi ya nchi
hiyo. Hata hivyo serikali za nchi za Umoja wa Ulaya bado hazijaufikia msimamo
wa pamoja juu ya suala hilo.Baadhi ya nchi hususan zile zenye uhusiano mkubwa
wa kibiashara na Urusi zinahofia kuchukua hatua kali zaidi zinazoweza kuzifunga
njia zote za mazungumzo na Urusi.
Waziri wa mambo ya nje wa Austria
Sebastian Kurz ametahadharisha juu ya kufanya pupa katika kuchukua hatua za
kiuchumi dhidi ya Urusi wakati Bulgaria inayotegemea gesi kutoka Urusi imesema
inapinga kuchukuliwa hatua za haraka za kuiwekea Urusi vikwazo vikali. Lakini
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank- Walter Steinmeier amesema vikwazo
dhidi ya Urusi haviwezi kukwepeka ikiwa Urusi itaendelea kujitandaza zaidi.
Katibu Mkuu kufanya ziara Urusi na Ukraine
Wakati huo huo Katibu Muuu wa Umoja
wa Mataifa Ban Ki-moon anatarajiwa kuwasili Moscow kwa ajili ya mazungumzo na
Rais Wladimir Putin na viongozi wengine wa Urusi juu ya mgogoro wa Ukraine.
Katibu Mkuu Ban, pia atafanya ziara Ukraine katika juhudi za kutafuta suluhisho
la kidiplomasia.
Mabalozi watoleana kauli kali
Kwenye Umoja Mataifa mabalozi wa
Urusi na Marekani walitoleana kauli kali kuhusiana na mgogoro wa Ukraine.
Balozi wa Marekani Samantha Power ameiita Urusi kuwa ni mwivi kwa sababu ya
matukio ya jimbo la Krimea. Na Balozi wa Urusi, amesema kuwa kauli za kashfa
zilizotolewa na Balozi wa Marekani dhidi ya nchi yake zitauhatarisha
ushirikiano baina ya nchi zao.
Nchini Ukraine kwenyewe serikali ya
muda imearifu kwamba inaandaa mipango ya kuwaondoa wanajeshi wake kutoka jimbo
la Krimea .
Mwandishi:Bernd Riegert.
Tafsiri:Mtullya Abdu.
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman
No comments:
Post a Comment