Mheshimiwa
Samuel Sitta, Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba;
Mheshimiwa
Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa
Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa
Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa
Anne Semamba Makinda; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
Mheshimiwa
Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Muda wa
Bunge Maalum la Katiba ;
Mheshimiwa
Rashid Othman Chande, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Viongozi
Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa
Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Wageni
waalikwa;
Mabibi
na Mabwana;
Pongezi
Nakushukuru
sana Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa fursa ya kuja kuzungumza na Waheshimiwa
Wajumbe wa Bunge letu Maalum la Katiba katika siku hii muhimu na ya kihistoria
kwa nchi yetu. Nimekuja kuwatakia heri na naungana na Watanzania wenzetu wote
kuwaombea baraka za Mwenyezi Mungu, ili muweze kuifanya kazi yenu kwa utulivu,
hekima, umakini mkubwa na kuimaliza kwa salama na kwa mafanikio
yanayoyatarajiwa na Watanzania.
Natoa
pongezi nyingi kwako na kwa Makamu wako kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge
hili maalumu na la kihistoria. Ushindi mkubwa mliopata ni kielelezo tosha cha
imani kubwa na matumaini waliyonayo Wajumbe wenzenu kwenu. Matumaini yao ndiyo
matumaini ya Watanzania wote, kwamba mtaliongoza vizuri Bunge hili, ili liweze
kutimiza kwa ufanisi mkubwa jukumu lake muhimu sana katika historia ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Niruhusu
pia niwapongeze kwa dhati Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa bahati ya
aina yake waliyopata ya kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Fursa hii hutokea mara chache sana katika historia ya nchi yo yote na watu
wake. Mkifanikiwa kuipatia nchi yetu Katiba nzuri majina yenu yataandikwa kwa
wino wa dhahabu, katika kumbukumbu za historia ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Ni
matarajio ya Watanzania kuwa mtatunga Katiba itakayokubalika na wengi. Katiba
inayotekelezeka. Katiba itakayoimarisha Muungano wetu kwa kuondoa changamoto
zilizopo sasa. Katiba itakayoipa nchi yetu mfumo bora wa kuongoza na kuendesha
mambo yetu. Katiba itakayoimarisha umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano
miongoni mwa wananchi wa Tanzania, licha ya tofauti zao za asili za upande wa
Muungano na maeneo watokako, au tofauti za jinsia, rangi, kabila, dini na
ufuasi wa vyama vya siasa. Katiba itakayodumisha amani, usalama na utulivu
nchini. Katiba itakayostawisha zaidi demokrasia, haki za binadamu, utawala wa
sheria, utawala bora na kudhibiti maovu.
Na,
mwisho ingawaje siyo mwisho kwa umuhimu, Katiba itakayoweka mazingira mazuri
kwa uchumi wa nchi kukua, na wananchi wengi kunufaika sawia na maendeleo
yatayopatikana.
Historia
ya Katiba Nchini
Mheshimiwa
Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Hii
itakuwa mara ya tatu tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili
26, 1964, kwa nchi yetu kuwa na mchakato wa kutunga Katiba mpya. Mara ya kwanza
ilikuwa mwaka 1965 ilipotungwa Katiba ya Muda na mara ya pili ni mwaka 1977
ilipotungwa Katiba ya Kudumu tuliyonao sasa. Tofauti na mara mbili zilizopita,
safari hii mchakato unahusisha watu wengi zaidi.
Wananchi wameshiriki moja kwa
moja kutoa maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na ndio watakaofanya
uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba mpya kwa kura ya maoni. Wananchi pia walipata
nafasi ya kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yaliyojadili Rasimu
ya Kwanza ya Katiba. Pia walipata nafasi ya kutoa maoni yao kupitia Mabaraza ya
Katiba ya taasisi. Katika Bunge hili wapo wananchi 201 kutoka makundi
mbalimbali.
Katika
mchakato wa kutunga Katiba za mwaka 1965 na 1977 kulikuwapo Tume za Kuandaa
Rasimu na Bunge Maalum la Katiba kama ilivyo katika mchakato huu. Hata hivyo,
kwa Katiba zilizopita Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano pekee ndio
waliounda Bunge Maalum. Safari hii Bunge Maalum linajumuisha Wabunge, Wajumbe
wa Baraza la Wawakilishi na wananchi 201 wanaotoka kwenye jamii, wakiwakilisha
asasi na makundi mbalimbali ya Watanzania kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.
Mchakato wa sasa utaishia kwenye kura ya maoni itakayoshirikisha wananchi wote
wa Tanzania wanaoruhusiwa kupiga kura. Michakato iliyopita iliishia Bunge
Maalum pekee.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Tangu
kutungwa kwake, tarehe 25 Aprili, 1977, mpaka sasa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ya mwaka 1977 imefanyiwa mabadiliko takriban mara 14. Mabadiliko hayo
yalitokana na kufanyika au kutokea kwa mabadiliko muhimu ya kiuchumi, kisiasa
na kijamii katika nyakati mbalimbali hapa nchini na katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Kwa
ruksa yako naomba nitaje baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa:-
Mabadiliko
ya 1979 yaliunda Mahakama ya Rufani ya Tanzania kufuatia kufa kwa Mahakama ya
Rufani ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki
mwaka 1977.
Mabadiliko
ya mwaka 1980 yalifanyika baada ya kutungwa kwa Katiba ya Zanzibar, hivyo
kulazimu Katiba hiyo kutambulika kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Mabadiliko
ya mwaka 1984 yaliweka utaratibu wa ukomo wa vipindi vya Urais ambao haukuwepo
kabla ya hapo. Aidha, masuala ya Haki za Binadamu (Bill of Rights) yaliingizwa
kwa mara ya kwanza katika Katiba. Vilevile, Mahakama ya Rufani ya Tanzania na
mambo mengine ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliongezwa katika
Orodha ya Mambo ya Muungano.
Mwaka
1992, yalifanyika mabadiliko yaliyoanzisha Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa badala
ya ule wa Chama kimoja uliokuwepo tangu 1965. Pia utaratibu wa uchaguzi wa Rais
na Wabunge ulirekebishwa ili uendane na mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Vilevile utaratibu wa kuwa na viti maalum vya wanawake katika Bunge
ulianzishwa. Wakati ule ilikuwa asilimia 15 ya Wabunge wote. Aidha, kwa mara ya
kwanza katika historia ya nchi yetu Bunge lilipewa mamlaka ya kumwajibisha Rais
na Waziri Mkuu kupitia kura ya kutokuwa na imani.
Mabadiliko
ya mwaka 1994 yaliweka mfumo mpya wa kumpata Makamu wa Rais kupitia Mgombea
Mwenza.
Mwaka
2000 na 2005, pamoja na mambo mengine yalifanyika mabadiliko yaliyopanua wigo
wa Haki za Binadamu na kuongeza uwakilishi wa wanawake.
Umuhimu
wa Mabadiliko ya Katiba
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kufanyika
kwa mabadiliko hayo kunathibitisha utayari wa Serikali kufanya mabadiliko kila
ilipoonekana inafaa kufanya hivyo. Pamoja na kufanya yote hayo na Serikali kuwa
na msimamo huo, kumekuwepo na madai yaliyokuwa yanajirudia ya kutaka Katiba ya
Tanzania iandikwe upya. Wako watu walioimithilisha Katiba yetu na nguo yenye
viraka vingi mno kiasi kwamba ingefaa kununua mpya badala ya kuendelea kuivaa.
Madai
ya kutaka Katiba mpya yalipazwa sauti baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi
vya siasa. Wapo waliokuwa wanadai Katiba mpya kwa imani, eti kwamba,
itawawezesha kuishinda CCM. Lakini, si hayo tu, hata katika mchakato wa
Serikali zetu mbili kushughulikia kero za Muungano, imedhihirika kuwa baadhi ya
changamoto zilikuwa zinahitaji mabadiliko ya Katiba ili kuzipatia ufumbuzi wa
uhakika na wa kudumu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa
kutambua ukweli huo na baada ya kushauriana na kukubaliana na viongozi wenzangu
wakuu wa Chama tawala na Serikali zetu mbili wakati ule, ndipo tarehe 31
Desemba, 2010, nikatangaza dhamira ya kuanzisha mchakato wa kutunga Katiba
mpya. Nilieleza siku ile kuwa katika mchakato huo tutakuwa na ushirikishwaji
mpana wa wananchi wa Tanzania kwa makundi yao ya jinsia, dini, siasa na
shughuli wazifanyazo kujipatia riziki na kwa maeneo wanayotoka katika pande
zetu mbili za Muungano.
Mchakato
wa Katiba Mpya
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Tarehe
16 Machi, 2011 Baraza la Mawaziri liliridhia kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba ya kuliongoza taifa katika mchakato wa kutunga Katiba mpya ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Tarehe 18 Novemba, 2011 Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania lilipitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa mujibu
wa Sheria hiyo, mchakato wa kutunga Katiba Mpya ulikuwa unaanza kwa kuunda Tume
ya Mabadiliko ya Katiba. Tume hiyo imepewa jukumu la kusikiliza maoni ya
wananchi mmoja mmoja na kwa makundi yao ya maslahi, taasisi zao na kupitia
Mabaraza ya Katiba. Mwishowe Tume imetakiwa kutengeneza Rasimu ya Katiba mpya
itakayofikishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba kujadiliwa na Katiba mpya
kutungwa. Mchakato wa Katiba utahitimishwa kwa wananchi kupiga kura ya maoni ya
kuamua kama wanaikubali au kuikataa Katiba mpya.
Tarehe
6 Aprili, 2012 nilifanya uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na
kuwaapisha tarehe 13 Aprili, 2012. Tume ilianza kazi tarehe 2 Mei, 2012 na
kuikamilisha kwa mafanikio, hatua zote zilizoihusu na kukabidhi kwangu na kwa
Rais wa Zanzibar, Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba tarehe 30 Desemba, 2013.
Kitendo cha Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu
hiyo mbele ya Bunge hili tukufu tarehe 18 Machi, 2014, kinahitimisha rasmi kazi
ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kazi inayofuatia ni ya Bunge hili kujadili,
kuamua na kutunga Katiba mpya. Baada ya hapo Katiba mpya itafikishwa kwa
wananchi kwa uamuzi wa mwisho kwa njia ya kupiga kura ya NDIYO au HAPANA.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Rasimu
ya Katiba ilichapishwa kwenye gazeti la Serikali na magazeti mengine
yanayosomwa na wananchi kama ilivyoagizwa katika Kifungu cha 20(2) cha Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na hayo, Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba
viliwekwa wazi kwenye tovuti ya Tume kwa kila mtu kusoma. Inafurahisha kuona
kuwa watu wengi wameisoma Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba na kumekuwa na
mjadala mpana kuhusu nyaraka zote hizo muhimu. Watu wengi wametoa maoni yao na
wanaendelea kufanya hivyo. Kwa maoni yangu hili ni jambo jema sana na ni
kielelezo thabiti kuwa demokrasia imestawi na inazidi kuota mizizi Tanzania.
Pia, kwamba, Watanzania wako huru kushiriki na kutoa maoni yao kwa mambo
yanayowahusu.
Pongezi
kwa Tume
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa
mara nyingine tena narudia kutoa pongezi za dhati kwa Wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba
akisaidiwa na Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani, kwa kazi kubwa na nzuri
waliyofanya. Kazi yao haikuwa rahisi hasa ukizingatia ukubwa wa nchi yetu,
wingi wa watu wake, utitiri wa taasisi na pigo la kumpoteza Mjumbe mwenzao
muhimu Dkt. Sengondo Mvungi aliyetangulia mbele ya haki katikati ya mchakato.
Pamoja
na hayo, kwa bidii kubwa Wajumbe wa Tume wameweza kutembelea mikoa yote nchini
na kuwafikia watu 351,644 waliotoa maoni yao kwa mdomo na kwa maandishi.
Halikadhalika, walipokea na kuchambua maoni 772,211 kutoka kwa wananchi na
taasisi mbalimbali. Baada ya kupokea maoni ya wananchi, kufanya utafiti na kwa
kutumia maarifa na uzoefu wao, Wajumbe wakafanya kazi ngumu, kuliko yote, ya
kutengeneza Rasimu ya Katiba iliyoko mbele ya Bunge hili. Ni kweli kwamba
Wajumbe hawakuweza kuwafikia wananchi wote wa Tanzania, lakini wameweza
kuwafikia wananchi wengi, ambao kwa kiasi kikubwa wanawakilisha taswira na
mitazamo mipana ya jamii yetu.
Baadhi
ya Masuala Yaliyojitokeza Katika Mjadala wa Mapendekezo ya Tume
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Tume
imefanya kazi nzuri, yenye thamani kubwa na ya manufaa kwa taifa la Tanzania.
Rasimu imeandikwa vizuri na kwa weledi wa hali juu. Tume imetoa mapendekezo
ambayo kwa kiasi kikubwa yanahuisha na kuboresha Katiba ya nchi yetu, kwa namna
ya pekee. Katiba inayopendekezwa, imejumuisha dhana na mambo kadhaa mapya
yanayokwenda vyema na wakati tulionao na kuweka msingi mzuri kwa huko mbele
tuendako. Kwa taratibu za kawaida za marekebisho ya Katiba tuliyonayo,
isingekuwa rahisi kuingiza mambo mengi mapya kiasi hiki.
Wajumbe
Wana Kazi Kubwa
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Waheshimiwa
Wajumbe;
Rasimu
ya Katiba ni kitabu kikubwa kilichosheheni mambo mengi. Kina kurasa 106, sura
17 na ibara 271. Wajumbe wa Bunge hili mnatakiwa kusoma na kuelewa vizuri kila
kilichoandikwa ili muweze kufanya uamuzi ulio sahihi. Mnawajibika kuchambua kwa
kina na umakini mkubwa kila kilichomo, sura kwa sura, ibara kwa ibara, sentensi
kwa sentensi na hata neno kwa neno. Hamna budi kujiridhisha kuhusu uandishi wa
vifungu vya Rasimu ya Katiba na kufaa kwa dhana mbalimbali zilizoingizwa na
kujengeka katika Rasimu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kile
ambacho Wajumbe mtaona kinastahili kuboreshwa au kurekebishwa au kufutwa
msisite kufanya hivyo ili Watanzania wapate Katiba iliyo bora. Msipofanya hivyo
kuna hatari ya kupata Katiba ambayo ni ngumu kuitekeleza. Aidha, tunaweza kuwa
na Katiba ambayo itanung’unikiwa na watu wengi na kusababisha madai ya kutaka
ifanyiwe marekebisho muda mfupi baada ya kupitishwa. Bunge hili linao wajibu
maalum wa kuzuia balaa hilo lisitokee katika nchi yetu. Ngazi mbalimbali
zilizowekwa katika mchakato huu ni kama chujio la kuepusha hali hiyo isitokee.
Kile ambacho hakikuonekana katika hatua moja kitaonekana katika hatua
inayofuata na kurekebishwa. Nawaomba fursa mliyonayo muitumie vizuri.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Nimekwishaeleza
kuwa moja ya jambo mnalotegemewa kufanya ninyi wenzetu mliopewa dhamana ya
kutunga Katiba ya nchi yetu ni kujiridhisha na uandishi wake. Yapo maoni
yaliyotolewa kuhusu uandishi ambayo naomba myatafakari na kuamua ipasavyo. Kwa
mfano, kuna baadhi ya vifungu vya Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo
mengi mno kuliko inavyostahili Katiba kuwa (too prescriptive). Pia kuna mawazo
kwamba baadhi ya mambo hayangetakiwa kuwa katika Katiba bali yawe kwenye Sheria
zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Yako
mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ambayo yanatakiwa kuelezwa wazi kuwa mtu
hatakwenda mahakamani kuidai Serikali impatie (non justiciable). Mambo
yaliyotajwa kwenye Katiba ni mazuri na yanavutia, lakini lazima yaendane na
uwezo wa nchi na uchumi wake kuhimili. Simaanishi kwamba tuyatoe kwenye Katiba,
bali yabakie kama dhamira pale uwezo wa nchi utakaporuhusu yatekelezwe.
Tusipofanya hivyo, kuna hatari ya Serikali kujikuta inalaumiwa au hata
kufikishwa mahakamani kila wakati kwa madai ya jambo moja au jingine ambayo
haina uwezo nayo. Ni muhimu sana mambo kama hayo muyatazame ili tusije kuwa na
Katiba ambayo ni ngumu kutekeleza.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Yapo
pia maoni kuwa baadhi ya vifungu vina upungufu katika uandishi wake, hivyo
kuhitaji kufanyiwa marekebisho. Isipofanyika hivyo kunaweza kuwepo athari na
nyingine zinaweza kuwa mbaya. Kwa mfano, Ibara ya 2 ya Rasimu inayotambulisha
eneo na mipaka ya nchi yetu. Ibara hiyo inasomeka kuwa “Eneo la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ni eneo lote la Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya
bahari na eneo lote la Zanzibar likijumuisha sehemu yake ya bahari”.
Maelezo
hayo yameacha kutambua, kwa upande wa Tanzania Bara, sehemu yetu ya maziwa na
mito ambayo ni kubwa sana. Kwa nini tuache kuitaja? Je hatutoi nafasi kwa nchi
tunazopakana nazo siku moja wakaja kupora sehemu zetu hizo na sisi kukosa
utetezi kwa kuwa hata Katiba yetu haikuyatambua maeneo hayo kuwa ni yetu? Hili
ni jambo kubwa ambalo Bunge hili lazima mlirekebishe. Wakati ndiyo huu hakuna
mwingine.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Jambo
jingine kuhusu uandishi ni mgongano kati ya pendekezo la msingi la Tume la kuwa
na muundo wa Serikali tatu na majukumu ya Serikali ya Muungano ambayo kimsingi
ni majukumu ya Serikali za nchi washirika. Katika Rasimu hii malengo ya taifa
yameainishwa na Serikali ya Muungano inatakiwa kuhakikisha kuwa malengo hayo
yanatekelezwa na itoe taarifa Bungeni.
Katika mfumo wa Serikali tatu
unaopendekezwa na Tume masuala yahusuyo uchumi na maendeleo ya jamii kama vile
kukuza kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, biashara, pembejeo, elimu, hifadhi ya
jamii na kadhalika yako chini ya mamlaka ya Serikali za nchi washirika. Mamlaka
ya Serikali ya Muungano ni kwa mambo saba tu yafuatayo:- Katiba na Mamlaka ya
Jamhuri ya Muungano, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano, Uraia na
Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa, Ushuru
wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
Kwa
Rasimu kupendekeza muundo wa Serikali tatu na kuipa Serikali ya Muungano majukumu
ambayo haina mamlaka nayo, ni kuzusha utata na migongano kati ya Serikali ya
Muungano na nchi washirika. Mkichagua mfumo wa Serikali tatu, inawalazimu
muyaondoe mambo hayo kwani Serikali ya Muungano haistahili kuyatekeleza na wala
haina uwezo wa kuweka masharti kwa Serikali za nchi washirika kwa mambo yaliyo
kwenye mamlaka ya nchi hizo.
Lakini kama mtaamua tuendelee na muundo wa
Serikali mbili, mambo haya mazuri yanatekelezeka na Serikali ya Muungano bila
ya matatizo. Katika uandishi wa Rasimu Utumishi katika Serikali ya Muungano
haumo katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Ni lazima liwemo. Hayo ni baadhi tu
ya masuala yahusuyo uandishi katika Rasimu. Naamini mkiisoma Rasimu kwa makini
mnaweza kuyagundua mengineyo.
Dhana
Mpya
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Katika
Rasimu kuna dhana mpya na mambo mapya kadhaa yaliyoingizwa ambayo yanabadili
utaratibu wa sasa wa uendeshaji wa nchi na mambo mbalimbali. Nawaomba mfanye
uchambuzi wa kina kwa kila kinachopendekezwa na kujiridhisha kuhusu kufaa kwake
na manufaa yake. Fanyeni hivyo ili tujihakikishie kuwepo kwa mambo mazuri na
uendeshaji mzuri wa shughuli katika taifa letu changa.
Mambo
ni mengi na kwa ufinyu wa muda sitaweza kuyazungumzia yote. Niruhusuni
nizungumzie baadhi ya dhana na mambo mapya yaliyomo katika Rasimu. Jambo la
kwanza, kwa mfano, linahusu Ibara ya 128 (2)(d) inayoleta dhana ya “Mbunge
kupoteza Ubunge iwapo atashindwa kufanya kazi za Mbunge kwa miezi sita
mfululizo kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza”.
Watu
hawana tatizo na Mbunge kuwa kizuizini ndani ya gereza kama amepatikana na
hatia Mahakamani na kuhukumiwa kifungo. Lakini, isijekuwa yuko rumande kwa
tuhuma akisubiri kesi kusikilizwa. Je akija kuonekana hana hatia na kuachiliwa?
Naungana na wale wanaoshauri kuwa jambo hili lifafanuliwe vizuri na kutambua
Mbunge kutiwa hatiani na kupata adhabu ya kifungo cha kipindi hicho. Ni bora
ifanyike hivyo sasa ili kuondoa mikanganyiko. Hakuna haja ya kusubiri mpaka
jambo hili lije kufafanuliwa baadaye kwa Sheria itakayotungwa na Bunge.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa
upande wa mtu kupoteza Ubunge kwa sababu ya “kuugua kwa miezi sita mfululizo”
ni maoni ya watu wengi kuwa huu ni ukatili ambao haustahili kufanywa na Katiba.
Kuugua ndiyo ubinadamu na wakati mwingine Mbunge anaweza kupata ajali
akiwatumikia wananchi wa Jimbo lake. Anaweza kuugua kwa miezi sita au zaidi na
kupona kabla ya kipindi chake cha Ubunge kufika mwisho. Kwa nini awekewe ukomo
wa miezi sita? Katiba ya mwaka 1977 tunayotumia sasa haina sharti hilo.
Watu
wanauliza hoja na haja ya kuwa na sharti hili kwenye Katiba mpya ni ipi?
Wanasema kwa kweli anachostahili Mbunge huyu kufanyiwa ni kuuguzwa afya yake
iimarike ili aendelee kutumikia watu wake, na siyo kupoteza uongozi wake.
Tusiwatie watu kishawishi cha kukatiza matibabu ili kukwepa sharti hilo. Ni
vyema jambo hili mkalitazama kwa makini, na muone kama linastahili kuwepo au
hapana.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Katika
Rasimu hii imeingizwa dhana mpya ya kuweka ukomo wa vipindi vitatu kwa Wabunge.
Tena mapendekezo haya hayasemi vipindi vitatu mfululizo au la!. Jambo hilo
limezua mjadala motomoto katika jamii. Ni vizuri mkajiridhisha juu ya sababu za
msingi na manufaa ya kufanya hivyo hapa Tanzania. Mazoea yetu na ya kwingineko
duniani ni kuweka ukomo kwa Wakuu wa Nchi kwa sababu nzuri na rahisi kuzielezea.
Lakini, kuwawekea ukomo Wabunge ni jambo jipya na huenda Tanzania tukawa wa
kwanza. Nashawishika kuungana na wale wanaopendekeza kuwa pengine ni mapema mno
kuanzisha utaratibu huo hapa kwetu.
Nachelea
kuwa tutainyima nchi yetu fursa ya kupata watu wenye maarifa na uzoefu mzuri wa
uongozi kwa nafasi ya Ubunge au kwa nafasi za uongozi wa Taifa bila ya sababu
za msingi.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Jambo
lingine jipya linalopendekezwa na Tume ni utaratibu wa kumuondoa Mbunge
katikati ya kipindi chake cha uongozi. Kwa hoja linaonekana kuwa jambo jema
lakini naomba athari zake mzitafakari vizuri. Kuna hatari ya kuanzisha
misuguano kwenye Majimbo na kuwaacha Wabunge wasifanye kazi zao kwa utulivu
bali wawe wanajihami dhidi ya wapinzani wao kuwatengenezea fitna za kuwatoa.
Utaratibu unaopendekezwa wa Chama chake kujaza nafasi ya Mbunge inapokuwa wazi
katika mazingira hayo nao unaweza kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha vuguvugu la
kumuondoa Mbunge. Walioshindwa kwenye kura ya maoni wanaweza kufanya kazi ya
kuwachimba wenzao mpaka waondoke. Jipeni muda wa kupima faida na hasa thamani
inayoongezwa na kuanzisha utaratibu huo. Naomba tujiridhishe kama jambo hili
jipya lina tija. Hivi kupewa nafasi kila miaka mitano kurudi kwa wananchi
hakutoshi kumuondoa Mbunge ambaye watu wamemchoka?
Muundo
wa Muungano
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Jambo
lingine kubwa lililopendekezwa na Tume ambalo limevuta hisia za karibu watu
wote nchini linahusu muundo wa Muungano wetu kuwa wa Serikali tatu badala ya
mbili za sasa. Pendekezo hili limezua mjadala mkubwa tangu lilipotolewa katika
Rasimu ya kwanza na kurudiwa katika Rasimu ya pili. Wakati mwingine mjadala
umekuwa mkali na wa hisia kali kwa kila upande.
Kwa
kweli hili ndilo jambo kubwa kuliko yote katika Rasimu kwa sababu linapendekeza
kuanzishwa kwa muundo na mfumo mpya wa kuendesha nchi yetu. Hii ndiyo agenda
mama ya Bunge hili ambayo kila Mtanzania anasubiri kwa hamu uamuzi wenu utakuwa
upi. Ombi langu kwenu ni kuwa watulivu mnapojadili suala hili. Epukeni jazba
ili mfanye uamuzi ulio sahihi. Lazima mtambue uamuzi usiokuwa sahihi kwa jambo
hili una hasara kubwa. Tunaweza kupoteza kitu tulichokijenga kwa gharama kubwa
kwa nusu karne iliyopita. Tanzania inaweza kuwa nchi iliyojaa migogoro na
matatizo mengi ambayo hatunayo.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Waheshimiwa Wajumbe;
Kama
alivyoeleza Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba, mara
kadhaa, mjadala au madai ya kutaka muundo wa Serikali tatu si jambo jipya.
Ulikuwepo hata wakati wa mazungumzo ya kuunganisha nchi zetu mbili mwaka 1964.
Ulikuwa kiini cha kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar mwaka 1984.
Muundo huu uliwahi kupendekezwa na Tume ya Nyalali mwaka 1992, ndiyo hoja ya
G55 mwaka 1993 na umependekezwa pia na Tume ya Jaji Kisanga ya mwaka 1998.
Lakini mara zote hizo mapendekezo hayo hayakukubaliwa.
Waasisi
wa taifa letu, yaani Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya
Tanganyika wakati ule na Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Jamhuri
ya Watu wa Zanzibar wakati ule, waliamua kuchagua Muungano wa Serikali mbili
tulionao sasa. Walitoa sababu mbili kuu: “ni muundo unaoihakikishia Zanzibar
kuwa haimezwi na Tanganyika; na pia unaiepusha Tanganyika kubeba mzigo mkubwa
wa kugharamia Serikali ya Tanganyika na ile ya Muungano”.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Natambua
kuwepo kwa rai ya kutaka Mwalimu Nyerere asitumiwe katika mjadala huu. Nionavyo
mimi ni vigumu kuacha kujadili fikra za Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume katika
jambo hili. Wao ndiyo wa mwanzo kujadili na kukubaliana kuwa mfumo wa Serikali
mbili ndiyo bora kwa nchi yetu. Iweje leo tunapozungumzia kuubadili, mawazo yao
yawe hayafai kutumika au hata kuzungumzwa. Hivi hasa mawazo ya nani pekee ndiyo
bora zaidi kutumika? Tutakuwa hatuutendei haki mjadala huu na sisi wenyewe
tunaoshiriki katika mchakato huu. Rai yangu kwenu ni kuwa mzitazame hoja zote
kwa marefu na mapana yake ili mpime kama zipo sababu za kuubadili muundo wa
sasa wa Muungano wa Serikali mbili na kuleta wa Serikali tatu. Na, kama zipo
mabadiliko hayo yaweje! Lazima mfanye uamuzi kwa utambuzi na hoja zenye
mashiko. (you must make an informed decision).
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Tume
imetoa sababu mbili kubwa za kupendekeza muundo wa Serikali tatu. Sababu ya
kwanza ni kwamba ndiyo matakwa ya Watanzania wengi kote Zanzibar na Tanzania
Bara. Inaeleza kuwa idadi kubwa ya Watanzania waliotoa maoni, yaani asilimia
60.2 wa kutoka Zanzibar wanaunga mkono muundo wa Serikali ya Mkataba, na
asilimia 61.3 wa kutoka Tanzania Bara wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu.
Sababu ya pili ni kwamba muundo huo unatoa majawabu ya uhakika na endelevu kwa
changamoto za muundo wa sasa wa Serikali mbili zinazonung’unikiwa na watu wa
pande zetu mbili za Muungano.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Sababu
hizi mbili kuu zilizotolewa na Tume zimezua mjadala mkali katika jamii. Wapo
wanaokubaliana na Tume na wapo wasiokubaliana nayo. Wapo wanaosema Tume imesema
kweli kwamba Watanzania wengi wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu, hivyo
muundo wa Serikali tatu hauepukiki. Ndiyo matakwa ya wengi hivyo msemo wa
Kiswahili usemao wengi wape uheshimiwe.
Lakini
wapo wanaodai kuwa takwimu za Tume hazionyeshi ukweli huo. Wanasema kuwa
taarifa ya Tume imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni yao kwa Tume kwa mdomo
na maandishi walikuwa 351,664. Kati yao ni wananchi 47,820 au sawa na asilimia
13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano hivyo wakauzungumzia. Wananchi
303,844 au sawa na asilimia 86.4 muundo wa Muungano kwao halikuwa tatizo, ndiyo
maana hawakuuzungumzia kabisa. Wanahoji kuwa iweje leo asilimia 13.6 ya
Watanzania wote waliotoa maoni wageuke kuwa ndiyo Watanzania walio wengi!
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Wanasema
pia, kwamba mbona Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk. 66 na 67),
inaonesha kwamba kati ya hao watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu Muungano, ni
watu 17,280 tu ambao ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo waliotaka muundo wa
Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali mbili, asilimia 25.3
walipendekeza Serikali ya Mkataba na asilimia 7.7 walipendekeza Serikali moja.
Hii hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu msingi wake upi?
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Takwimu
za Tume (uk. 57) zinaonyesha, vilevile kuwa Tume ilipokea maoni 772,211. Kati
ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia
88.6 hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine. Hivyo basi wanahoji pia
kwamba kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo linalowakera Watanzania wengi,
lingedhihirika kwenye idadi ya watu waliotoa maoni na kwenye idadi ya maoni
yaliyotolewa. Yote hayo hayakujitokeza. Waliouzungumzia Muungano walikuwa
asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa maoni na maoni yanayohusu Muungano
yalikuwa asilimia 10.4 ya maoni yote. Hivyo basi, wanauliza “usahihi wa hoja ya
Watanzania wengi kutaka Serikali tatu uko wapi?”
Changamoto
za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa
Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Kama
nilivyokwishagusia awali, sababu ya pili ambayo Tume inatoa kuhusu kufaa kwa
muundo wa Serikali tatu ni kwamba mfumo huu unajibu changamoto nyingi za muundo
wa Serikali mbili. Tume imeainisha vizuri changamoto za muundo wa Serikali
mbili. Kwa upande wa Zanzibar wanalalamikia kile kinachoitwa Tanzania Bara
kuvaa koti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo kutumia mamlaka ya
Serikali ya Muungano kujinufaisha yenyewe.
Fursa hiyo Zanzibar hainayo. Aidha,
wanasema mipaka na mamlaka ya Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano, na
kwa mambo ya Tanzania Bara haijaainishwa vizuri ikaeleweka. Wazanzibari pia,
wanazungumzia mkanganyiko kuhusu ugawanaji wa mapato, na jinsi ya kuchangia
shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar. Vilevile, wanalalamikia Rais wa Zanzibar kuondolewa kuwa Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Aidha,
kuna malalamiko kuwa orodha ya mambo ya Muungano iliyoongezwa kutoka mambo 11
mwaka 1964 mpaka 22 mwaka 1992 imepunguza uhuru wa Zanzibar kwa mambo yake ya
ndani.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa
upande wa Tanzania Bara, Tume inaeleza kuwepo kwa manung’uniko kuwa Muungano wa
Serikali mbili umepoteza utambulisho wa kihistoria wa Tanganyika na fursa ya
watu wa upande wa Tanzania Bara kutetea maslahi yao ndani ya Muungano. Wanasema
Zanzibar sasa imekuwa nchi huru; ina bendera yake, wimbo wake wa taifa na
Serikali yake. Aidha, wanasema Zanzibar imebadili Katiba na kujitambulisha kama
nchi na kuchukua madaraka ya Bunge la Muungano, kwa vile Sheria zinazotungwa na
Bunge lazima zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi kupata kibali cha kutumika
Zanzibar.
Wananchi wa Tanzania Bara pia wanalalamikia kutokuwa na haki ya
kumiliki ardhi Zanzibar wakati wenzao wa kutoka Zanzibar wanayo haki hiyo
Tanzania Bara. Na wao vilevile wananung’unikia mkanganyiko kuhusu ugawaji wa
mapato na jinsi ya kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli za Muungano
baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hizi ndizo baadhi ya
changamoto ambazo Tume inaona jawabu lake ili kuzitanzua ni kubadili muundo wa
Muungano kuwa wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa.
Faida
za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imefafanua kwamba mfumo wa Serikali tatu utagawanya
vizuri madaraka kati ya mamlaka tatu za Muungano. Unawezesha Washirika wa
Muungano kubaki na utambulisho wao wa kihistoria na kiutamaduni na hivyo,
utawezesha kuondoa hisia za Zanzibar kumezwa na Muungano. Pia unawezesha kila
upande wa Tanzania kuendesha mambo yake yasiyo ya Muungano kadri wanavyoona
inafaa. Vile vile unaweza ukaleta ushindani wa kimaendeleo baina ya washirika
na hivyo kusaidia kukuza maendeleo ya nchi.
Faida
za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Pamoja
na kuainisha changamoto za muundo wa Serikali mbili na kupendekeza kuwa muundo
wa Serikali tatu ndio utakaosaidia kuzitatua, Tume haikuacha kutambua manufaa
na mchango muhimu uliotolewa na muundo wa Serikali mbili kwa nchi yetu. Tume
inasema kuwa muundo wa Serikali mbili unapunguza gharama za uendeshaji wa
shughuli za umma. Umesaidia kujenga uhusiano na ushirikiano mzuri katika nyanja
mbalimbali baina ya wananchi wa pande zetu mbili za Muungano. Umezuia mkubwa
kummeza mdogo; na umedumisha Muungano mpaka kuufikisha hapa ulipo tangu
kuasisiwa kwake takriban miaka 50 iliyopita (1964). Aidha, umesaidia kudumisha
amani, umoja na utulivu hapa nchini.
Changamoto
za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Pamoja
na kuelezea ubora wa muundo wa Serikali tatu kama jawabu kwa changamoto za
Serikali mbili, Tume inakiri kuwa hata muundo huu nao una changamoto zake.
Kwanza kabisa, Taarifa ya Tume inaeleza kuwa kutakuwa na gharama kubwa za
uendeshaji wa shughuli za umma. Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba alitutoa hofu
kuhusu gharama ingawaje mwaka 1993, Mwalimu alikuwa na mawazo tofauti. Alisema
kwamba: “watu …wanaodhani kuwa gharama ya Serikali yo yote kati ya hizo
ingekuwa ndogo, (Waulizeni Wazanzibari) na wala gharama ya Serikali ya
Shirikisho isingekuwa ndogo hata bila gharama ya mambo yasiyo ya Shirikisho”.
Ni matumaini yangu kwamba katika mjadala wenu mtajipa nafasi ya kulitafakari
suala hili kubwa na nyeti.
Tume
imesema pia kwamba, Muundo huu, unaweza kuibua tatizo la uchangiaji wa gharama
za uendeshaji wa shughuli za umma baina ya nchi washirika. Vilevile, kuna
uwezekano wa kuwepo sera zinazokinzana au kutofautiana juu ya masuala ya msingi
ya nchi na kuzua mgogoro kati ya washirika wa Muungano na baina ya nchi
washirika na Serikali ya Muungano. Aidha, upo uwezekano mkubwa kwa muundo huu
kuleta tofauti za kimaendeleo baina ya pande mbili za Muungano kutokana na kila
upande kuwa na sera na mipango tofauti.
Tume
pia imeelezea hatari ya muundo wa Serikali tatu kukuza hisia za utaifa
(nationalistic feelings) kwa nchi washirika, hivyo kuweza kudhoofisha Muungano.
Muundo huu pia unaweza kuleta misuguano (paralysis and deadklocs in decision
making) katika kufanya uamuzi juu ya masuala muhimu ya kitaifa. Changamoto hizo
si tu zinaweza kuwa tishio kwa ustawi wa Muungano bali pia hata uhai wake. Kwa
ajili hiyo kuchagua muundo wa Serikali tatu kuna maana ya kufanya kazi ya ziada
ya kuzikabili changamoto hizi ili zisiue Muungano wenyewe. Changamoto ambazo si
ndogo hata kidogo.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Wanaounga
mkono muundo wa Serikali mbili wanasema kuwa kwa mlolongo huu wa changamoto
zilizoainishwa na Tume yenyewe, unadhihirisha kuwa muundo wa Serikali tatu
hautapunguza matatizo ya Muungano wetu bali utayaongeza maradufu kuliko ilivyo
sasa. Wanakiri kuwepo kwa changamoto katika muundo wa sasa wa Muungano. Hata
hivyo, wanaamini zinaweza kushugulikiwa na kupatiwa ufumbuzi bila ya kuhitaji
kuwa na Serikali ya tatu. Wanatoa mifano kadhaa ya jinsi Serikali zetu
zilivyoshughulikia changamoto za Muungano katika kipindi cha uhai wake na
mafanikio yaliyopatikana.
Katika
kushughulikia kero za Muungano, Serikali zetu mbili ziliunda Tume ya Shelukindo
mwaka 1992 na Kamati ya Pamoja ya Serikali zetu mbili mwaka 1993. Mambo mengi
yaliyoainishwa katika Tume ya Shelukindo na Kamati ya Pamoja yameshughulikiwa
na kupatiwa ufumbuzi. Kwa upande wa kero zilizoelezwa kwenye Tume ya
Shelukindo, ilipofikia mwaka 2006 yalikuwa yamebakia mambo 13 kati ya 31. Kwa
jumla, kwa kero zilizoibuliwa na Tume ya Shelukindo na Kamati ya Pamoja, hivi
sasa yamesalia mambo sita tu. Kimsingi ni mambo yahusuyo maslahi ya kiuchumi na
yote yapo katika hatua nzuri za kuyamaliza. Mambo hayo ni:
Mgawanyo
wa mapato:
(a)
Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki
(b)
Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu.
Utafutaji
na uchimbaji mafuta na gesi asili.
Ushirikiano
wa Zanzibar na taasisi za nje.
Ajira
kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano.
Usajili
wa vyombo vya moto.
Tume
ya Pamoja ya Fedha.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Serikali
zetu mbili zimeamua kwa dhati kutumia fursa ya mchakato huu wa mabadiliko ya
Katiba kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Mambo hayo ni matatu yafuatayo:
Utafutaji
na uchimbaji mafuta na gesi asili.
Ushirikiano
wa Zanzibar na taasisi za nje.
Tume
ya Pamoja ya Fedha.
Matatu
mengine yatamalizwa kwa kutumia taratibu za kiutawala. Hali kadhalika, katika
kipindi cha mpito kinachopendekezwa na Tume yaani 2015 – 2018 ni nafasi nzuri
ya kushughulikia masuala yenye migongano kati ya Katiba ya Zanzibar na ile ya
Jamhuri ya Muungano. Mimi naishi kwa matumaini na kwa vile tunayo dhamira njema
ya kuimarisha Muungano wetu, naamini tutaweza kuziondoa tofauti zilizopo.
Orodha
ya Mambo ya Muungano
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kuhusu
orodha ya mambo ya Muungano kuwa 22 badala ya 11 ya awali, napenda
kuwahakikishia kuwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
hazina kigugumizi wala upungufu wa dhamira ya kisiasa ya kuyapunguza yale
yanayopunguzika. Napenda kwanza kabisa, ieleweke kuwa kilichoongeza orodha hiyo
si hila za Serikali ya Muungano kutaka kupunguza madaraka ya Zanzibar kwa mambo
yake ya ndani. Na, wala siyo udhaifu wa viongozi wa Zanzibar katika kutetea maslahi
ya nchi yao. La hasha.
Pili,
naomba ieleweke kuwa, kila kilichoongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano
kilikuwa na sababu inayoeleweka, inayoelezeka na iliyokubalika na pande zote
mbili za Muungano. Hakuna hata jambo moja lililoingizwa kwenye Katiba kwa
kificho. Taratibu stahiki za kikatiba na kisheria zilifuatwa. Hoja
ziliwasilishwa Bungeni na kujadiliwa kwa uwazi na uamuzi ulifanywa na Bunge kwa
kuzingatia kanuni ya theluthi mbili ya kura za kila upande wa Muungano.
Kumbukumbu zipo katika Hansard za Bunge la Muungano, ambazo ziko wazi kwa kila
mtu anayetaka kuzisoma asome. Nashauri mkazisome ili mpate kujua ukweli na
undani wa kila kilichoongezwa na sababu za kufanya hivyo.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Nchi
zetu mbili zilipoungana mwaka 1964 na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
kulikuwa na mambo 11 kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Mambo hayo ni haya
yafuatayo:
Katiba
ya Jamhuri ya Muungano,
Mambo
ya Nje,
Ulinzi,
Polisi,
Hali
ya Hatari,
Uraia,
Uhamiaji,
Biashara
ya nje na mikopo,
Utumishi
katika Serikali ya Muungano,
Kodi
ya Mapato, Kodi ya Makampuni, Ushuru wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,
Bandari,
Mambo ya Anga, Posta na Simu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kati
ya mwaka 1965 na 1992 mambo ya Muungano yaliongezeka kutoka 11 hadi kufikia 22,
kimsingi kutokana na mambo mbalimbali yaliyotokea nchini na kwenye ukanda wetu
wa Afrika Mashariki. Pande zetu mbili za Muungano zilikubaliana kuwa mambo hayo
yaongezwe katika Katiba na taratibu za kisheria na Kikatiba zilifuatwa. Kwa
idhini yako naomba nitoe maelezo kwa ufupi kwa yale yaliyoongezwa na kitu
kilichosababisha mabadiliko hayo kufanywa.
Jambo
la kwanza kuongezwa, yaani la 12 lilikuwa ni “sarafu, mabenki na fedha za
kigeni”. Hii ilifanyika tarehe 10 Juni, 1965 kufuatia kuvunjika kwa Bodi ya
Sarafu ya Afrika Mashariki (East African Currency Board) mwaka 1964. Kwa ajili
hiyo, kila nchi mwanachama wa Jumuiya ililazimika kuwa na sarafu yake na
mipango yake ya kusimamia mambo yake ya kibenki na fedha. Serikali zetu mbili
zilikubaliana masuala hayo yashughulikiwe na Serikali ya Muungano na Muswada
husika wa Bunge uliidhinishwa kuwa Sheria na Mzee Abeid Amani Karume aliyekuwa
akikaimu Urais tarehe 10 Juni, 1965.
Tarehe
11 Agosti, 1967 yaliongezwa mambo yafuatayo kwenye Orodha ya Mambo ya
Muungano:-
(a)
Leseni za Viwanda na Takwimu, (Jambo la 13)
(b)
Elimu ya Juu, (Jambo la 14)
(c)
Jambo la 15 lilikuwa ni mambo yote yaliyokuwa kwenye Nyongeza ya 10 ya Mkataba
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nyongeza hiyo ilikuwa na mambo 27 ambayo
Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la uratibu. Mambo hayo ni pamoja na
Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki, Utabiri wa Hali ya Hewa, Utafiti,
Vipimo na Mizani, Huduma ya Usafiri wa Reli, Barabara, Usafiri wa Majini na
kadhalika.
Tarehe
22 Julai, 1968 “rasilimali ya mafuta, petroli na gesi asilia” iliongezwa kwenye
Orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa jambo la 16. Kimsingi Serikali ya Muungano
ilipewa jukumu la kuagiza mafuta ya petroli na gesi asilia kwa ajili ya nchi
nzima. Baada ya kupanga upya Orodha ya Mambo ya Muungano, suala la rasilimali
ya mafuta likawa la 15.
Tarehe
22 Novemba, 1973 Baraza la Mitihani la Taifa liliongezwa na kuwa jambo la 16.
Hii ilifuatia kuvunjika kwa Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki mwaka 1971
na hivyo nchi yetu kulazimika kuunda Baraza la Mitihani la Taifa mwaka 1973.
Mwaka
1984 yalipofanyika mabadiliko makubwa katika Katiba ya mwaka 1977, Orodha ya
Mambo ya Muungano ilipangwa upya. Mambo yaliyokuwemo kwenye Nyongeza ya 10 ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuorodheshwa kama Jambo la 15 katika Orodha ya
Mambo ya Muungano yalipunguzwa na kubaki matano. Mambo hayo yalipewa namba kama
ifatavyo:- Usafirishaji wa Anga kuwa Jambo la 17, Utafiti kuwa la 18, Utabiri
wa Hali ya Hewa kuwa la 19 na Takwimu kuwa la 20 na Mahakama ya Rufani ya
Tanzania ikawa jambo la 21.
Tarehe
17 Mei, 1992 likaongezwa jambo la “Uandikishaji wa Vyama vya Siasa” na kuwa
jambo la 22. Hii ilifuatia kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa na
hasa uamuzi kuwa vyama vitakuwa vya kitaifa.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Bila
ya shaka maelezo haya yatasaidia kuelezea nini kimeongezwa na mazingira ya
kuongezwa kwake ni yepi. Kulikuwepo na sababu za msingi na wala siyo hila ya
namna yo yote ile iliyofanywa na mtu ye yote mwenye nia mbaya na Zanzibar. Kama
tulivyoona mambo mengi yalihusu kilichokuwa kinatokea ndani ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Kila yalipotokea mabadiliko katika uendeshaji wa shughuli za
Jumuiya ya Afrika Mashariki, huduma zilizokuwa zikitolewa na Jumuiya
zilikabidhiwa Serikali ya Muungano kubeba kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa
kiuchumi. Yale yaliyokuwa yanagusa sehemu zetu mbili za Muungano yaliingizwa
katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Mengineyo yaliachiwa kila upande
kushughulikia ilivyoona inafaa. Kwa maana hii basi, mambo ambayo yalitokana na
uamuzi wetu wenyewe ni mawili tu. Mambo hayo ni rasimali ya mafuta na gesi
asilia (1968), na uandikishaji wa vyama vya siasa (1992).
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Ni
msimamo wa Serikali zetu mbili, tangu mwanzo mpaka leo kwamba, iwapo Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshajenga uwezo wake wa kufanya baadhi ya mambo
katika Orodha ya Mambo ya Muungano ipewe uhuru wa kufanya hivyo. Lililo muhimu
ni kuwa zisiondolewe tunu zenyewe za Muungano wetu. Ndiyo maana, mambo kama
vile bandari, takwimu, kodi ya mapato, leseni za biashara, utafiti na
mengineyo, yanasimamiwa na kuendeshwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
pamoja na kuwemo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Imekuwa hivyo kwa miaka
kadhaa sasa na imethibitika kuwa Zanzibar inayamudu. Ni makusudio yetu kutumia
fursa ya mchakato huu sasa kuyaondoa rasmi mambo hayo na mengineyo
tutakayokubaliana kutoka kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
Rasilimali
ya Mafuta na Gesi Asilia
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa
ajili hiyo tumekubaliana kuliondoa suala la rasilimali ya mafuta na gesi asilia
lisiwe jambo la Muungano. Jambo hili tulishakubaliana tangu wakati wa Rais
Amani Abeid Karume tuliondoe na hata alipokuja Rais Shein msimamo
haukubadilika. Kilichotuchelewesha kutekeleza ni kuibuka kwa fikra za kuwa na
mchakato huu wa Katiba mpya. Tuliona kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria wa
kuondoa jambo hili katikati ya mchakato huu, ingeweza kuzua matatizo yasiyokuwa
ya lazima. Tungeulizwa haraka ni ya nini tungeweza kukosa majibu.
Hatimaye
wakati wake wa kulimaliza suala hili sasa umefika. Misemo ya wahenga ya “subira
yavuta heri” na “kawia ufike” imetuongoza vyema tumefika mahali tunaweza
kufanya hivyo. Zipo sababu mbili zilizotushawishi kuamua kuitoa rasilimali hii
kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Kwanza kwamba, siku hizi Serikali haiagizi
mafuta. Kazi hiyo hufanywa na makampuni binafsi. Pili, kwamba, rasilimali ya
mafuta na gesi yakipatikana Zanzibar ni suala la kiuchumi ambalo lipo kwenye
mamlaka ya Zanzibar kama ilivyo karafuu, hiliki, mwani na kadhalika. Au kama
ilivyo dhahabu, gesi, pamba, kahawa na kadhalika kwa upande wa Tanzania Bara.
Hivyo, Zanzibar iachwe kumiliki rasilimali yake ya kiuchumi.
Zanzibar
na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Jambo
lingine muhimu ambalo Serikali zetu mbili zimelizungumza na kukubaliana tulitafutie
ufumbuzi ni kuhusu Zanzibar kupata fursa ya kujiunga na mashirika ya kimataifa,
kukopa na kupata misaada kutoka nchi za nje bila kizuizi. Kwa sasa fursa hiyo
ina vikwazo vya namna mbalimbali. Ni ukweli usiopingika kuwa jambo hili
limechangia kwa kiasi kikubwa kujenga hisia hasi kuhusu Muungano kwa upande wa
Zanzibar. Aidha, limechangia sana kuchafua hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar kwa
nyakati mbalimbali. Hata zile kauli kwamba Tanzania Bara imejificha kwenye koti
la Serikali ya Muungano, na kutaka itoke ionekane ili iache kunufaika
isivyostahili, zinazochangiwa sana na mazingira haya iliyonayo Zanzibar.
Serikali zetu mbili zinaamini kuwa mambo haya yakipatiwa ufumbuzi tutakuwa
tumeondoa kizingiti kikubwa katika ustawi wa Muungano wetu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
tumekubaliana kuwa, tutumie fursa za mchakato huu kuyamaliza mambo haya yaishe!
Bahati nzuri dhana iliyopo katika Ibara ya 65(2) ya Rasimu inatoa jawabu
mwafaka kwa tatizo hili. Tukikubaliana, itaipa Zanzibar “uwezo na uhuru wa
kuanzisha uhusiano na ushirikiano na jumuiya au taasisi yo yote ya kikanda na
kimataifa kwa mambo yaliyo chini ya mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya nchi”
bila kizuizi. Ni maoni ya Serikali zetu mbili kuwa fursa hiyo inaweza kutolewa
kwa Zanzibar bila ya kulazimika kuwa na muundo wa Serikali tatu. Hatuuoni
ulazima huo.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa
maoni yangu kitu kingine muhimu cha kufanya ni kuongeza msukumo,
utakaohakikisha kuwa Tume ya Pamoja ya Fedha inatimiza ipasavyo majukumu yake.
Wanaohusika na utekelezaji wa maamuzi yake wabanwe ipasavyo kutimiza wajibu
wao. Iwekwe mifumo na masharti katika sheria au Katiba ya kuwabana watekelezaji
kwa ajili hiyo. Hali kadhalika ihakikishwe kuwa, Akaunti ya Pamoja inaanzishwa
bila ajizi na kutumika na pande zote. Aidha, mfumo wa mawasiliano na
ushirikiano baina ya Serikali zetu mbili yaani Kamati ya Pamoja ya Serikali ya
Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, upewe nguvu ya kisheria na kama
hapana budi upewe nguvu ya Kikatiba. Tukifanya hivyo tutafanikiwa kuyaweka
mambo yote sawa hata bila ya kuhitaji kuunda Serikali ya tatu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Waheshimiwa
Wajumbe;
Katika
mjadala kuhusu mapendekezo ya kuwa na muundo wa Muungano wenye Serikali tatu,
wananchi wametoa maoni na mapendekezo mengi mazuri kuhusu changamoto za
Serikali tatu zilizoainishwa na Tume na namna ya kuzitatua. Tena yapo maoni ya
watu wanaopenda muundo wa Serikali tatu na wasiopenda muundo wa Serikali tatu.
Nawaomba myatafakari kwa uzito unaostahili. Yapo mambo muhimu ya kuyatafutia
ufumbuzi. Kwanza, kwa mfano ni ile hoja kwamba Serikali ya Muungano
inayopendekezwa haikujengeka kwenye msingi imara. Haina nguvu yake yenyewe za
kusimama. Inategemea mno ihsani ya nchi washirika. Kwa sababu hiyo inaweza
kuanguka wakati wowote, na Muungano kusambaratika, iwapo itakosa ihsani ya nchi
washirika. Tena inaweza kuwa hivyo hata kama ni mmoja wa washirika amefanya
hivyo.
Pili,
kwamba, haielekei Serikali hiyo ina chanzo cha uhakika cha mapato ya kuiwezesha
kusimama yenyewe na kutekeleza majukumu yake. Ushuru wa bidhaa unaopendekezwa
unatiliwa shaka kuwa hautatosheleza mahitaji. Pia, kwamba, hakuna uhakika wa
fedha hizo kupatikana kwa vile, Serikali ya Muungano haina chombo chake
chenyewe cha kukusanya mapato hayo. Itategemea vyombo vya nchi washirika
kuikusanyia na kuipelekea. Kuna hatari ya shughuli za Serikali ya Muungano
kusimama wakati wo wote au hata kusimama kabisa kwa sababu ya nchi washirika
kuchelewa au kushindwa kuwasilisha makusanyo ya kutoka kwao.
Bahati
mbaya Serikali ya Muungano haina uwezo wala nyenzo za kuhakikisha kuwa mapato
yake yanawasilishwa. Serikali hiyo haina mamlaka ya kuzibana nchi washirika
kuwasilisha au kuziwajibisha zisipofanya hivyo. Katika mazingira hayo ni rahisi
kwa Serikali ya Muungano kukwama na kushindwa kutekeleza majukumu yake. Huu ni
muundo ambao inakuwa ni rahisi sana kwa Muungano kuvunjika.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Katika
Rasimu ya Katiba, Serikali ya Muungano inapewa fursa ya kukopa kama chanzo cha
kujipatia mapato ya kuendesha shughuli zake. Lakini, kwa sababu ya kukosa
rasilimali zake yenyewe, huenda ikawa vigumu kwa Serikali hiyo kukopesheka. Kwa
jumla hii ni Serikali ambayo ukuu wake hauna nguvu iliyo thabiti, na watu
wengine wanaona kama vile ukuu huo haupo kabisa. Akitokea kiongozi ye yote wa
nchi washirika akatunisha misuli dhidi ya Rais wa Muungano au kupinga maamuzi
ya Serikali au chombo cha Muungano, Rais na Serikali yake watakuwa hawana lo
lote la kufanya. Kwa kweli uhai wa Muungano katika muundo wa Serikali tatu ni
wa mashaka makubwa.
Hofu
hizi kuhusu udhaifu wa Serikali ya Muungano chini ya mfumo wa Serikali tatu
unaopendekezwa, zinawasumbua hata wale wanaopendelea mfumo wa Serikali tatu
kuwepo. Wao wangependa iwepo Serikali ya Muungano yenye nguvu na inayoweza
kusimama yenyewe kwa kujitegemea. Wanaona kilichopendekezwa hakitoi matumaini
hayo. Hii ina maana kuwa lazima mawazo bora zaidi yatolewe ili kupata Serikali ya
tatu yenye ukuu unaoonekana na inayoweza kusimama yenyewe bila kuwa tegemezi na
egemezi kwa nchi washirika. Pia inaweza kuwa nguzo ya kutegemewa na nchi
washirika. Bila ya shaka Bunge hili likiamua tufuate mfumo huo linaweza
kuonyesha njia ya kuondoa hofu hizo. Kwa waumini wa Serikali mbili wanaona kuwa
huu ni uthibitisho wa ubora wa muundo wa Serikali mbili.
Changamoto
za Hisia za Utaifa
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Katika
kuainisha changamoto za muundo wa Serikali tatu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imeyataja mambo mengine mawili makubwa ambayo ningependa Waheshimiwa Wajumbe
muyape tafakuri stahiki. Mambo hayo ni mosi, misuguano na mikwamo (deadlocks
and paralysis) katika kujadili na kufanya uamuzi kuhusu mambo muhimu ya
Muungano. Na pili, ni kuibuka kwa hisia za utaifa (nationalistic sentiments) wa
zamani kwa nchi washirika. Nawaomba myatafakari kwa makini sana mambo haya, kwa
sababu ya uwezo wake mkubwa wa kuhatarisha siyo tu ustawi na uhai wa Muungano,
bali hata usalama wa raia na mali zao. Naona hata Tume haikuweza kupata
ufumbuzi ulio mwafaka kabisa kwa changamoto hizi. Bila ya shaka katika mijadala
yenu Waheshimiwa Wajumbe mnaweza kusaidia.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Ni
lazima lifanyike kila linalowezekana kuhakikisha kuwa maamuzi hayakwami kwani
yakikwama maana yake shughuli za Muungano zitakuwa zimekwama. Kama
hazitakwamuliwa kwa wakati ustawi wa Muungano utaathirika. Ikishindikana kabisa
kupatikana ufumbuzi Muungano unaweza kuvunjika. Kuibuka na kukua kwa hisia za
utaifa (nationalistic feelings) kwa nchi washirika, yaani Utanganyika na
Uzanzibari ni tishio kubwa sana kwa uhai wa Muungano.
Hebu fikiria, watu
walioishi pamoja kidugu na kwa kushirikiana, kama watu wamoja na raia wa nchi
moja yaani Watanzania kwa miaka 50, kuja kujikuta uhusiano wao kuwa ni kati ya
Watanganyika na Wazanzibari na siyo kati ya Watanznaia. Kwa mujibu wa sensa
iliyopita takriban asilimia 90 ya Watanzania waliopo sasa wamezaliwa baada ya
mwaka 1964. Nchi wanayoijua ni Tanzania. Litakuwa ni jambo lenye mshtuko mkubwa
na athari zisizoweza kutabirika, watu hao watakapojikuta ni wageni wanaotakiwa
kutengenezewa utaratibu maalum wa kusafiri na kuishi wakiwa upande wa Muungano
ambao siyo kwao kwa asili. Wanakuwa wageni na fursa walizokuwa wanazipata
waendapo popote haiwi rahisi tena kuzipata.
Katika
mazingira hayo ni rahisi sana chuki kupandikizwa na watu waliokuwa ndugu mara
moja watajikuta maadui. Aidha, watu wanaweza kujikuta wakilazimika kurudi kwao
kwa asili ama kwa kufukuzwa au kwa sababu ya mazingira kuwa magumu kiasi cha
kuona bora waondoke. Watu hao wanaweza kulazimika kuondoka huku wakiacha nyuma
kila kitu walichokichuma maishani.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Changamoto
hizi kubwa mbili za mfumo wa Serikali tatu ambazo Tume imeziona, ni za kweli.
Si mambo ya kufikirika. Yale yaliyowakuta watu wenye asili ya Tanzania Bara ya
kuchomewa moto biashara zao Zanzibar mwaka 2012 na watu wenye hisia kali za
Uzanzibari, na kuwataka watu wa Bara waondoke Zanzibar, huenda yakawa madogo.
Matukio ya namna hii yanaweza kutokea pande zote mbili na kusababisha maafa
makubwa. Itaanza baina ya watu, baadaye itakuwa baina ya Serikali zetu mbili na
kuzifikisha nchi zetu mbili zilizokuwa ndugu na rafiki, kwa nusu karne, ghafla
kuwa maadui wasioombana chumvi na wasiotakiana heri. Umoja wetu utatetereka na
Muungano wetu unaweza kuvunjika. Kwa nini tufike huko?
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Sisi
viongozi tuliopewa dhamana ya kuamua kwa niaba ya wananchi wetu, hatuna budi
kuyapima mambo haya kwa umakini mkubwa ili tufanye uamuzi ulio sahihi. Tusije
tukajutia uamuzi wetu tutakapoona watu wanafukuzana, wanauana na mali zao
kuporwa. Na, tukifikia hatua hiyo Muungano kusambaratika halitakuwa jambo la
ajabu.
Kwa
kweli, unapoyatafakari haya, ni rahisi kuelewa kwa nini wazee wetu waasisi
waliamua walivyoamua. Waliona mbali. Tusipuuze fikra zao na maono yao. Kuna
hatari ya nchi yetu na watu wake kupoteza kila kitu tulichokijenga kwa miaka
50. Badala ya kujenga tunaweza kujikuta tumebomoa hata msingi katika nchi
washirika. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1993 alituasa kuhusu
hatari hiyo: “Hamuwezi kutenda dhambi kubwa namna hiyo bila adhabu… na adhabu
nyingine zimo mle mle ndani ya kitendo hazisubiri.”
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Siku
moja kiongozi mmoja wa juu wa madhehebu ya dini nchini aliniuliza: “Hivi
Serikali mbili zikiwa na matatizo jawabu ni kuongeza ya tatu? Si matatizo ndiyo
yatazidi? Je, matatizo yakizielemea hizo Serikali tatu si kila mtu atachukua
njia yake? Mtakuwa mmepoteza kila kitu. Mimi nawashauri msichoke kutafuta
majawabu kwa matatizo ya hizi mbili! Huko mnakotaka kwenda kuna hatari nyingi”.
Pengine
na ushauri huu wa mtu wa Mungu nao ni vyema kuupa nafasi na kuutafakari.
Kazi
Yenu Kubwa
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Mambo
ya kuyasemea ni mengi mno lakini kwa sababu ya ufinyu wa muda, nisingeweza
kuyazungumzia yote. Naamini, mtayaona katika kuipitia Rasimu na kwenye
majadiliano yenu. Napenda kusisitiza kwenu kuwa kazi iliyo mbele yenu ni kubwa
sana. Ni kubwa kwa maana mbili. Kwanza, jukumu lenyewe la kutunga Katiba ya
nchi ni zito sana. Taswira ya nchi yetu itakuwaje na itaendeshwa vipi kwa miaka
mingi ijayo iko mikononi mwenu. Ipeni nchi yetu hatima njema. Pili, ni kubwa
kwa maana ya uzito wa mambo ya kujadili na kuyafanyia uamuzi. Kwa ajili hiyo,
ni muhimu sana kuisoma Rasimu na Taarifa ya Tume kwa makini na kuzielewa.
Jipeni muda wa kutafakari kila neno, kila sentensi, na kila dhana ili muweze
kufanya uamuzi ulio sahihi. Mkifanya hayo mtakuwa mmeisaidia nchi yetu na
Watanzania wote kupata Katiba nzuri.
Nimefarijika
sana kusikia kuwa mtajigawa kwenye Kamati 12 wakati wa kujadili Rasimu. Huu ni
utaratibu mzuri kwani mkiwa katika vikundi vya watu wachache, mtakuwa na
mijadala ya kina zaidi. Watu wote wanaweza kupata fursa ya kutoa maoni yao, kwa
kila kifungu na kila jambo linaloibuliwa na kuzungumzwa. Kwa kufanya hivyo, mtatimiza
kwa ukamilifu jukumu lenu la kutunga Katiba. Wote mtakuwa mmeshiriki kujadili
kila sura na vipengele vyake vyote. Mkimaliza kazi yenu mtapokea kwa haki sifa
nzuri kama Katiba itakuwa nzuri, au lawama stahiki iwapo itakuwa kinyume chake.
Pongezi
kwa Mwenyekiti wa Muda
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Nitakuwa
mwizi wa fadhila kama nitamaliza hotuba yangu bila ya kutambua kazi nzuri
iliyofanywa na Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi,
alipokuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hili. Kazi yake haikuwa rahisi hata
kidogo, lakini kwa umahiri na ustadi mkubwa ameweza kufanikisha mambo kwa kiasi
ambacho anastahili pongezi zetu sote. Anastahili pongezi kwa sababu yeye
aliendesha Bunge hili bila ya kuwepo kwa kanuni. Tatizo hili hatakuwa nalo
Mwenyekiti wa Kudumu kaka yangu Mheshimiwa Samuel Sitta.
Napenda
pia kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa hatua
mliyofikia. Hata hivyo, mmechukua muda mwingi katika hatua ya awali hivyo hamna
budi kuongeza kasi. Naomba niwakumbushe kuwa mijadala yenu hii inafuatiliwa kwa
karibu sana na Watanzania. Wamewekeza sana matarajio yao kwenu. Hamna budi,
haiba na taswira ya uongozi muionyeshe wakati wote wa kuendesha mijadala yenu
kwa lugha na vitendo vyenu. Wakati wa semina na mjadala wa kupitisha Kanuni za
Bunge hili, baadhi ya wananchi wamekwazika sana na mwenendo wa baadhi ya
Wajumbe. Hawakutegemea kuyaona matendo waliyoyaona mkifanya na kusikia maneno
waliyoyasikia kutoka kwenye vinywa vya baadhi yenu.
No comments:
Post a Comment